Anayeanzisha fujo Dunia itamtenga asema Rais Shein, azindua Kongamano la Amani Kitaifa

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Ali Mohamed Shein amesema juhudi za Serikali katika kuwahamasisha na kushirikiana na wananchi pamoja na Asasi mbali mbali kwa lengo la kudumisha amani, ni utekelezaji wa miongozo ya Ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 na ile ya 2020-2025, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Alhaj Dk. Shein amesema hayo leo Oktoba 7,2020 katika uzinduzi wa Kongamano la Amani Kitaifa, lililofanyika katika ukumbi wa Dk.Ali Mohamed Shein uliopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhubiri umoja na mshikamano na kupinga ubaguzi wa aina zote na kuliweka suala la kulinda na kudumisha amani kuwa kipaumbele chake katika Ilani zilizopita na zitakazokuja.

Alhad Dk. Shein alinukuu kifungu vya Ilani ya 2015-2020 (Ibara ya 127), kinachobainiusha dhamira ya kuendeleza sera ya kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar katika kipindi cha 2015 -2020 CCM pamoja na kuendelea kuwa muumin wa kweli wa amani na utulivu ili kuimarisha mafanikio yaliokwisha kupatikana.

Alisema Chama hichio kimeielekeza Serikali kuendeleza jitihada za kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa amani, umoja na mshikamano ili kujenga mazingira ya kuaminiana, kuvumiliana na kushirikiana katika masuala mbali mbali ya kijamii.

Aidha, alisema kimeielekeza serikali kuendelea kupiga vita na kudhibiti vitendo vya ubaguzi vinavyojitokeza katika sehemu za utoaji huduma za kiuchumi, kisiasa na kijamii miongoni mwa wananchi.

Alhaj Dk. Shein alisema Kongamano hilo ni muhimu kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuzingatia kuwa maudhui yake makuu yanahusiana na wajibu wa Serikali wa kulinda amani na usalama kama ilivyoelezwa ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Alieleza kuwa Katiba ya Zanzibar ya 1984 kifungu cha 9 (1) na (2) b na c kimebainisha Zanzibar itakuwa nchi ya Kidemokrasia, ambapo usalama na hali nzuri kwa wananchi itakuwa ndio lengo kubwa la Serikali pamoja na kuhakikisha wananchi wanashiriki katika serikali yao.

Alisema kazi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kutunza amani iliopo pamoja na kuwashughulikia wale wote watakaovuruga amani hiyo.

Alisema katika kipindi cha uchaguzi nchi nyingi Duniani hukumbwa na majaribio yenye kuashiria uvunjifu wa amani, ambapo baadhi yake hushindwa kudhibiti matokeo hayo na kupata athari mbali mbali, ikiwemo za kiuchumi.

Aidha, alisema athari nyingine zinazopatikana kutokana na uvunjifu wa amani ni kwa baadhi ya vyama vya siasa kufanya kampeni zenye kuwagawa watu kwa misingi ya dini zao, makabila, uwezo au sehemu wanazotoka.

Alitumia fursa hiyo kutoa shukran za dhati kwa wananchi wa Zanzibar kwa mashirikiano makubwa waliyompa katika kulinda na kudumisha amani ya nchi na kusema juhudi hizo zimewezesha kupanga na kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kupitia sekta zote za kuchumi na kijamii.

“Miradi mbali mbali ya maendeleo ni matokeo ya kufanyakazi kwa bidii na katika mazingira halisi ya amani na utulivu uliopo,"alisema.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kutafakari na kuepuka makosa ya kuwachaguwa viongozi wasio na dhamira ya kuendeleza umoja na mshikamano wa Wazanzibari.

Aliwataka wananchi kuepuka kuwachaguwa viongozi wasio na uwezo au uzoefu katika kulinda na kudumisha amani, kwani lengo lao ni kuwagawa.

Aidha, alisisitiza kuwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni Taifa huru na lililo salama, hivyo kazi ya kuendeleza mambo hayo ni ya wananachi wote.

Alisema lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 ssio kuleta fujo , bali ni kudumisha Uhuru na kubainisha kuwa hakuna mbadala wa amani, hivyo akawataka wananchi kutokubali kuvurugwa.

Alhaj Dk. Shein aliwataka wananchi kuwataaa viongozi wanaopinga Muungano, akimaanisha kwamba viongozi hao wanapinga Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, hivyo hawafai kuiongoza nchi.

Alisema Umoja wa mataifa (UN) uliunda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kusimamaia amani duniani, “dunia nzima haitaki vita, hakijaanzishwa chombo cha Dunia kinachoshughulikia fujo………anaeanzisha fujo dunia itamtenga”, alisema.

Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa nchi zote Duniani zina Serikali zao na kufuata Katiba na sheria zilizotungwa ikiwa ni mihimili ya kuongoza Dola, hivyo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia sheria na Katiba yake na haitachelea kuwachukulia hatua watu wote watakaokwenda kinyume, iwe kabla au baada ya uchaguzi.

Dk. Shein alibainisha furaha yake kwa hatua zilizochukuliwa na Kamati ya Amani Kitaifa ya kuanda kongamano hilo, wakati huu Taifa likikaribia kuelekea kwenye Uchaguzi mkuu, hivyo akawapongeza viongozi wote waliofanikisha maandalizi ya kongamano hilo.

Mapema, Makamo wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd aliwataka Wazanzibari na Watanzana kwa ujumla kuienzi amani iliopo, kwa kutambua kuwa kuna watu wengi wanaolionea wivu Taifa hili kutokana na tunu hiyo adhimu.

Aliwataka viongozi wa dini zote nchini na wadau wengine kuungana kwa pamoja na kupambana na wale wote wenye nia ya kutaka kuvuruga amani iliopo.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kupendana, kushirikiana na kuvumiliana, sambamba na kuepuka vishawishi.

Nae, Mgombea wa Kiti cha Urais kupitia CCM, Dk. Hussein Mwinyi katika salamu zake, alisema wakati huu vyama vya siasa vikinadi sera zao kuelekea uchaguzi mkuu baadae mwezi huu, ni vyema kusisitiza uwepo amani nchini, kwa kigezo kuwa hakuna maendeleo yoyote yatakayoweza kupatikana bila amani.

Alisisitiza kwa kusema kuwa jukumu la kuhubiri amani sio suala la viongozi wa dini au viongozi wa vyama vya siasa pekee, bali ni la wananchi wote.

“Amani huletwa na utulivu wa wananchi wake na sio kundi kubwa la askari au vifaa vya kivita”, alisema.

Dk. Mwinyi aliushukuru Uongozi wa Kamati ya Amani Kitaifa kwa kazi kubwa ya kuhubiri amani nchini jambo linalopaswa kuungwa mkono na kila mwananchi, huku akiahidi Serikali ijayo kuendelea kuijengea uwezo kamati hiyo.

Aidha, Mgombea wa nafasi ya Urais kupitia chama cha ADC Hamad Rashid Mohamed, alisema nchi nyingi za Kiafrika zimeingia katika migogoro na uvunjifu wa amani kutokana na uchu wa madaraka wa baadhi ya viongozi wake pamoja na kugombea rasilimali za Taifa.

“Duniani hakuna tunu zaidi ya amani, watu wanatumiwa kwa lengo la kuwanufaisha watu wengine “, alisema.

Alitoa wito kwa Wazanzibari kuendelea kushirikiana na kuungana kwa lengo la kupambana na watu wenye kiu ya madaraka.

Vile vile, mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ADA TADEA Juma Ali Khatibu akitoa salam zake katika kongamano hilo, aliwataka Wazanzibari kuithamni amani iliopo kama mboni za macho yao, kabla na hata baada ya uchaguzi mkuu, sambamba na kukemea kwa nguvu zote kauli za wanasiasa wanaoshajiisha uvunjifu wa amani kwenye majukwaa.

Alitoa indhari dhidi ya kauli za baadhi ya viongozi wanaowahamasisha wanachama na wafuasi wao kwenda kupiga kura siku tarehe 27 Oktoba, 2020, il-hali sio waliolengwa wa zoezi hilo walioidhinishwa na Tume hya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Wakati huo huo, akisoma dua ya ufunguzi wa kongamano hilo Mufti mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Ka’abi alimuomba Mwenyezi Mungu amzidishie hekima na busara Rais wa Zanzibar na Mwenyekit wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kipindi hiki akimalizia muda wake wa uongozi na baada ya kustaafu.

Aidha, alimitakia ushindi mkubwa na ulio wazi mgombea wa kiti cha Urais kupitia Chama cha Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi.

Post a Comment

0 Comments