Wizara ya Elimu Zanzibar kuimarisha mkakati wa kuibua vipaji katika skuli

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema itaendelea kuibua vipaji vya michezo na sanaa katika Skuli ili kupatikana vipaji vitakavyoiletea sifa nchi, anaripoti Talib Ussi (Diramakini) Zanzibar.

Ameyasema hayo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma wakati wa usiku wa sanaa uliofanyika jijini Zanzibar.Waziri amesema, hatua hiyo itatokana kwa kushirikishwa vipaji vya wanafunzi kupitia michezo ya kuigiza,ngonjera, nyimbo,ngoma pamoja na vipaji vya utenzi.

Amewataka wazazi na walezi kuwashajiisha watoto wao kujihusisha na michezo ili kuweza kupata wachezaji bora ambao wataweza kuitangaza Zanzibar kupitia sanaa wanazozionesha.

Amesema, pamoja na kushiriki michezo, lakini elimu nayo isiachwe nyuma, kwani Serikali inajitahidi katika kuweka miundombinu imara ili kuweza kuzalisha wasomi zaidi hapa nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Dkt. Idrissa Muslim Hija amewapongeza walimu kwa kuwafundisha wanafunzi na kuibua vipaji vya watoto hao.

Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Hassan Khairalla Tawakal amesema, idara itaendelea kuimarisha na kufufua shughuli za michezo na sanaa katika nchi.


No comments

Powered by Blogger.