Mafunzo hayo yatakayokuwa yakitolewa kwa wachimbaji wadogo ni pamoja na elimu ya utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu ili kuwawezesha kufanya uchimbaji wenye tija na kusaidia kuinua vipato vyao na kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la taifa.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 21, 2020 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wakati wa makabidhiano na uzinduzi wa kiwanda hicho kilichogharimu takribani shilingi bilioni 1.7 mpaka kukamilika kwake.
Naibu Waziri Nyongo ametumia fursa hiyo kuishukuru Kampuni ya Tan Discovery Mineral Consultancy kwa kukamilisha ujenzi wa viwanda hivyo na kuvikabidhi vikiwa katika ubora kwa mujibu wa makubaliano.
Aidha, Nyongo amebainisha kuwa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lilipewa jukumu la kuhakikisha linasimamia na kuhakikisha ujenzi wa viwanda hivyo vitatu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Ameendelea kusema kuwa, kwa sasa STAMICO limeonesha kuwa ni shirika linalojiendesha kwa faida baada ya kuanza kutoa gawio kwa serikali kwa kiasi kisichopungua shilingi bilioni moja mwaka 2019 na bilioni 1.1 mwaka huu 2020.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri Nyongo ameitaka STAMICO kuthamini gharama kubwa iliyotumika katika ujenzi wa miradi hii na kuweza kuisimamia ipasavyo ili kuleta matokeo chanya hususani katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kuzalisha kwa tija kwa kutumia vifaa vyenye teknolojia rahisi na bora walivyowekewa na serikali yao.
Ameendelea kuisisitiza Stamico kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa wakazi wa maeneo jirani na kilipo kituo ili waweze kunufaika na matunda ya kuwepo kwa mradi huu.
Naibu Waziri, Nyongo ametoa wito kwa wachimbaji wadogo wa Itumbi na maeneo jirani kukitumia kituo hicho kujifunza na kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na shughuli za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji pamoja na biashara ya madini kwani kituo kimejengwa kwa ajili yao.
Akielezea muda uliotumika katika ujenzi wa miradi hiyo, ikiwa ni pamoja na Lwamgasa, Katente mkoani Geita na Itumbi unaokabidhiwa leo, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal amesema, mradi ulianza mnamo mwaka 2016 ambapo mwezi Aprili 2020 viwanda viwili vya Katente na Lwamgasa vilikabidhiwa na uzinduzi wa kiwanda cha Itumbi kinakamilisha mradi wa tatu uliokuwa umesalia.
Amesema, wanatumia teknolojia rahisi ili kuwawezesha wachimbaji hao kutumia mitambo hiyo kwa elimu ndogo wanayopewa na wataalamu wake kwa kipindi kifupi.
Amebainisha kuwa, mkataba waliopewa uliwataka kubuni na kujenga mtambo wa kuchenjua dhahabu, lakini wakaona ni vema kutumia fursa hiyo kwa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo katika maeneo ilipo mitambo hiyo ili waweze kufahamu namna ya kuendesha mashine hizo pamoja na elimu nyingine zinazohusiana na uchimbaji, utafutaji na uchenjuaji wa dhahabu watakazokuwa wakipewa.
Aidha, amebainisha kuwa, vijana waliohusika katika ujenzi wa kiwanda hicho na vile vya Katente na Lwamgasa wamewawezesha kwa kuwapa mashimo ya kuchimba ili waweze kujipatia kipato kutokana na uchenjuaji watakaokuwa wakiufanya kiwandani hapo.
Pamoja na kuwapa mashimo hayo, Sezigwa amesema wamewatambulisha vijana hao katika ofisi za wilaya na mkoa ili waweze kuwatumia kutekeleza miradi mingine kwani wameonesha uwezo wa kufanya hivyo.
Aidha, amebainisha hatua ya juu zaidi waliyoichukua ili kuwawezesha vijana hao kwa kuanzisha kampuni inayoitwa Tanzim itakayokuwa ikijishughulisha na uendeshaji wa mitambo hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Meja Jenerali mstaafu Michael Isamuhyo aliishukuru Serikali kwa namna ilivyoelekeza nguvu zake na fedha katika kuwasaidia vijana na kubainisha kuwa katika kipindi hiki vijana wanatazamwa kwa namna ya pekee katika kuharakisha maendeleo ya jamii.
Ametoa kauli hiyo baada ya kubaini kuwa, wananchi wengi wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu kuwa ni vijana na hivyo kukiri kuwa ukizungumzia wachimbaji wadogo unazungumzia vijana.
Pamoja na hayo, mstaafu Michael Isamuhyo amebainisha wajibu wa Shirika la Madini la Taifa kuwa ni pamoja na kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali na kubaini mashapo yaliyopo na kutenga kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Ameongeza kuwa, katika kutekeleza hilo tayari shirika hilo limefanya tafiti 20 na tatu kati ya hizo zipo mkoani Chunya ambapo ni eneo la Itumbuli, Sangambi na Shoga
.
Jukumu lingine alilolibainisha ni kukuza uelewa wa wachimbaji kwa teknolojia rahisi na isiyokuwa na athari kwa afya na mazingira pamoja na majukumu mengine mengi.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Stamico, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chunya na wengine wengi.