MATIs,FTC zatakiwa kujijengea dhana ya kujitegemea kuleta mapinduzi ya kiuchumi kupitia kilimo

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amewaambia watumishi wa Idara ya Mafunzo Utafiti na Huduma za Ugani kuwa ziara ambazo amekuwa akifanya kwenye Vyuo Vya Mafunzo ya Kilimo (MATI’s) pamoja na Vituo vya Mafunzo ya Wakulima (FTC) zina lengo la kujenga dhana ya kujitegemea ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa watumishi na wakulima nchini, anaripoti Revocatus A. Kassimba (WK) Dodoma.

Katibu Mkuu Kusaya ameyasema hayo leo Oktoba 6,2020 baada ya kufanya ziara ya kutembelea Kituo cha Wakulima cha Bihawana, nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya (katikati) akizungumza na wakufunzi wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Bihawana Dodoma alipotembelea kukagua utendaji kazi na kuagiza kibuni miradi ya kujitegemea kimapato.

Katibu Mkuu Kusaya amesema tangu ateuliwe na Mheshimiwa Rais Magufuli kuiongoza Wizara ya Kilimo ametembelea Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI’s) vya Umma na Binafsi 14 pamoja na Vituo vya Mafunzo ya Wakulima (FTC) vinne huku akiwa amebakiza Kituo kimoja tu na kuongeza kote huko alipopita si kwa lengo la kufanya utalii bali kujenga dhana ya kujitegemea kiuchumi na wakati huo huo kujiletea mapinduzi ya kweli ya kiuchumi.

Katibu Mkuu Kusaya amewaasa viongozi wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Bihawana kuwa wanapaswa kuongeza maeneo makubwa kwa ajili ya kuanzisha mashamba makubwa na ya kimkakati hata kama yatakuwa nje au mbali ya Vituo vya Wakulima ili siku moja wazalishe mbegu bora au mazao ambayo; yatauzwa na kuleta faida kwa Vituo.

“Napenda kuwaona mkiwa mmeanzisha miradi mingi, muwe na mashamba darasa ili mazao hayo yaje kuuzwa na fedha hizo zitumike kuendesha shughuli za usimamizi na maendeleo.

“Napenda pia mfikirie kuongeza maeneo kwa ajili ya kuwekeza na muwe mkiongea na Viongozi wa vijiji au mitaa; kuwaomba maeneo makubwa kwa ajili ya kuongeza tija na faida katika kilimo”. Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.

Katika ziara yake hiyo; Katibu Mkuu Kusaya alitoa ng’ombe wakubwa wawili, vifaranga vya kuku 1,000 kwa ajili ya kuanzisha mradi mkubwa wa ufugaji pamoja na kutoa kiasi cha fedha cha shilingi milioni kumi (10,000,000) kama sehemu ya mtaji wa kuanzisha miradi ya kujenga dhana ya kujitegemea na kujiendesha kwa faida.

Sambamba na vitu hivyo Katibu Mkuu Kusaya pia alimkabidhi Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima cha Bihawana Emmanuel Mtenga pikipiki moja kwa ajili ya kuongeza ufanisi kwa utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news