Mtaalamu aeleza uwezo wa mashine za kisasa uchunguzi saratani ya matiti

Uwezo wa mashine ya kisasa ya uchunguzi wa saratani ya matiti katika kugundua iwapo mtu anakabiliwa na saratani ya matiti au la ni wastani wa asilimia 85 hadi 90 ikiwa picha imechukuliwa vizuri, anaripoti Rachel Balama (Diramakini) Dar es Salaam.

Mtaalamu Bingwa wa Matumizi ya Mionzi katika Uchunguzi wa Magonjwa ORCI, Stephen Mkoloma amebainisha hayo leo alipozungumza katika semina ya siku moja ya kuwapa uelewa wafanyakazi wa taasisi hiyo kuhusu kipimo hicho.
Semina hiyo iliyohudhuriwa na wafanyakazi zaidi ya 25 wa taasisi hiyo imefanyika ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya mwezi Oktoba ambao ni maalum duniani katika uelimishaji kuhusu saratani ya matiti.

“Ni mashine yenye uwezo mkubwa, ni kipimo muhimu kwenye kuchunguza saratani katika hatua za awali kwani ina uwezo wa kuona kivimbe cha saratani ambacho kwa kawaida kingegundulika miaka miwili au mitatu baadae.

“Kwa maana kwamba mtu anaweza kufanya ‘screening’ kwa mashine nyingine na isigundulike lakini kwa kipimo cha Mammography kikagundulika,”amebainisha.

Amesema ikiwa picha imechukuliwa vizuri ina uwezo wa kuonesha matatizo kati ya asilimia 85 hadi 90 kwamba kwa kiwango cha asilimia 15 tu ndiyo inaweza kushindwa kuonesha matokeo.

“Hakuna duniani kifaa cha uchunguzi ambacho kinaweza kutoa majibu kwenye kila kesi, ikikosekana kwa mfano kwa kesi ya matiti akifanyiwa uchunguzi na ikionekana iko ‘inclusive’ wanaweza kuja wataalamu wa pathologia wakachukua majimaji au kinyama (sampuli) na kwenda maabara kuichunguza na vipimo vya huko vikaweza kubaini tatizo,”amebainisha.

Mtaalamu Bingwa wa Matumizi ya Mionzi katika uchunguzi wa magonjwa ya saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Stephen Mkoloma (mbele) akiwasilisha mada wakati wa semina hiyo mapema leo.

Amesema hata hivyo, licha ya kipimo hicho kuwa na uwezo mkubwa katika  kugundua saratani hiyo lakini endapo mgonjwa husika amechora tattoo kifuani mwake huwa changamoto kubwa katika kutambua picha za majibu yake.

“Tatoo ni miongoni mwa vitu ambavyo havipitishi mionzi wakati wa upimaji ili kuweza kugundua kama mgonjwa ana saratani ya matiti au la!, ‘tunapoituma’ mionzi kwenye matiti zile tattoo kwa kuwa hazipitishi mionzi, zitaonekana moja kwa moja kama zilivyo kwenye picha zetu, hii ni changamoto.

“Ni rahisi kuchanganya katika mtiririko wa matibabu ya mgonjwa, kwa sababu si mtaalamu mmoja
ambaye anamuona mgonjwa, wapo ambao huiona picha tu, sasa mtaalamu anapoiona picha anaweza kudhani ni tatizo kumbe la hasha ni urembo tu wa muhusika,” amesema.

Ameongeza “Tunaishauri jamii hasa vijana kuepuka kuchora tattoo kwenye maeneo ya mwili hasa matiti, kwa sababu tunapata tabu kufanya uchunguzi.

“Kuna wengine wanaweka hereni kama urembo, hawa wakija hatutaweza kuwafanyia uchunguzi kwa mashine hii, labda kama wataondoa kwanza vinginevyo tutatumia mashine nyingine ambazo tunazo kuwachunguza,” amebainisha.

Wataalamu wa Ocean Road wakimsikiliza mtaalamu huyo (hayupo pichani) wakati wa semina hiyo mapema leo.

Mtaalamu hiyo amesema mashine hiyo ya Mammography ni maalum ikitumia mionzi midogo katika uchunguzi wa saratani hiyo kwenye titi kwa sababu matiti ni sehemu ambazo seli zake zinaweza kuathirika zaidi mionzi inapokuwa mikubwa.

Amesema wenye umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea ndiyo wanaoshauriwa kuchunguzwa kwa kutumia mashine hiyo.

“Mgonjwa akija tunashauri asipake ‘diodolant’ (pafyumu), ‘losheni’, poda au mafuta eneo la kifua, matiti na kwapa, maana bidhaa hizo zina kemikali ambazo hazipitishi mionzi zinaweza kuonekana kwenye picha ya titi la mgonjwa ikatuchanganya tukadhani ni tatizo kumbe la hasha.

“Mwanamke akiwa kwenye hedhi hawezi kufanyiwa uchunguzi kwa kipimo hiki au akiwa katika kipindi cha kushika ujauzito (ovulation),” amebainisha.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa amesema pamoja na jitihada za Serikali kuboresha huduma za uchunguzi na tiba katika taasisi hiyo bado kuna mwamko mdogo kwa wananchi kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani hiyo.

“Ushiriki wa wananchi kufanya uchunguzi wa awali wa saratani hii tunaona mwitiko si mkubwa kulinganisha na tatizo lilivyo katika nchi yetu, taasisi imejikita kutoa elimu kuhusu vihatarishi na visababishi vinavyoweza kuchangia mtu kupata saratani hii na nyinginezo.

“Tumeboresha huduma zetu katika kitengo cha uchunguzi wa awali, Serikali imenunua mashine hii ya kisasa iliyotengenezwa mwaka 2019 kwa Sh. milioni 189, yenye uwezo wa kugundua saratani ya matiti mapema sana.

“Tumeboresha huduma za upatikanaji wa dawa za saratani za kemikali sasa ni wa kiwango cha asilmia 94,” amesema.

Ameongeza “Tumeanza mafunzo kwa wafanyakazi wetu kuwapa uelewa wa mashine hii kwa sababu tumefanya maboresho kuhakikisha hospitali hii inakuwa ya mfano katika utoaji matibabu katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

“Saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa kwenye taasisi yetu, kati ya wagonjwa 100 wanane wanaugua saratani hii na kundi linaloathirika hivi sasa linaonekana ni la wenye umri mdogo kulinganisha na miaka ya nyuma,”amesema.

Amesema hata wastani wa umri umepungua kutoka miaka 70 hadi 57 na hata wale wenye umri wa miaka 24 kitu ambacho hakikuwa cha kawaida na wengi hufika ugonjwa ukiwa kwenye hatua za juu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news