Mwenyekiti CCM Mara asema Rais Magufuli atafunga hesabu mapema Oktoba 28

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) amesema kuwa, ushindi wa Chama hicho katika nafasi ya Urais, wabunge na madiwani mkoani hapo Oktoba 28,mwaka huu utakuwa wa mapema asubuhi kutokana na namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano, miaka mitano iliyopita imetekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

“Awamu ya Tano katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 imetekeleza kwa asilimia zaidi ya 100 Ilani ya Uchaguzi, jambo ambalo limewafanya Watanzania kuwa na imani zaidi kwa Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli ambaye Jumatano ijayo kwa umoja wetu wana CCM na wananchi Mkoa wa Mara tumemwandalia zawadi ya kipekee.

“Hii zawadi si nyingine bali ni ushindi wa kishindo kwa mafiga matatu, yeye (Dkt.Magufuli) anakwenda kupata ushindi wa kutosha wa kwenda kuwatumikia Watanzania kwa miaka mitano tena, wagombea ubunge wa CCM, wanakwenda kupata kura za kutosha vivyo hivyo kwa madiwani, Watanzania tumeridhia kwa dhati kabisa kutoa ushindi huo kwa kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais Magufuli ambaye amekuwa mtetezi wa wanyonge;

Kiboye ameyasema hayo mkoani Mara wakati akizungumza juu ya tathimini ya kampeni za wagombea wa chama hicho mkoani hapo, huku akibainisha kuwa, kwa asilimia 100 wameendelea kufanya kampeni za kistaarabu, zilizojielekeza katika kunadi sera na ilani ya chama kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025.

Amesema kuwa, wagombea wa CCM wameongoza mkoani humo kwa kuendesha kampeni zenye mvuto na hamasa kutokana na namna ambavyo wagombea hao wanajinadi kwa wananchi huku wakijikita kuyajibu maswali na kero ambazo wananchi wanahitaji zikapatiwe ufumbuzi.

“Wagombea wetu wamejikita sana kunadi sera na ilani ya chama, hivyo kuwapa wananchi nafasi ya kuelewa ni kwa namna gani ambavyo wakiwapa kura zao Oktoba 28, mwaka huu wanakwenda kutekelezewa mahitaji yao ikiwemo kushirikiana na Serikali kuzikabili baadhi ya changamoto na kukamilisha miradi ambayo inaendelea na watakayobuni,” amefafanua Kiboye.

Pia Kiboye amesema, mafanikio ya utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo chini ya Rais Dkt.Magufuli ikiwemo katika sekta ya elimu, afya, miundombinu, nishati,maji, usafirishaji wa angani, majini na nchi kavu ikiwemo mingine mingi inazidi kuwapa nguvu Watanzania na kuona kuwa, kwa sasa hakuna mbadala wa chama hicho tawala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news