Micheweni FM yaomba ushirikiano zaidi

Redio Jamii Micheweni ambayo iliongoza nchini Tanzania mwaka 2019 kwa ubora wa maudhui ya redio katika utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam imefanikiwa zaidi katika uzalishaji wa maudhui bora ya vipindi vya redio licha ya kukabiliwa na changamoto ya uwezo wa kifedha.
Meneja wa redio hiyo, Ali Masoud amesema, ni furaha kuona kwamba mafaniko yote yanatokana na uwezo waliojengewa na mashirika mbalimbali zaidi hasa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambao umewezesha kituo kukidhi mahitaji yake ikiwemo wafanyakazi pamoja na ujuzi wa kituo katika masuala ya kiutawala.

Amesema, kupitia maarifa ya uandaaji wa harambee waliyopata kupitia mpango huo iliwezesha kukiweka kituo karibu na jamii ya Micheweni katika shughuli zake zote ambapo kupitia hilo kilifanikiwa kufanya hafla za kukusanya fedha.

Amesema, Micheweni FM imefanikiwa kuandaa hafla ya kutafuta fedha kwa uendelevu wa kituo mnamo Agosti 19, 2020 iliyohudhuriwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali aliyekusanya jumla ya shilingi milioni tano kwa ajili ya ununuzi na ufungaji wa sola kwenye kituo hicho.

Pia kupitia mpango mkakati ulioandaliwa, kituo kiliweza kupata wadau wapya wa kushirikiana na kufanya nao kazi ambao ni (TAMWA ZNZ), ActionAid, na RTI ambapo kupitia wadau hao imesaidia kuongeza mapato ya kituo kwa kiwango cha shilingi milioni 11.

Amesema, ujuzi wa ufuatiliaji na tathmini umekipa nguvu kituo hicho kukusanya taarifa kwa wakati kutoka kwenye vipindi vyake na kuziweka kwenye kumbukumbu kwa ajili ya kuzishirikisha kwa wadau wengine, kuzichambua pamoja na kujibu masuala yaliyojitokeza iwe ya ndani au nje.

Ameongeza kuwa, kituo hicho pia kimeimarisha utumiaji wa teknolojia kwa kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter na Instagram ambayo inasikika hadi nje ya mipaka ya eneo la redio jamii ya Micheweni.

"Zamani hatukujua umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii, lakini kupitia programu hii, tumewekeza nguvu zaidi katika mitandao hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kwa wadau wetu kutoa maoni yao moja kwa moja kupitia mitandao hiyo,”amesema Meneja Ali Kombo.

Meneja huyo amesema kuwa, changamoto pekee ambayo kituo kinakabiliwa nayo kwa sasa ni ukosefu wa fedha za kutekeleza mipango yake kabambe ambayo inahusu kuandika na kufuatilia maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyofikiwa na jamii ya Micheweni sambamba na kubaini changamoto zilizojitokeza.

Akiongea na waandishi wa habari, Dkt.Mzuri Issa ambaye ni mmoja wa washauri waelekezi amesema, Redio ya Jamii Micheweni imepiga hatua kubwa sana katika eneo la uendelevu wa kitaasisi tangu UNESCO ilipozindua mpango wa mafunzo ya kukuza uwezo wa vituo hivyo mapema mwaka 2019.

Amesema, kituo kimeweza kuweka miundo na mifumo yote muhimu ikiwa ni pamoja na sera, mpango mkakati ya kudumu na ya mara kwa mara.

Pia amesema kuwa, kimefanikiwa kujipambanua kama redio ya kijamii kwa kuifanya jamii ya Micheweni kuwa sehemu ya juu ya kufanya maamuzi katika safu ya uongozi wa kituo hicho, kuwa na bodi huru yenye kuishirikisha jamii pamoja na ushiriki wa jamii katika kuandaa habari, vipindi, mijadala, sherehe na harambee.

Safia Mohamed Mzirai mmoja wa wadau wa kituo hicho amesema, “kwa sasa tunaona redio jamii imebadilika sana kwani sisi wasikilizaji tunapata kile tunachohitaji kwa wakati kutokana na mfumo ambao wameuweka hivi sasa wa kutushirikisha katika kila kitu wanachofanya, hii imesaidia sana."

Ameongeza kuwa, kulingana na uwezo na juhudi za redio kushughulikia maswala ya kijamii na kiuchumi yanayojitokeza kwa kuishirikisha jamii yenyewe hali hiyo imewafanya kuendelea kujivunia uwepo wa kituo hicho ndani ya jamii yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news