Wanawake Jumuiya ya Kikristu Tanzania waeleza madhara ya siasa chafu

Kwenye ulingo wa siasa kuna siasa safi na siasa chafu. Siasa safi ni zao au tunaweza kusema ni matokeo ya ushiriki wa wananchi katika kuchagua viongozi walio na dhamira safi kwa ajili ya maendeleo yao. Siasa chafu ni zao la wananchi kuchagua viongozi katika misingi isiyo safi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Misingi ya rushwa na ghilba hufanywa na wanaotaka kuchaguliwa kwa lengo la kushawishi kuchaguliwa. 

Nao wananchi kwa kujua au kutojua hujiingiza katika mtengo wa kuwachagua viongozi wasiofaa na hatimae kupata viongozi wasio na malengo thabiti ya kuwakwamua wananchi hao katika changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Ukweli ni kwamba wahanga wakubwa wa siasa chafu ni wanawake kama inavyobainishwa na Ester Muhagachi, Afisa wa Programu, Idara ya Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Jinsia, Jumuiya ya Kikristu Tanzania (CCT,) alipokuwa akizungumza katika semina ya viongozi wanawake wa jumuiya hiyo kutoka maeneo mbalimbali nchini, semina iliyofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro. Mwandishi Diramakini anakupitia hatua kwa hatua endelea...

Semina hiyo iliwaleta pamoja wenyeviti na makatibu wa idara za wanawake katika makanisa yaliyo chini ya Jumuiya ya Kikristu Tanzania (CCT) ikiwa na malengo makuu matatu.

Mosi kuwajengea uwezo wanawake viongozi wa kidini kufahamu wajibu wao katika uchaguzi mkuu na pili kufahamu haki za jinsia katika mtazamo wa kikristu. Sambamba na hilo semina hiyo ililenga kuliombea Taifa ili lifanye uchaguzi wa amani na utulivu.

“ Panapotokea vurugu au vita, wanaoteseka ni akina mama na watoto. Hilo lipo wazi na tunaona mifano mahali pengi Duniani ambako vurugu hutokea. Akina mama na watoto ndio huwa wahanga wakubwa wa machafuko hayo.

Hivyo wanawake tuna kila sababu na ni wajibu wetu nyakati hizi za uchaguzi kuwa makini ili tuchague viongozi ambao hawataliingiza Taifa hili kwenye machafuko. Pia tuna kila sababu ya kupiga magoti na kuomba kwa unyeyekevu mkubwa ili Mungu alijalie alibariki na kulilinda Taifa letu Tanzania tufanye uchaguzi kwa kuzingatia misingi ya haki ambayo ndio kiini cha amani na utulivu,"anaeleza Ester Muhagachi.

Kauli ya Ester Muhagachi inaungwa mkono na Joyce Mekere, Katibu wa Umoja wa Wanawake Kanisa la Mennonite Tanzania mmoja ya viongozi wa idara za wanawake wa Kikristu waliohudhuria semina hiyo.

Mekere anawaonya wanawake kote nchini kuacha na kutojitumbukiza katika ushabiki wa kisiasa kwani ni jambo lenye madhara makubwa kwa mustakabari wa maendeleo ya wanawake wenyewe na Taifa kwa ujumla.

Mekere anasema kuwa dhana na dhima nzima ya uchaguzi ni kuamua mustakabari wa maisha ya baadae.

Anakitaja kipindi cha uchaguzi kuwa ni kipindi muhimu sana kwani ndicho kipindi ambacho wananchi wanapata fursa ya kusikiliza sera za wagombea, sera zinazohusu ustawi wao kiafya, kielimu, kilimo, miundombinu, biashara, ulinzi na usalama na yote yanahusu mwenendo wa maisha ya kila siku.
“Kuna tatizo moja kwa upande wa wanawake kipindi hiki cha uchaguzi.

Ukweli ni kwamba wanawake ndio wapiga kura. Wanawake hupiga kura kwa wingi kuliko wanaume. Tatizo ninaloliona hapa kwa wanawake wengi ni ushabiki bila kujua kile wanachokishabikia, kupembua na kuchambua kwa kina sifa na sera za wagombea,"anasema Mekere.

Mekere anaongeza kwa kusema kuwa, wanawake huwachagua wagombea kwa mtazamo wa kishabiki na kimakundi, jambo ambalo halitoi fursa kwa mtu mmoja mmoja kupata fursa ya kusikiliza na kuamua kulingana na sera za mgombea.

“Uchaguzi ni maisha. Ni mbegu inayopandwa na kuvunwa kwa mfululizo wa miaka mitano. Ni vema wanawake wakajikita katika kusikiliza kwa makini sera za wagombea na kuamua pasipo kufuata mkumbo na ushabiki kwani matokeo mabaya yanayotokona na kukosea kuchagua huwapata wanawake wenyewe kwa kiasi kikubwa,"amesema.

Mekere anatolea mfano wa ukosefu wa maji na huduma za afya. Anasema ni wajibu wa viongozi kuandaa na kusimamia sera ambazo zitafanikisha upatikanaji wa huduma hizo. Ikiwa huduma hizo hazitapatikana akina mama ndio huteseka zaidi.

“ Hebu fikiria ni akina mama wangapi wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma za afya wakati wa kujifungua au kupeleka mtoto hospitali? Hebu fikiria ni akina mama wangapi wanaoteseka kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji?

Fikiria pia ni watoto wangapi wa kike wanaoshindwa kumaliza shule kwa kuwa wanapata ujauzito kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shule na hatimae kurubuniwa na wanaume wakware.?

Mifano ipo mingi, inatosha tu kusema kuwa wanawake wanapaswa kuwa makini mno katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Waache ushabiki na kupokea rushwa za vitenge na vijisenti ambavyo havina msaada wowote kwa kesho ya maisha yao.

Wanawake wajikite katika kusikiliza, kupembua na kubaini sera bora za wagombea na hatimae kuchagua viongozi makini kwa ajili ya mustakabari wa maisha yao.” Anaeleza Mekere kwa uchungu

WANAWAKE NA NGUVU YA USHAWISHI

Mekere anawataja wanawake kuwa Mungu aliwajaalia uwezo mkubwa wa kushawishi lolote na likawezekana. Anasema kuwa hata nyakati za Biblia ipo mifano hai ya wanawake waliowahi kuwashawishi waume zao na kufanikisha. Anasema kuwa wanawake wanaweza kushawishi hivyo wajikite katika kushawishi yaliyo mazuri ili jamii inufaike kwayo.

“ Wanawake wana nguvu kubwa ya kumshawishi mwanaume na hata jamii kwa ujumla. Mwanamke ni mama, ni mke pia.

"Anaweza kumshauri na kumshwishi vema mume na hata mtoto. Tunayo mifano ya Delila wa Biblia alivyomshawishi Samson na hata Samsoni akataja siri za nguvu zake.

"Lakini pia upo mfano wa mwanamke Abigaili aliyemshawishi mfalme asimuue mumewe. Itoshe tu kusema kuwa wanawake wana nguvu kubwa ya kumshawishi mwanaume akabadili mwendo na mtazamo wake,"anasema Mekere.

Mekere anatoa wito kwa wanawake viongozi, wanaowania uongozi na wanawake wenye waume ambao wanawania uongozi kutumia nguvu hiyo ya ushawishi walio nayo kusisitiza amani, utulivu na ustawi wa maisha ya Watanzania.

“ Sauti za wake wa viongozi na zitumike sasa kuwashauri na kuwashawishi waume zao wasitende yaliyo kinyume na maadili ya jamii ili jamii isitumbukie katika machafuko.

"Wanawake viongozi na wanaowania uongozi waishawishi jamii yote kwa upana wake kuenenda kwa kufuata misingi ya sheria, kumwogopa Mungu na kufanya kampeni za kistaarabu na hatimae tupate viongozi wazuri watakao litumikia Taifa hili kwa weredi mkubwa ili tuzidi kujikwamua katika lindi la umaskini,"anasema Mekere.

IDADI YA WANAWAKE WALIO JITOKEZA KUGOMBEA

Akizungumzia idadi ya wanawake waliojitokeza kuwania uongozi katika nafasi mbali mbali, Mekere anasema kuwa hajafurahishwa na uchache wa wanawake waliojitokeza kugombea.

“Sijafurahishwa na idadi ndogo ya wanawake waliojitokeza kuwania uongozi katika nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Binafsi nilitaraji uchaguzi wa mwaka huu utazingatia ile sera ya 50 kwa 50. Lakini wanawake waliojitokeza ni wachache mno.” Anasema.

Mekere anaongeza kusema kuwa tamanio lake ni kuongezeka kwa idadi ya viongozi wanawake katika vyombo vya maamuzi kwa kuwa wanawake wameonesha kufanya vizuri katika nyanja za uongozi mahali pengi. Anasema kuwa usawa kijinsia katika vyombo vya maamuzi ungeharakisha zaidi kufikia maendeleo endelevu.

WANAWAKE NA MATUMAINI

Joyce Malimali ni Mratibu wa Huduma ya Wanawake Wakristu wenye Tumaini. Akizungumza katika semina hiyo amesema kuwa, wanawake wanakutana na changamoto nyingi. 

Changamoto hizo huwafanya baadhi kupoteza matumaini na kuishi kwenye mashaka, machozi na majonzi. Anatoa wito kwa wanawake wa Tanzania kumwomba Mungu ili awapatie Watanzania viongozi safi watakaorejesha tumaini.

“ Wapo wanawake waliopoteza matumaini kwa kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali. Changamoto za ndoa, mila potofu, mirathi, malezi, upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii kama vile, afya, maji, na elimu ni miongoni mwa mambo yanayowafanya wanawake kupoteza matumaini.

"Wakati huu wa uchaguzi ni wakati muafaka kwa wanawake kumwomba Mungu awape maono ya kumchagua kiongozi mcha Mungu, mwenye maono ya kuendelea kutatua changamoto zote zinazowakabili wanawake na jamii ya Kitanzania kwa ujumla wake ili kwa pamoja tuishi kwa amani na furaha.

"Wanawake wanapaswa kuchagua viongozi makini watakaofanya siasa safi, kwani kuwachagua viongozi ambao hawana mlengo wa kufanya siasa safi, waathirika namba moja wa matokeo ya siasa hizo chafu ni wanawake,"anasema Joyce.

No comments

Powered by Blogger.