NEC yamsimamisha Tundu Lissu kwa siku saba

"Leo Oktoba 2, 2020 Kamati ya Maadili ya Kitaifa imesikiliza malalamiko dhidi ya Mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

"Malalamiko yaliwasilishwa na Chama cha NRA na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Chama cha NRA wakilalamikia kitendo cha mgombea wa kiti cha kiti cha Rais kupitia CHADEMA kutoa maneno ya uchochezi yasiyothibitika;

Katibu wa Kamati ya Maadili ya Kitaifa, Emmanuel Kawishe ameyabainisha haya leo Oktoba 2, 2020 baada ya wajumbe wa kamati kukutana, anaripoti Mwandishi Diramakini (diramakini@gmail.com).

"Ambapo akiwa mkoani Mara, alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameitisha kikao cha wasimamizi wa uchaguzi nchi nzima ili kuhujumu uchaguzi. Pia imeelezwa kuwa alitoa maneno ya kichochezi na ya kudhalilisha kinyume na maadili ya uchaguzi mkoani Geita.

"Barua ya kumtaka kujibu tuhuma iliwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA kwa mujibu wa taratibu. Katibu Mkuu wa CHADEMA alijibu kuwa, malalamiko hayakihusu chama, hivyo, mgombea na chama ni vitu viwili tofauti.

"Pamoja na kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA alijibu barua ya malalamiko kuwa apelekewe Tundu Lissu mwenyewe, Kamati ya Maadili imeridhika kuwa taarifa kuhusu malalamiko ya ukiukaji wa maadili iliwasilishwa kwa mlalamikiwa kwa mujibu wa taratibu kwa kuzingatia mashariti ya Ibara ya 39 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambapo Bwana Tundu Lissu alidhaminiwa na CHADEMA kugombea kiti cha Rais.Hivyo, barua ya malalamiko kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu ni sahihi kabisa," ameeleza Katibu huyo kupitia taarifa iliyoonwa na Mwandishi Diramakini.

Amesema, "Kamati imejiridhisha kuwa, kitendo cha mlalamikiwa kutojibu malalamiko na kuitaka kamati impelekee mgombea malalamiko yeye mwenyewe si sahihi, kwa kuwa malalamiko yote ya maadili yaliwasilishwa kwa Katibu Mkuu na haijawahi kuamuliawa vinginevyo.

"Hivyo, wajumbe 11 kati ya 15 wamekubali kuwa malalamiko yamezingatia utaratibu na wajumbe wawili kati ya 15 wamesema uwasilishaji wa malalamiko haukufuata taratibu. Kwa maania hiyo, kamati imeridhia kuwa malalamiko yaliwasilishwa kwa mujibu wa taratibu.

"Baada ya majadiliano ya kina, Kamati imekubali kuwa,Tundu Lissu amekiuka maadili ya uchaguzi kwa kutoa lugha ya kichochezi na tuhuma zisizothibitika kinyume cha kanuni 2.1(a), (b), (d) na (n) na kanuni za maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2020.

"Hivyo, baada ya majadiliano ya kina na uchambuzi wa maadili ya uchaguzi, ambayo wawakilishi wa CHADEMA wameshiriki kikamilifu, Kamati ya Maadili ya Kitaifa imeamua kwa mamlaka iliyopewa chini ya Kanuni ya 5.11(c) na (e) ya Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Mdiwani ya mwaka 2020 imemsimamisha kufanya kampeni Tundu Lissu, mgombea kiti cha Rais kupitia CHADEMA kwa siku saba kuanzia tarehe 3 Oktoba, 2020 hadi tarehe 9 Oktoba,2020.

"Hivyo, mgombea huyo haruhusiwi kufanya kampeni za uchaguzi mpaka atakapomaliza adhabu yake. Ana haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa,"Katibu wa Kamati ya Maadili ya Kitaifa, Emmanuel Kawishe ameyabainisha haya leo Oktoba 2, 2020 kupitia taarifa iliyoonwa na Mwandishi Diramakini (diramakini@gmail.com).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news