Mvua yaua 12 Dar, majina yatajwa

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibithisha kuwa, watu 12 wamefariki dunia jijini Dar es Salaam kwa mafuriko kutokana na mvua iliyonyesha Oktoba 13 na Oktoba 14, 2020 kuanzia alfajiri ambayo iliendelea kwa siku nzima na kupelekea mafuriko baadhi ya maeneo jijini humo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

"Miili ya watu watano ilipatikana kando kando ya Mto Msimbazi eneo la Jangwani, kati ya hao watu wawili walifahamika kwa majina kama ni Herieth Kanuti (18) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Lutihinda.

"Mwingine ni Ipyana Mwakifuna (19) mkazi wa Jangwani ambaye ni askari jeshi la akiba la mgambo na miili mingine ya watu watatu bado haijatambuliwa ikiwa ni wanaume wawili na mwanamke mmoja,"Kamanda Mambosasa ameyasema hayo leo Oktoba 16,2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema, tukio lingine la kifo limeripotiwa Oktoba, 14,2020 majira ya saa 12:45 huko Tabata ambapo mwili wa mtu mmoja mwanaume aliyefahamika kwa majina ya Philipo Feliciani (30) mkazi wa Tabata Kimanga, ulionekana ukiwa umenasa kwenye matope katika mto Tenge baada ya kudondoka na kusombwa na maji alipojaribu kuvuka kwenye daraja la waenda kwa miguu Tabata Kimanga.

Pia amesema, mwili wa mtu mmoja mwingine mwanaume asiyefahamika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30 hadi 35 alikutwa akiwa amefariki dunia katika eneo la Ukonga Sabasaba Manispaa ya Ilala.

Mbali na hao amesema, jumla ya watoto wawili wa familia moja na watu wazima wawili walifariki dunia kutokana na athari za mvua akiwemo Ibrahim Hassan (24) mkazi wa Kigogo Buyuni, Hussein Awadhi (5) mkazi wa Kigogo Buyuni na Bakari Awadhi (14) mkazi wa Kigogo Buyuni.

"Watoto hao walifariki dunia kwa kusombwa na maji baada ya nyumba yao iliyopo katika bonde la Kigogo kujaa maji na watoto hao kushindwa kujiokoa na marehemu Ibrahim Hassan alijaribu kumuokoa mtoto mmoja, lakini na yeye akasombwa na maji na kufariki dunia. 

"Pia Oktoba 14, 2020 majira ya saa mbili asubuhi huko Mabibo mwili wa mtu mmoja mwanaume asiyefahamika anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 35 ulionekana unaelea kwenye mfereji unaopeleka maji katika mto Msimbazi.Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,"amesema Kamanda Mambosasa leo Oktoba 15,2020.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news