Mafunzo ya BRELA yabadili fikra za maafisa biashara,kuwezesha matokeo chanya nchini


Afisa Tawala na Rasilimali Watu Mkuu wa BRELA, Migisha R.Kahangwa akimkaribisha mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma, Dkt.Vedast Makota kufunga mafunzo ya utoaji wa huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kwa maafisa TEHAMA na Maafisa Biashara wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mkoa wa Kigoma, Tabora na Katavi yaliyofanyika kwa muda wa siku tano mkoani Kigoma. (BRELA/Diramakini).
Maafisa biashara nchini wametakiwa kutekeleza jukumu lao la msingi la kuwa washauri wa biashara na uwekezaji ili kuweza kukuza biashara ili kwenda sambamba na ukuaji wa uchumi wa taifa letu, anaripoti Christina Njovu (BRELA) Kigoma.

Kaimu Katibu Tawala ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma, Dkt.Vedast Makota ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya utoaji wa huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kwa maafisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na maafisa biashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma yanayoendendeshwa na Wakala ya Usajili Biashara na Leseni (BRELA) na kufanyika kwa muda wa siku tano mkoani Kigoma.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma, Dkt.Vedast Makota akifunga mafunzo ya utoaji huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kwa maafisa biashara na TEHAMA wa mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi yaliyofanyika mkoani Kigoma. (BRELA/Diramakini).

“Kama mnavyojua nchi yetu kwa sasa imeingia katika uchumi wa kati unaokwenda sambamba na ukuaji wa biashara, pamoja na majukumu mengi mlionayo itumieni fursa hii kufanya majukumu yenu ya msingi na kwa kusisitiza yatumieni mafunzo haya ili kuweza kuhakikisha tunawapata wafanyabishara wengi na kuwasajili,"amesema.

Aidha, ameongeza kuwa, hivi karibuni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli alipofika mkoani Kigoma na kumpokea Rais wa Burundi,Évariste Ndayishimiye alizungumza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha Mkoa wa Kigoma unakuwa ni kitovu cha biashara katika Ukanda wa Magharibi,hivyo wao ambao ndio maafisa biasharani lazima watambue kuwa wana jukumu kubwa la kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.

Meneja wa Kiwanda cha Chumvi Uvinza, Bonny Mwaipopo akizungumza na Maafisa wa BRELA walipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya ukaguzi mkoani Kigoma. (BRELA/Diramakini).

Dkt.Makota amewaomba maafisa biashara katika kutekeleza majukumu yao, wahakikishe yale ambayo wamejifunza wanayazingatia kwa upana wake ili kuweza kuhakikisha kuwa huu mtazamo wa kitaifa wa kuufanya Mkoa wa Kigoma unakuwa kitovu cha biashara wanautekeleza katika utendaji kazi wa kila siku.

Hata hivyo, Dkt.Makota amesema, maafisa biashara wasijikite tu katika ukusanyaji wa mapato bali pia wawe marafiki washauri wa wafanyabiashara, kwani kukua kwa biashara ndiko kunakosababisha kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Akitoa rai kwa washiriki wa mafunzo, wengine waliokwisha yapata na wanaotarajia kupatiwa mafunzo hayo yanayotolewa na BRELA kwa lengo la kuwawezesha wataalamu wa TEHAMA na biashara kutoa huduma hiyo saidizi kwa wananchi kwa weledi na uadilifu mkubwa na kujiepusha na vitendo vya kuomba ama kupokea rushwa katika utoaji wa huduma hizo.

Lengo pia likiwa ni kuyafanya mafunzo hayo yaoneshe matokeo chanya na kuondoa urasimu usiokuwa na lazima kwani Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikisisitiza watumishi wa umma kubadilika na kuwa mfano bora kwenye utendaji kazi na uwajibika.

Mafunzo hayo yanayoendeshwa na Wakala ya Usajili Biashara na Leseni (BRELA) yamepangwa kufanyika nchi nzima, yatawawawezesha wafanyabiashara kuweza kurasimisha biashara zao kwa urahisi kwa kuwa sasa hivi mtu anaweza kufanya usajili kwa njia ya mtandao hata akiwa nyumbani kwake na kujipatia leseni ya jina la biashara ama leseni na kuipa biashara yake utu wa kisheria na thamani.

Hata hivyo, maafisa hao wamesema kuwa, mafunzo hayo yamebadili fikra zao kwa asilimia kubwa, hivyo wataenda kuyafanyika kazi ili kuwezesha kuyafikia matokeo chanya nchini, ambayo yana tija kubwa katika kuinua viwango vya uchumi na kuboresha hali za maisha ya Watanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news