Mgombea Udiwani Emmy Kiula alivyobadilisha klabu cha pombe kuwa zahanati mjini Morogoro

Kutokana na changamoto zinazowakabili wanawake katika jamii hususani katika kugombea nafasi za uongozi, wanawake wameamua kuja na mbinu mbalimbali za kukabiliana nazo, anaripoti Mwandishi Diramakini (diramakini@gmail.com).

Imeelezwa kwamba, wanawake hawana budi kujitoa, kujituma, kusaidiana, kuaminiana na kupendana wenyewe kwa wenyewe ili kuweza kusonga mbele na kufikia malengo yao ikiwemo kuleta maendeleo kwao na jamii kwa ujumla.

Mgombea Udiwani kata ya Mji Mpya Emmy Kiula kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mwenye kiu ya kuleta maendeleo katika kata yake kama mama, anasema huko nyuma kulikuwa na uoga kwa wanawake kujitokeza katika kugombea nafasi za uongozi pamoja na kuto aminiana wenyewe kwa wenyewe, lakini kwa sasa wanawake wanajiamini na wakithubutu wanaweza.

Anaeleza kuwa, wanawake kwa sasa wanajitokeza kugombea lakini wanashindwa kupambana na wanaume, huku akitoa mfano kwa wanawake wa Manispaa ya Morogoro waliojitokeza kugombea nafasi ya udiwani kuwa walikuwa wengi lakini waliofanikiwa kupita kura za maoni ni wawili tu kati ya kata 29.
Mgombea Udiwani kata ya Mji mpya Emmy Kiula kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). (Diramakini).

Kiula anasema baada ya kujiona kuwa yuko tayari na anauwezo wa kuwa kiongozi, huku akiwa na kiu na nia thabiti ya kuhakikisha kata yake inapata maendeleo katika sekta ya elimu, afya, miundo mbinu, maji na huduma mbalimbali za kijamii aliamua kuingia katika uongozi.

Anasema alianza safari yake ya uongozi akiwa Mwenyekiti wa mtaa wa Mjimpya mwaka 1999 hadi 2009, na kuendelea kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika chama na serikali ikiwemo katibu wa elimu, uchumi, malezi na mazingira nafasi ya mkoa CCM, Mjumbe Sekretarieti ya mkoa, Jumuiya ya wazazi, diwani kata ya Mjimpya, na hatimae kugombea nafasi ya udiwani kata ya mji mpya tena.

Anaeleza kuwa ili kutimiza kiu yake ya kuleta maendeleo kwa jamii alifanya mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari ya Mjimpya ambayo alitamani sana kuijenga ndani ya kata yake, lakini kutokana na kata hiyo kuwa na eneo dogo ilibidi wapewe eneo katika kata ya Lukobe.

“Nilijenga shule ya sekondari ya Mjimpya ambayo mpaka namaliza miaka yangu mitano 2005 mpaka 2010 ilikuwa imeshatoa watoto wa form four, lakini kiu yangu kubwa ilikuwa ifike kidato cha sita, inafanya vizuri imeshakuwa ya tatu kimanispaa, kwa sasa imehamishwa baada ya kupitiw a na mradi wa treni ya mwendo kasi, na imejengwa nyingine ya mfano” anasema Kiula.

Anasema ujenzi wa shule hiyo ulileta manung’uniko kidogo kwa baadhi ya watu, kuwa iko mbali na ndipo alipowaza afanye nini kuwafurahisha wananchi wake na kuja na wazo la kuwajengea zahanati, kutokana na kata kutokuwa na zahanati.

“Nashukuru Mungu kwenye utawala wangu niliacha jina kipindi cha nyuma, baada ya kuona wananchi wangu wamekuwa na ukakasi kwenye mioyo yao kuwa shule imeenda kujengwa mbali, nikaona ili niwaweke wananchi wangu vizuri niwatafutie kitu ambacho kitafuta hiyo ya maumivu ya shule kujengwa mbali,"amesema Kiula.

Anasema, baada ya kuona kuna eneo la Kaloleni katika kata yake lina kilabu cha pombe ndipo alipoenda kumuona Waziri wa ardhi ambae ni Rais wa sasa, ili kuomba kibali cha ujenzi wa Zahanati katika eneo lile kwani lilikuwa la serikali, baada ya awali kumuomba Mkurugenzi nakusema pana ugumu kidogo labda kwa Waziri.

“Kwa kweli binafsi nilipanda basi kwenda kwa waziri wa ardhi, ambae ndio Rais wangu wa sasa, kwani halmashauri hazina mamlaka ya kufuta maeneo bila ya Wizara husika, nilipofika wizarani sikumkuta Waziri lakini nilipokelewa na Katibu wake dada mmoja mama Sijaona, nikamweleza shida yangu nae akanyanyua simu akampigia Waziri, Waziri akakubali," ameeleza.

Anasema,alifanikiwa kupata eneo hilo na kukatiwa mipaka, kwa kuwa alikuwa amesha andaa ramani kazi ikawa ni kusafisha eneo hilo ambalo lilikuwa na tani nyingi ya majivu yaliyotokana na upishi wa pombe katika eneo hilo toka enzi ya mkoloni ambao ulifanya mlima mkubwa sana.

“Palikuwa na kazi kubwa ya kuzoa majivu kwani toka enzi za mkoloni watu walikuwa wanapika pombe na wanalundika katika eneo hilo, tulizoa tani na tani ya majivu mpaka kuifikia ardhi ya kawaida” alisema.

“ Nilijenga ile zahanati mpaka nafika mwaka 2010 wakati wa uchaguzi nikawa nimeshapandisha boma lote limekamilika, na nikawa nimeshapata bati 150, nondo, kopo 50 za rangi na fedha milioni 17.2, lakini ikawa imeshafika ukomo lazima tuvunje mabaraza tuondoke kwenda kwenye uchaguzi,"alieleza Kiula.

Akizungumzia miundombinu katika kata hiyo alisema sio mibaya sana,na kwamba ana kiu ya kukamilisha vipande vya barabara vilivyobaki ikiwemo mitaro ya maji kuepuka tatizo la mafuriko, hasa kipande cha mtaa wa Makaburi na Ngoma C, pamoja na kukarabati kidaraja kinachounganisha Mjimpya na kichangani.

“Kwa upande wa barabara za mtaa ninampango wa kuzikarabati kwa kiwango cha changarawe au lami, lami ndio nzuri zaidi mitaa itapendeza, ninawaza baadhi ya barabara ziwe na taa, na ukizingatia ninakituo kizuri cha stendi ya vijijini ambayo niliipigania mpaka nikaunda kamati ya wazee kusukuma hicho kitu, lilikuwa ni wazo langu,"anaeleza.

Anasema ndoto yake ni kuhakikisha Kata ya Mjimpya inakuwa na maendeleo huku huduma muhimu zikipatikana kwa urahisi ikiwemo vikoba, ujasiliamali na kuhamasisha michezo kwa vijana kwa kushindanisha kata mbalimbali, pamoja na kuwawezesha walemavu.

Nae Mkazi na mfanyabiashara katika Manispaa ya Morogoro Grace Mwasomola, anaeleza namna alivyonufaika na kikoba na ujasiriamali kupitia mgombea huyo, nakusema kwamba wana imani na yeye na kwamba ataendeleza yale mazuri aliyoyaanzisha.

Kwa upande wake mkazi wa Mjimpya,Neema Kapombe anasema Kiula alifanya mengi wakati akiwa diwani wa kata hiyo mwaka 2005 mpaka 2010, ambapo alifanya vyema katika sekta ya elimu kwa kujenga shule ya sekondari Mjimpya, zahanati, michezo kwa vijana na kuwainua wanawake kiuchumi kwa kupitia vikoba na ujasiriamali.

“Mama Kiula aliwahi kuwa diwani hapo awali, ambapo alipumzika kutokana na changamoto ya kuuguliwa na mume wake, kwakweli ni mama mchapa kazi sana aliyetuletea maendeleo katika kata yetu kwa kujenga shule, zahanati, kuhimiza michezo, na kututoa katika umasikini kwa kuanzisha vikoba na kujifunza ujasiriamali mbalimbali uliotuwezesha kutuinua kiuchumi,” anasemama Kapombe.

Hata hivyo, mkazi wa Mjimpya,Kibwana Zuberi anasema Mgombea huyo ni mfano wa kuigwa kwa kina mama na hata wanaume, kwa jinsi anavyojitoa kupambania maendeleo ya jamii kutokana na kufanya mengi alipokuwa diwani, na kwamba yale aliyoyafanya ni kielelezo tosha kwa yeye kukubalika na kupewa ridhaa tena ya kuwa diwani wa kata hiyo.

Wanawake wamekuwa wakifanya vizuri katika uongozi pale wanapopata nafasi, mbali na kukumbana na changamoto nyingi katika jamii, hivyo ni vyema jamii ikaacha mtazamo hasi kwa mwanamke, nakumpa nafasi ya kuwa kiongozi ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, na kuleta maendeleo kwenye jamii na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments