Waziri Kalemani:Umeme sasa ni Kitongoji kwa Kitongoji

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizindua Mradi wa Ujazilizi Umeme Vijijini Fungu la Pili A katika Kijiji cha Bukene wilayani Nzega mkoani Tabora amesema kuwa,Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 190.7 kufikisha umeme kitongoji kwa kitongoji katika vitongoji 1,103 vya mikoa tisa, anaripoti Mwandishi Diramakini (Tabora).
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akizindua na kuwasha umeme katika moja ya nyumba ya mwananchi aliyenufaika na mradi katika Kijiji cha Bukene Migombani wilayani Nzega mkoani Tabora wakati wa uzinduzi wa mradi huo. (Diramakini).
Ametaja mikoa hiyo ambayo vitongoji vyake vitanufaika moja kwa moja na mradi huo kwa sasa kuwa ni Dodoma, Tabora, Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Singida, Pwani, Mbeya na Tanga.

“Uzinduzi huu wa Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili A ni muendelezo wa usambazaji umeme kwa wananchi wote. Kazi hii bado inaendelea, ndani ya miaka miwili toka sasa, tutakuwa tumevifikia vijijini vyote takribani 12,304 na vitongoji vyake vyote 64,839 nchini,”amesema Dkt.Kalemani.

Waziri Kalemani amewataka Watanzania ambao hawajafikiwa na huduma ya umeme kuwa watulivu kwani lengo na mipango ya Serikali ni kuwafikishia wananchi wote umeme ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo ndani ya kipindi cha miaka miwili toka sasa. 

“Tumepeleka umeme kijiji kwa kijiji na sasa tunakaribia kumaliza vijiji vyote nchini, sasa tunakwenda kitongoji kwa kitongoji, kaya kwa kaya mpaka tutakapowafikia wananchi wote,”amesema Waziri.

Kwa upande wa wananchi wa Bukene, waliohudhuria katika uzinduzi huo walionesha kufurahishwa na kufarijika sana na mradi huo wa ujazilizi kuanzia na kuzinduliwa kitaifa katika kijiji na vitongoji vyao vya Kijiji cha Bukene Migombani. 

Mwandu Igusule mkazi wa eneo la Bukene amesema kuwa, wanatarajia kutumia umeme huo kwa maendeleo yao ya kijamii pamoja na kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi na shughuli mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news