Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera amewasili nchini kwa ziara yake ya siku tatu kuanzia leo Oktoba 7 hadi Oktoba 9, 2020 yenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Malawi katika masuala ya kibiashara na kupokelewa na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli. Akizungumza baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli ameeleza namna walivyokubaliana kushirikiana kukuza uchumi wa wananchi wa Tanzania na Malawi katika Sekta ya Biashara na Miundombinu.
Rais Magufuli amesema kuwa, katika mazungumzo yao ya muda mfupi wamekubaliana kuanzishwa kwa ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lilongwe ambayo itasogeza huduma za wafanyabiashara kutoka Malawi. “Tumezungumza na Mheshimiwa Rais wa Malawi kwamba upande wa Malawi Waziri anayehusika na usafirishaji ahakikishe kuwa anawezesha mambo yaliyokuwa yamekwama hususani ufunguzi wa ofisi za TPA Mjini Lilongwe,"amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alitoa wito kwa Rais Chakwera kuwa, mahusiano kati ya nchi hizo mbili yanatakiwa yawe ni mahusiano ya kibiashara ambayo kwa kiasi kikubwa yatawezesha kukua kwa uchumi kati ya Tanzania na Malawi. Katika Sekta ya usafirishaji Rais Magufuli alieleza mambo yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania ikiwemo kuimarishwa kwa sekta ya usafiri wa anga, kwani sekta hiyo ni kiungo muhimu katika mahusiano ya kimataifa hasa kwa Tanzania na Malawi kama wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
“Tunataka Malawi waamue wenyewe wanataka kutumia
usafiri wa njia gani, kwa njia ya treni, barabara, ndege au bandari na
ndiyo maana tunataka ule mkataba uliokuwa haujakamilika kati ya Malawi
na Tanzania kuhusu usafiri wa ndege umalizwe haraka kwa sababu sekta hii
ni muhimu kwa utalii”, Amesema Rais Magufuli. Rais. Magufuli
aliongeza kuwa sekta ya umeme ni muhimu kwa nchi hizo mbili kwa hiyo
wataangalia jinsi gani wataweza kushirikiana katika ujenzi wa mradi wa
umeme wa Songwe ambao utatarajiwa kuzalisha megawatt 180, kwani Tanzania
ina uzoefu mkubwa wa ujenzi wa miradi kama hiyo ikiwa inatekeleza
ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Julias Nyerere Hyroelectric
Power (JNHPP), wenye kuzalisha Megawatt 2,115.
Kwa upande wake Rais wa
Malawi, Dkt.Lazarus Chakwera amesema kuwa ni muda sasa kwa Waafrika
kuungana na kufanya maendeleo ya pamoja kama ndugu ili kukuza uchumi wa
nchi za Afrika na bara kwa ujumla. “Ni muda sasa kwa waafrika
kutafuta mwelekeo wetu na kufanya maendeleo kwa kasi yetu, kuliko
kusubiri watu wengine waje kufanya haya, hii itapelekea kuwepo na
uhusiano mzuri na mwenendo mzuri wa kibiashara ambao utaleta uwazi
katika biashara na kupelekea matumizi ya pamoja ya rasilimali zetu”,
Amesema Chakwera.
Rais Chakwera aliongeza kuwa muda umefika wa
Afrika sasa kuzungumza habari zinazofanana kuhusu maendeleo ya Afrika
bila kusubiri watu wengine kuzungumzia Afrika katika hatau za maendeleo
inazozipiga. Aidha Rais Chakwera alimshukuru Rais Magufuli kwa
kumkaribisha na kubadilishana mawazo kuhusu mashirikiano katika sekta
mbalimbali zikwemo siasa, uchumi na sekta za uzalishaji madini ili
kuinua uchumi wa wananchi wa Tanzania na Malawi.
0 Comments