Kampeni ya Amsha Amsha 2020 'Kichinjio Mkononi' yaingia mtaani

Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Ngw'ilabuzu Ludigija amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura, ili kuwachagua viongozi wanaowataka Jumatano ijayo ya Oktoba 28 mwaka huu, anaripoti Abdallah Hussein, Dar es Salaam.

Akizindua Kampeni ya Amsha Amsha 2020 "Kichinjio Mkononi" inayoendeshwa na Uhuru Fm, Ludigija amesema kupiga kura ni jambo muhimu na kuwataka wananchi kuchagua maendeleo kupitia wagombea wa CCM na kuacha kuchagua malalamiko ya wapinzani.

Amesema, kutokana na mafanikio makubwa yaloyoletwa na Rais Magufuli, kuna kila sababu ya waTanzania kuwarejesha madarakani viongozi wa CCM ili wazidi kuiinua Tanzania kimaendeleo.

Lubigija ameyataja baadhi ya mambo ya kujivunia kwa Rais Magufuli ni pamoja na ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, stendi, masoko na madaraja, pamoja na maboresho katika huduma za maji, umeme na afya.

Amesema Rais John Magufuli ameifanyia nchi makubwa, hivyo ni vyema watanzania wakajitokeza kumchagua tena. Aidha, amepongeza namna Serikali ilivyowasaidia watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mikopo ambayo imewainua kimaisha kwa kuendesha miradi mbalimbali.

Kampeni ya Amsha Amsha Kichinjio Mkononi inalenga kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura, katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28,2020.

No comments

Powered by Blogger.