CHADEMA kumpangia Tundu Lissu kazi nyingine

Leo Oktoba 4,2020 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Freeman Mbowe ametoa tamko kupitia mkutano wa waandishi wa habari,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Tamko la leo ni kuhusu maazimio ya Kikao Maalum cha Kamati Kuu ya chama kilichoketi Oktoba 3,2020 na kumalizika usiku jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Mkutano huo umewakutanisha pamoja pia viongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini humo.

"Ndugu wanahabari, ninapenda kuwaeleza Watanzania kupitia ninyi waandishi wa habari mambo kadha wa kadha yaliyojiri katika kikao chetu cha Kamati Kuu ya chama kilifanyika katika Ukumbi wa Bahari Beach Hotel siku ya jana kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane.

"Kikao kilikuwa na ajenda mahsusi moja ambayo ni kujadili mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa Urais, Wabunge, Rais wa Zanzibar, Wawakilishi pamoja na Madiwani wote kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani.

"Kamati Kuu imeridhika na mwenendo wa misafara ya kampeni ya mgombea wetu wa Urais na mgombea mwenza ukiondoa matukio machache ya...yaliyofanyika katika maeneo ya Nyamongo kwa upande wa mgombea wetu wa Rais na tukio la msafara wa mgombea mwenza kupigwa mabomu katika mji wa Ifakara.

"Pili kamati kuu imeitafsiri sana na kuitathmini Tume ya Taifa ya Uchaguzi na baadhi ya maamuzi yake na mwenendo wake. Kamati kuu imesikitishwa na kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuengua wagombea 36 wa ubunge, 35 wakitoka Tanzania Bara na mmoja kutoka visiwani na kuengua wagombea udiwani wetu 577.

"Tunatambua kwamba uchaguzi wote husimamiwa na sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, vilevile tunatambua sababu mbalimbali zilizotolewa na tume hazina mashiko ya kisheria, hazina mashiko ya kimantiki, zinavunja mfumo wote wa kidemokrasia katika nchi.

"Kwamba wagombea wote wa CCM hakuna hata mmoja aliweza kuenguliwa hata wale ambao sisi tulikata rufaa dhidi yao kwa makosa ya msingi na wazi.

Tume imetoa adhabu mbalimbali zisizo za msingi, zisizo za kidemokrasia bila kutia maanani kipindi cha uchaguzi ni kipindi kifupi sana.

Kipindi cha kampeni, kwa mfano mgombea wa CHADEMA wa kiti cha ubunge cha Ubungo, baada ya mchakato kuanza alikatiwa rufaa kwa hiyo hakuruhusiwa kufanya kampeni kwa wiki mbili na nusu kwa sababu ilikuwa haijatoa rufaa yake, baada ya wiki moja, Chama Cha Mapinduzi kikakata rufaa na tume tena ikamsimamisha kwa wiki nyingine moja, wamemchelewasha kwa wiki tatu.

Mgombea wetu wa ubunge Same Magharibi alifungiwa kwa wiki mbili, hatujasikia mgombea wa Chama Cha Mapinduzi akisimamishwa.

Tume imeendelea kuchelewesha majibu katika majimbo kadhaa, jimbo la Iramba Magharibi lenye mgombea Jesca Kishoa, dada makini kabisa, madiwani wake wote wameenguliwa katika uchaguzi kwa sababu ambazo hazina msingi kabisa.

Tumepeleka malalamiko kadhaa ya makosa ya msingi yanayofanywa na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi kwa tume tukilalamikia masuala ambayo yanakatazwa kisheria.

Kwa mfano, katika kampeni watumishi wa serikali ikiwemo Rais, waziri mkuu, mawaziri au watendaji wowote hawaruhusiwi kutumia ushawishi wa miradi au kutoa maelekezo ya ujenzi wa miradi mbalimbali katika kampeni.

Tunaona Rais anaagiza bila woga, waziri mkuu anaagiza bila woga. Tumelalamika Tume ya Taifa ya Uchaguzi, lakini tume haichukui hatua yeyote.

Tumeona mali za serikali, magari ya serikali yaliyobadilishwa rangi na kuwa rangi ya kijani na kuwekwa namba za Chama Cha Mapinduzi, yale yote ni magari ya Ikulu. CCM hawajaagiza gari hata moja, yale ni magari ya Ikulu na kama CCM wanapinga watoke hadharani na document hizi hapa.

Tumeona msafara wa Rais una magari zaidi ya 80, magari zaidi ya 50 ni ya serikali au watendaji wa serikali. Hii ni unfairness kwa sababu unampa Rais msuli wa serikali inayoendeshwa kwa kodi za wananchi wote.

Walimu wanalazimishwa kwenda kwenye mikutano ya Chama Cha Mapinduzi, hatuna tatizo CCM wakiwaalika wasanii, ile ni initiative yao lakini walimu wa nchi yetu ni watumishi wa umma, wanafunzi ni watoto wa watanzania mbalimbali wakiwemo wa Chama Cha Mapinduzi, vyama vya upinzani.

Tumeona vyombo vya habari vya umma kama TBC vinamtangaza Magufuli asubuhi mpaka asubuhi, magazeti ya umma. Mamlaka nnyingi za kiserikali.

USHIRIKIANO

Tumesikia viongozi kadhaa wakizungumza dhana ya ushirikiano wa vyama na tumemsikia Msajili wa Vyama vya Siasa akitokeza hadharani akisema nyinyi hamruhusiwi kuunga mkono chama kingine, muda umeshapita, haya ni mambo ya kusikitisha sana.

Hauwezi ukanitungia mimi sheria ya kujenga mahusiano na rafiki ama kujenga uadui na mtu, hayo ni mahusiano ya watu na watu.

Wamekuwa wakipinga kauli zozote zinazoashiria ushirikiano wa njia yoyote kati ya CHADEMA na ACT, lakini wakati huo huo akifumbia macho viongozi wa hivi vyama vya upinzani kama TLP au UDP vikitoka na kumuunga mkono Magufuli.

"Kamati Kuu baada ya kushauriana kwa kina na mgombea wetu Urais wa Zanzibar, tumeona ni sahihi kabisa kwa chama chetu kumuunga mkono Seif Sharif Hamad, mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ACT kwa hiyo mgombea wetu ameridhia kujitoa yeye mwenyewe kwa mapenzi yake, taratibu zake za kujitoa zitafuata.

Kamati Kuu imeridhia kuendelea na mazungumzo kuungana mkono kwa baadhi ya kata hata majimbo ambayo tunafikiri tukiweza kumuunga mkono wa chama kingine mwenye nafasi zaidi tunaweza tukapata mwakilishi aliye bora zaidi wa eneo hilo.

KUZUIWA MIKUTANO URAIS

"Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumzuia mgombea wetu, nimeshazungumza kuhusu tume kuwa mchezaji na refarii. Awali mheshimiwa Lissu alisema ataendelea na mikutano yake ya kampeni ambayo kimsingi ni haki yake, lakini akasema uamuzi wa mwisho anaiachia Kamati Kuu ya chama chetu. Tumekubaliana tufanye yafuatayo

"Kwa sababu tunatambua nia na dhamira Tume ya Uchaguzi, kwa sababu tunatambua sababu mbalimbali zisizo na mantiki sana zinazotafutwa kujaribu kumkwaza zaidi mgombea Urais, tumeamua kutowapa fursa hawa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

"Hata kabla sijaeleza maamuzi yetu, naomba nieleze ni nini kilifanyika, tumepokea hukumu kutoka tume ya Taifa ya Uchaguzi, katika kujitetea kwake, Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na mambo mengine kadhaa ilijaribu kujenga dhana kwamba adhabu iliyotolewa haikutolewa na tume, imetolewa na vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi huu.

"Fair enough, lakini mwenyekiti wa kikao na katibu wake ni watendaji wakuu wa tume kwa maana hiyo wanarusha lawama kwamba hawakuamua wao, waliopiga kura ni vyama vyenyewe vya siasa.

Tuna vyama 15 vilivyoshiriki kikao hicho... na katika kura 15 zilizopigwa, kura tatu zilikataa kumfungia Mheshimiwa Lissu mikutano yake, lakini kura 12 ya hivi vyama vilipiga kura eti ya kumuengua mheshimiwa Lissu asiendelee na kampeni, sisi kama CHADEMA tunapinga hukumu hii.

Tumemshauri mgombea wetu asiendelee na mikutano kwa hiyo mheshimiwa Lissu hataendelea na mikutano ya kampeni kwa kipindi hiki ambacho tume imezuia mikutano yake.

Tundu Lissu sio tu ni mgombea Urais wa chama chetu, huyu ni Makamu Mwenyekiti wa chama na chama hiki kina kazi kubwa za kufanya, za kisiasa na za kijamii kwa hiyo Tundu Lissu hatakosa kazi ya kufanya kwa kipindi cha siku saba.

"Chama kitampangia programu mahsusi kama makamu mwenyekiti wa chama kufanya majukumu ya kijamii na kisiasa katika maeneo ambayo chama kitapanga,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Freeman Mbowe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news