Nyongo ataka ajira za mgodi mpya zitolewe kwa wazawa

Mgodi mpya wa Singida Gold Mine, uliozinduliwa mkoani Singida wilayani Ikungi umeagizwa kuzingatia utoaji wa ajira za wafanyakazi mgodi hapo huku kipaumbele kikiwa kwa wananchi wanaozunga mgodi huo,anaripoti Issa Mtuwa (WM), Singida.
Mkurugenzi wa Singida Gold Mine, Filbert Rweymamu akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo baada ya uzinduzi wa Singida Gold Mine.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo katika hafla ya uzinduzi wa mgodi huo Oktoba, 2020. Ameongeza kuwa, uwepo wa mgodi huo utakuwa chachu ya maendeleo kwa Wanasingida na nchi nzima kwa ujumla. 

Nyongo amesema, kwenye mgodi huo kuna fursa nyingi zitakazotolewa kwa wananchi kushiriki mambo mbalimbnali ndani na nje ya mgodi alitoa mfano biashara, ulinzi, ajira rasmi na ajira zisizo rasmi. Ameongeza kuwa,kodi itakayolipwa na mgodi kwenye halmashauri fedha zake zitakwenda kutumika kwa ajili ya maendeleo Ikungi.

Akizungumzia ulipaji wa maduhuli ya Serikali, Nyongo amesema, Wizara ya Madini iko mstari wa mbele kuchangia pato la Serikali. "Mwaka jana tulipangiwa kukusanya bilioni 470, mpaka kufikia mwisho wa mwaka, Wizara iliweza kukusanya kiasi cha bilioni 528. Mwaka huu 2020/2021 wizara imepangiwa kukusanya maduhuli ya Serikali bilioni 526.9,"amesema. 
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akifuatilia kwa makini katika uzinduzi wa wa Singida Gold Mine Ikungi mkoani Singida.

Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini amesema, kuzinduliwa kwa mgodi huo, kunaongeza wigo wa kukusanya maduhuli ya Serikali ambayo yanakusanywa na Tume ya Madini. Hivyo kuwe na mpango wa haraka wa kuanza kuzalisha.

Meneja Mkuu wa Singida Gold Mine, Filbert Rweymamu amemwambia rgeni rasmi, Naibu Waziri wa Madini kuwa, mgodi umejipanga kushirikiana na Wanaikungi na kuweka mipango ya kuwainua wananchi kimaendeleo. Amesema, wamepanga kutoa ajira kwa wafanyakazi 200 kipaumbele kikiwa wananchi wa Ikungi na Singida. 

Kuhusu kushirikiana na wachimbaji wadogo, mgodi umepanga kutoa mafunzo ya wachimbaji wadogo kuhusu namna ya uchimbaji salama katika maeneo yao. 
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akihutubia hadhara ya uzinduzi wa ujenzi wa Singida Gold Mine, Ikungi mkoani Singida kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi.

Akizungumzia mchango kwa taifa, Rweymamu amesema, wanazingatia sheria mpya ya madini inayoipa Serikali kwa niaba ya wananchi, umiliki wa asilimia kumi na sita (16% free carried interest) watazilipa kodi kama zitakavyobainishwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amesema, amefurahi kuzinduliwa mgodi huo ili uanze uzalishaji. Uzalishaji utakapoanza anategemea vijana wa Singida hawatakuwa na muda kwenda Dodoma Makao Makuu kwakuwa ajira hapa zitakuwa za kutosha kwa watakao ajiriwa ndani na wengine watajiajiri kwa kupeleka bidhaa na huduma mgodini.
Baadhi ya viongozi mbalimbali waliohudhuria kwenye uzinduzi wa Singida Gold Mine.

Kwa upande wa wananchi kwa nyakati tofauti, wamefurahia kuzinduliwa mgodi huo kwani wana matumaini kwa kuwa kutakuwa na fursa nyingi zitakazo tolewa. Wameomba fursa za mgodi wapewe kipaumbele wanaozunguka mgodi. 

Waziri wa Madini, Doto Biteko aliwahi kusema; "Geita kuna dhahabu lazima dhahabu iwanufaishe wana Geita, Tanga kuna vipepeo vya kipekee ambapo watalii hufika kuviangalia, vipepeo hivyo lazima viwanufaishe Wanatanga, Shinyanga kuna Almasi, lazima Almasi hiyo iwanufaishe Wanashinyinga, hata korosho kule Mtwara lazima ziwanufaishe Wanamtwara". Kwa maelezo ya Biteko, dhahabu hii ya Singida lazima iwanufaishe watu wa Singida kutokana na fursa ya uwepo wa dhahabu.

No comments

Powered by Blogger.