Wavuvi watakiwa kuzingatia sheria, taratibu za uvuvi

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Mahmoud Kimbokota amewataka wavuvi mkoani Lindi kuzingatia sheria na taratibu zinasimamia uvunaji wa rasilimali za Bahari,anaripoti Mbaraka Kambona, Lindi.

Kimbokota aliyasema hayo alipokutana na timu ya Wataalamu wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOfish) walipokwenda kufanya ufuatiliaji na kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Mkoani Lindi Septemba 28, 2020.

Akizungumza na timu hiyo wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa SWIOfish, Kimbokota alisema kuwa  Wavuvi wanatakiwa kutambua kuwa uvuvi ni shughuli rasmi ya kujipatia kipato kama zilivyo shughuli nyingine, hivyo ni lazima waiheshimu na kuithamini.

“Wavuvi ni lazima wazingatie Sheria na taratibu, na wabadilike,ule uvuvi wa kutumia Mabomu, Kokoro na matumizi ya nyavu haramu waache, kila mvuvi awe mlinzi na mwalimu wa mwenzake, uvuvi haramu tuukomeshe sisi wenyewe,” alisema Kimbokota.

Wavuvi wakiendelea na kazi yao ya kuvua samaki katika moja ya maeneo hapa nchini. (Mtandano).

 “Uvuvi wa kutumia mabomu haufai, kwanza ni hatari kwa maisha yao, pia unaharibu mazalia ya samaki na mazingira ikiwemo uoto wa miti ya mikoko, miti ya mikoko ni lazima iachwe ili kulinda mazalia ya samaki baharini,”aliongeza Kimbokota.

Kimbokota aliishukuru Serikali kwa kupeleka mradi  wa SWIOfish Wilayani humo na kusema kuwa  jamii imeanza kubadirika, huku akiiomba Serikali kuendelea kuwawezesha wavuvi ili waweze kukuza mitaji yao na kupata zana za kisasa na kuachana na matumizi ya zana za kienyeji.

“Mradi  uendelee kutoa elimu kwa wavuvi ili maeneo yote ya Uvuvi yaendelee kuwa Salama na wavuvi wafanye shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu,”alisisitiza Kimbokota

Kimbokota aliongeza kwa kusema kuwa kutokana na uboreshwaji wa usimamizi wa rasilimali uliofanywa na mradi hususani katika eneo la doria, wavuvi wameanza kufuata sheria  na taratibu na  umesababisha kudhibitiwa vizuri kwa mapato ya Halmashauri.

“Kutokana na kuimarishwa kwa doria Halmashauri imeweza kudhibiti mapato yatokanayo na shughuli za uvunaji wa rasilimali za baharini, na mapato yamepanda kutoka shilingi Milioni 13. 5 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi Milioni 29.9 mwaka 2020, hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 50,”alifafanua Kimbokota

Aliendelea kueleza kuwa kufuatia doria hiyo kumeisaidia Halmashauri kuwa na Takwimu sahihi ya vyombo vya uvuvi vinavyotumika katika shughuli za uvuvi Wilayani humo, huku akisema kuwa doria imepelekea pia uvuvi wa kutumia mabomu, makokoro na nyavu haramu kupungua kwa kiasi kikubwa.

Aidha, aliushukuru mradi wa SWIOfish kwa kuamua kujenga Ofisi ya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Bahari (BMU) katika Kijiji cha Sudi huku akisema kuwa ofisi hiyo itasaidia kuimarisha ulinzi wa rasilimali za bahari na katika maeneo hayo na hivyo uvuvi haramu hauna muda mrefu utakoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news