Diwani Mteule Kata ya Mkambarani Charles Mboma awa tumaini la wananchi Mkono wa Mara baada ya kukosa huduma zote muhimu toka mwaka 1974

Wananchi wa Kijiji cha Mkono wa Mara Kata ya Mkambarani mkoani Morogoro wamesema wana imani kubwa na Diwani Mteule wa kata hiyo kuwa atawaletea maendeleo kutokana na kijiji hicho kukosa huduma zote muhimu toka kianzishwe mwaka 1974,anaripoti Victoria Kazinja (Diramakini) Morogoro.

Wakizungumza na Diramakini kijijini hapo, wanakijiji hao wamesema kuwa kijiji hicho kimesahaulika na hivyo kupelekea kukosa huduma muhimu kama umeme, maji, zahanati huku miundombinu ikiwa ni mibovu.

Diwani Mteule wa Kata ya Mkambarani, Charles Mboma kwa tiketi ya CCM.(Diramakini).

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Mwanika, Antoni Kunambi anasema kijiji hicho kimesahaulika toka enzi za operesheni vijiji hali iliyopelekea wakazi wake kuishi maisha ya tabu na mahangaiko.

‘’Cha ajabu toka mwaka 1974 mpaka leo hatukumbukwi, hakuna barabara, maji, umeme wala zahanati, kijiji hiki kipo umbali wa kilomita 28 toka Mkambarani senta, tunahitaji umeme, barabara, maji na zahanati, tuna imani sana na Diwani wetu mteule kuwa atalisimamia hili,"amesema Kunambi.

Nae Mjumbe wa Halmashauri Kata ya Mkambarani, Japhet Mpende, ambae pia ni mkazi wa kijiji hicho amesema ni kweli changamoto hizo zipo, na kuongeza kuwa kijiji hicho kipo nyuma kabisa kielimu na kiafya hali inayopelekea akina mama wajawazito na watoto kuhangaika kwa kukosa kituo cha kupimia.

‘’Hakuna kituo, huwa tunajitahidi kutafuta waganga ili kuwapima watoto juu ya mti, tiba tunapata taasisi ya magereza, ila kuna umbali sana kufika huko na gharama ni kubwa, kwa pikipiki ni shilingi elfu kumi na tano, wengine wanashindwa kabisa hususani wajawazito wakitaka kujifungua, tumefurahi kwa diwani wetu kupita bila kupingwa, tuna imani nae sana atatusaidia,’’anaeleza.

Kwa upande wake Diwani Mteule wa Kata ya Mkambarani, Charles Mboma kwa tiketi ya CCM, anasema kwa kuziona changamoto hizo pamoja na zingine zinazowakabili wananchi wa kata hiyo, ndizo zilizomsukuma kuwania nafasi hiyo ili aweze kutoa mchango wake kwa kushirikiana na wananchi ili kuleta maendeleo.

‘’Kilichonivutia ni ili kutoa mchango wangu katika kata yangu na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, pia kutokana na kuona baadhi ya maeneo mambo hayaendi vizuri, ikiwemo sekta ya elimu, tuna matatizo ya madarasa, shule nyingi kuchakaa, vyoo na upungufu wa sekondari, na wananchi wetu wanaishi maisha ya umasikini sana,"anasema Mboma.

Akizungumzia Kijiji cha Mkono wa Mara, Mboma amesema ni kweli kijiji hicho hakina zahanati, maji wala umeme toka kianzishwe, na kwamba wananchi wameshajichangisha ili waanze wenyewe ujenzi kabla ya kuomba msaada kwa serikali.

No comments

Powered by Blogger.