Mwalimu Makuru Lameck Joseph atoa ombi maalum Oktoba 28 kwa wana Musoma

Aliyekuwa miongoni mwa makada wa chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitosa kuwania nafasi ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kwenye kura za maoni kugombea Ubunge katika Jimbo la Musoma Mjini,Mwalimu Makuru Lameck Joseph amewaomba Watanzania wote kuthamini juhudi kubwa za maendeleo zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.
Mwalimu Makuru Lameck Joseph akiomba kura za mafiga matatu katika Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma leo.(Diramakini).
 Ni chini ya Uongozi wa Serikali ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli na hivyo wamchague kwa kishindo ili arudi madarakani akaendelee kuwaletea maendeleo Watanzania na Serikali atakayoiunda.

Mwalimu Makuru amesema, uongozi wa Rais Magufuli unapaswa uthaminiwe na kila mmoja kwani umelifanya Taifa kupaa kiuchumi kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati nchini ikiwemo ununuzi wa ndege, upanuzi wa viwanja vya ndege mikoa mbalimbali nchini,reli ya kisasa, utoaji elimu bure.

Pia uongezaji wa bajeti ya ununuzi wa madawa, kujenga hospitali za mikoa na wilaya,zahanati,vituo vya afya, ujenzi wa masoko, ukarabati wa shule kongwe zaidi ya 70 nchini na mingine mingi.

Mafanikio mengine ni kuongeza idadi ya fedha za mikopo kwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya vyuo vikuu nchini, kurekebisha mikataba ya madini kwa faida ya Watanzania, kuhamishia makao makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, kuajiri wafanyakazi katika sekta mbalimbali, kulifikisha Taifa Katika uchumi wa kati.
Sambamba na kukusanya mapato kwa kiwango thabiti na hivyo kuwezesha Serikali kugharimia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa fedha za ndani zaidi ya Shilingi Bilioni 300 bila kutegemea misaada kutoka nchi za nje.

Ameyasema hayo leo Oktoba 15,2020 wakati akiomba kura za mafiga matatu ikiwemo udiwani, ubunge na Urais katika Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma, ambapo pamoja na mambo mengine Mwalimu Makuru amewasisitiza Watanzania kutofanya majaribio kwa kuchagua wapinzani ambao amedai hawawezi kufanya maendeleo yoyote kwa wananchi.

 Amewasisitiza wakazi wa Kata ya Bweri wamchague Mgombea udiwani wa CCM, Dickson Mwandara, Mbunge Mathayo na Rais Magufuli kusudi wakashirikiane kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya kweli kwa manufaa ya wananchi.

"Rais Magufuli amefanya mambo mengi mazuri kwa kipindi cha miaka mitano tu, je? tukimpa miaka mingine mitano tena si nchi yetu itakuwa kama Ulaya," amehoji na kusema.

"Katika ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2020-2025 imeainisha mambo mengi ambayo yatatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania,mfano maji, huduma za afya, kushughulikia kero za wakulima, na mambo mengi kedekede, cha msingi sisi sote tuliojiandijisha tujitokeze kwa wingi kuwapatia kura wagombea wote wa CCM Oktoba 28,mwaka huu, tuchague Chama Cha Mapinduzi tukiamini kwamba ndicho chama pekee chenye ilani bora na yenye kutekelezeka kwa maslahi mapana ya Watanzania waoshio mijini na Vijijini,"amesema.

Naye Buhabi Musilanga ambaye ni Kada wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma, amesisitiza wanachama wa chama hicho na wananchi wote, kuendelea kudumisha umoja, upendo na mshikamano, huku aliwasihi vijana kutotumika kuvuruga amani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na hata baada ya uchaguzi.

No comments

Powered by Blogger.