Mhandisi Mmari: Ubungo Interchange ujenzi umefikia asilimia 81, kukamilika Desemba 30,2020

Mradi wa Ujenzi wa Barabara za Juu eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam maarufu kama Ubungo Interchange unaozikutanisha barabara tatu za Mandela, Sam Nujoma na ile ya Morogoro ambao unatekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) umefikia asilimia 81 na ifikapo Desemba 30, 2020 ujenzi utakuwa umekamilika, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Barakaeli Mmari amesema, kuwa ujenzi huo ambao ulianza mwezi Mei, mwaka 2017 unaendelea vizuri na sasa barabara zote mbili za juu zimefunguliwa kwa majaribio huku ujenzi ukitarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 ifikapo Desemba 30, mwaka huu 2020.

“Kwa mara ya kwanza Mei 30, 2020 tuliifungua barabara ya ghorofa ya chini ya Morogoro kwa majaribio ambapo tuliruhusu magari kupita na Septemba 30, 2020 barabara ya ghorofa ya pili ya Nelson Mandela/Sam Nujoma ilifunguliwa kwa majaribio pia na ni mategemeo yetu kuwa ifikapo Desemba 30, 2020 ujenzi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi kuendelea kufaidi barabara hiyo,”amesema Mhandisi Mmari.

Mhandisi Mmari ameongeza kuwa, ujenzi wa barabara za juu ulikuwa na lengo la kuondoa msongamano katika makutano ya barabara hizo katika eneo la Ubungo ambapo kutokana na msongamano mkubwa wa magari uliosababisha watu kuchelewa kufika kwenye shughuli zao kwa wakati, hivyo kupoteza muda mwingi ambao ungetumika kuwaongeza kipato.

Akifafanua jinsi madereva watakavyokuwa wakitumia barabara hizo, Mhandisi Mmari amesema katika eneo hilo kuna barabara ngazi (ghorofa) tatu, ya chini, ya kati na ya juu, ambapo ngazi ya chini itatumiwa na magari yanayotoka Mjini kwenda Mwenge, Mwenge-Kimara, Kimara-Buguruni na Buguruni kwenda Mjini. Vile vile itatumiwa na magari yote yatakayokuwa yanapinda kushoto kwenye maungio hayo. 

Ngazi ya kati itatumiwa na magari yanayotoka Kimara kwenda mjini na yatokayo mjini kwenda Kimara.Ngazi ya juu itatumiwa na magari yatokayo Mwenge kwenda Buguruni na yatokayo Buguruni kwenda Mwenge.

Aidha, Mhandisi Mmari amesema barabara za juu zimejumuisha njia maalum kwa ajili ya mabasi ya mwendo kasi. Kwa upande wa ajira, Mhandisi Mmari amesema kuwa, ujenzi huo umekuwa ukiajiri watanzania wengi wakiwemo wananchi wa kawaida mpaka wahandisi ambao wanashughulika na kazi za kihandisi katika kutekeleza ujenzi kwa ufanisi. 

“Tumeajiri wafanyakazi kati ya 800 hadi 900 kwa mwezi na kati ya hao wafanyakazi wa nje ni asilimia 10 tu huku wafanyakazi wazawa wakiwa ni asilimia 90, kwa hiyo ujenzi huu umeleta faida kwa watanzania wengi hasa wakazi wa jiji la Dar es Salaam,”amesema Mhandisi Mmari.

Wananchi na wakazi wa Ubungo wameeleza furaha yao kwa kufunguliwa kwa majaribio barabara hizo, “Tunaishukuru Serikali ilichotutendea kwani foleni sasa hakuna, magari yanapita vizuri na sisi tunapita vizuri tu, ninaamini tunakoelekea tutafanya mambo mazuri zaidi ya haya,”ameeleza Bakari Juma.
Naye Johnson Mwakalukwa amesema, barabara hiyo imesaidia sasa kwa wasafiri kutoka mikoani kupata ahueni kwani sasa wakifika Mbezi wanakutana na barabara ile ya njia nane na wanakuja kumalizia na Ubungo Interchange kwa hiyo saa mbili za kukaa kwenye foleni kwenye maungio ya Ubungo hakuna tena.

"Kabla ya ujenzi wa barabara hizo usumbufu ulikuwa mkubwa kwa wananchi wa Dar es Salaam kwani walikuwa wakichelewa kufika majumbani, lakini kwa sasa hakuna foleni tena katika eneo hilo ambalo limesumbua kwa muda mrefu sasa,"amesema mwananchi mwingine Leshima Said mkazi wa jiji hilo la biashara nchini Tanzania. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news