Airtel yashirikiana na WordRemit kuzindua huduma ya kupokea pesa Kimataifa

Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania imeshirikiana na WorldRemit, kampuni ya malipo ya Kimataifa kuwezesha wateja wa Airtel Money kupokea pesa moja kwa moja kwenye akaunti zao za Airtel Money kutoka nje ya nchi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kupitia ubia huu wa Airtel Money na World Remit wateja sasa wataweza kupokea pesa kutoka nchi zaidi ya 50 duniani zikiwemo Merakani, Uingereza, Australia, Sweden, Canada, Ujerumani, Norway, Uholanzi, Denmark na Ubelgiji. Hii itachangia kukua kwa huduma za Kifedha kwa mtandao na kurahisisha maisha ya wateja wa Airtel Money.

Mkurugenzi wa Airtel Money, Isack Nchunda na Meneja Mkazi wa WorldRemit Tanzania Cynthia Ponera wakizindua rasmi Kampeni ya VUKA BODA ya kuwawezesha wateja wa Airtel Money wa kupokea Pesa toka nchi zaidi ya 50 Duniani wakati wa hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 6,2020 wakati wa kutangaza hatua hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Airtel Money Tanzania, Isack Nchuda amesema, "Hii ni Wiki ya Huduma kwa wateja ambapo Airtel tunaingia ubia na WorldRemit ili kupanua zaidi huduma ya Airtel Money.

"Huduma hii tunayozindua leo inawaunganisha wateja wetu wanaotumia simu kufanya miamala na Dunia na kuwezesha kufanikisha ndoto zao. Mteja ataweza kupokea pesa papo hapo kwenye akaunti yake ya Airtel Money kutoka kwa ndugu au marafiki nje ya nchi.

"Huduma hii ni salama na ya uhakika na itapanua upatikanaji wa huduma ya kupokea au kutuma pesa kwa wateja wetu katika maeneo ya mijini na vijijini, kwani sasa wanaweza kupokea fedha kutoka popote duniani moja kwa moja kwenye akaunti zao za Airtel Money bila ya kuwa na akaunti ya benki au huduma ya intaneti.

Ushirikiano wetu na WorldRemit utachangia sana kutimiza dhamira yetu ya kutoa huduma za kipekee, rahisi na nafuu kwa wateja wetu. Uzinduzi wa ushirikiano huu kati ya WorldRemit na Airtel Money ni ushahidi mwingine kwetu kwamba tumedhamiria kukuza na kuwa suluhisho la kutoa huduma bora ya fedha kwa mtandao hapa nchini pamoja na kuweka usawa kwa jamii ya mjini na vijijini.

Mkurugenzi wa Airtel Money, Isack Nchunda akizungumza wakati wa kutangaza ushirikiano wa Airtel Money na Kampuni ya Malipo ya Kimataifa ya WordRemit ya kuwezesha wateja wa Airtel Money kupokea Pesa moja kwa moja kutoka nchi zaidi ya 50 duniani wakati wa hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jijini . Kushoto ni Meneja Mkazi Tanzania Cynthia Ponera.
WorldRemit inarahisisha kutuma pesa moja kwa moja kwenye akaunti za Airtel Money hapa nchini Tanzania kutoka nchi zaidi ya 50 duniani. Wateja wanaweza kupakua 'applikesheni' au kutengeneza akaunti ili kuanza kutumia huduma hii na kuanza kutuma au kupokea fedha kwa familia na marafiki.

“Tunayo furaha kufanya kazi na Airtel Tanzania kuhakikisha kuwa Watanzania wanaweza kupata msaada wa kifedha kutoka kwa familia na marafiki zao walio nje ya nchi. Ushirikiano huu baina ya WordRemit na Airtel Money utaweza kuwapa wateja nafasi ya kufanya mambo mengi zaidi wakati wa kutuma au kupokea fedha kimataifa kwani tunatoa huduma ambayo ni ya haraka, salama na ya uhakika,"amesema Cynthia Ponera ambaye ni Meneja Mkazi wa WorldRemit Tanzania.

Huduma za kifedha kwa njia ya mtandano zimewaza kusaidia kupunguza gharama za kutuma au kupokea fedha, kuongeza unafuu pamoja na kurahishisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa mtu binafsi au hata biashara. 

Kwa mtu anayepokea fedha kutoka nje ya nchi kwa sasa haitaji tena kusafiri umbali mrefu kwenye matawi ya benki ili aweza kupata fedha zake. Ushirikiano katika ya Airtel Money na WorldRemit utapanua matumizi Airtel Money pamoja na kukuza malipo ya dijitali.

Airtel Money Tanzania kwa sasa imeunganishwa na makampuni zaidi ya 1000 pamoja na watoa huduma mbali mbali, vile vile Airtel Money imeunganisha zaidi ya taasisi 40 za kifedha. 

Airtel Tanzania inazidi kupanua huduma zake kote nchini kwa kasi kwani mpaka sasa tunayo maduka ya Airtel Money 'branches' zaidi ya 1800 yanayotoa huduma mbalimbali pamoja na kuuza bidhaa zote za Airtel.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news