Rais Dkt.Shein aagwa rasmi Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amelitaka Baraza la Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kuendelea kushirikiana na kuongeza bidii na ubunifu katika kuiendeleza Programu ya Ufundishaji wa Kiswahili ili kufikia dhamira ya kuifanya SUZA kuwa ‘Oxford ya Kiswahili’, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Zanzibar).

Dkt.Shein ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) alitoa rai hiyo katika hafla ya kuagwa, baada ya kukiongoza chuo hicho kwa miaka kumi, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema, ni vigumu kuzungumzia historia na maendeleo ya Kiswahili bila kuzungumzia historia na maendeleo ya kiutamaduni wa Zanzibar, huku akibainisha kuwa Zanzibar ni nchi ya Kiswahili kinachozungumzwa kwa ufasaha katika maeneo ya mjini.

Alisema, watu wengi huridhika kupata tafsiri ya maneno kutoka makamusi ya Kiingereza kutoka ‘Oxford’ kuliko makamusi mengine duniani, jambo ambalo linaweza kufikiwa nchini kwa kuweka nguvu katika kuikuza na kuiendeleza lugha hiyo.

Aidha, alihimiza umuhimu wa kuimarisha skuli ya Kiswahili na lugha za kigeni ili kuifanya Zanzibar kuwa ‘Centre of Exellence’.

Alieleza kuwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki imefungua kituo cha Kiswahili katika eneo la Gymkhana hapa Zanzibar, hivyo ni vyema SUZA ikachangamkia jambo hilo na kuwa kituo cha Kiswahili.

Dkt.Shein alisema ni jambo la kufurahisha hivi sasa Zanzibar kuwa na vyuo vikuu vitatu ambavyo kwa wastani hutoa wahitimu 3,000 kila mwaka na kubainisha umuhimu wa Wazanzibari kusoma elimu ya juu hapa nchini, kwani itamuwezesha mhitimu kufahamu changamoto ziliopo na jinsi ya kuisaidia jamii.

Akigusia mafanikio ya SUZA katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, Dkt.Shein alisema katika kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa wataalamu, imeanzisha fani mbalimbali ili kwenda sambamba na mahitaji.

Alisema, katika kipindi hicho kuna mafanikio makubwa ya kielimu yaliofikiwa kupitia SUZA , ikiwemo uanzishaji wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba pamoja na mafunzo ya Udaktari (doctor of Medicine), mafunzo yalioanza mwaka 2017/2018 na wanafunzi 25 kufaulu pamoja na wengine 48 waliofanikiwa kumaliza masomo yao mwaka 2018/2019.

Alisema, SUZA imefanikiwa kuanzisha mafunzo ya shahada ya kwanza ya udaktari wa meno mwaka 2019/2020 ambapo jumla ya wanafunzi sita wanaendelea vizuri na masomo hayo.

Rais Dkt.Shein alisema, jitihada za kusomesha madaktari ndani na nje ya nchi zimewezesha kuongeza idadi ya madaktari na watumishi wengine wa afya nchini, akibainishwa kuwepo uwiano wa madaktari na watu wanaowahudumia.

Alisema, hivi sasa daktari mmoja anawahudumia watu 6,276 kutoka wastani wa daktari mmoja aliyekuwa akiwahudumia watu 31,838 mnamo mwaka 2010.

Alisema, lengo hilo linaendana na Manifesto ya Chama cha Afro Shirazi pamoja na kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kwa nchi zinazoendelea cha daktari mmoja kuwahudumia watu 10,000.

Alieleza kuwa, katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, chuo hicho kimefanikiwa kupata Ithibati kamili (full Accreditation) ya Tume ya Vyuo vikuu Tanzania (TCU) .

Aidha, alisema Serikali ilifanya uamuzi wa kuziunganisha na SUZA taasisi mbalimbali, ikiwemo Chuo cha Utawala wa Fedha Chwaka, Chuo cha Kilimo Kizimbani, Chuo cha Habari Kilimani, Chuo ca Afya Mbweni pamoja na Chuo cha Utalii Maruhubi, kwa lengo la kuinua hadhi na kiwango cha elimu inayotolewa na taasisi za elimu ya juu.

Hata hivyo alisema wakati vyuo hivyo vinaunganishwa na SUZA wako watu walioonyesha kutokuelewa, hivyo akatumia fursa hiyo kuipongeza Kamati maalum iliyoundwa kushauri na kutoa mapendekezo ya kuunganisha vyuo hivyo.

Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alitoa shukurani kwa Mkuu wa Chuo hicho kwa juhudi kubwa za kusimamia mendeleo ya chuo hicho pamoja na hatua za kuhamasisha elimu ya juu kwa akinamama, hivyo kuongeza ufaulu kwa jinsia hiyo kwa kiwango cha juu. 

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Said Bakari Jecha alisema, katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Dkt.Shein, SUZA imepata mafanikio makubwa na ya haraka na kufanikiwa kupata umarufu mkubwa wakati ambapo vyuo vingi Duniani hupata mafanikio kama hayo baada ya miaka mingi kupita.

Akisoma maelezo hayo kwa niaba yake, mwanatalaamu Mwita Mgeni alisema,chuo hicho kimetekeleza kikamilifu Ilani ya CCM ambapo pamoja na mambo mengine kwa zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi wanasoma kupitia mikopo inayotolewa serikalini.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa chuo hicho, Dkt.Zakia Mohamed Abubakar alisema katika kipindi cha uongozi wake, Dkt. Shein alifanya juhudi kubwa kukiendeleza chuo hicho kiasi cha kupata mafanikio ya kupigiwa mfano, ikiwemo kukuza ubora wa elimu kufuatia hatua za uimarishaji wa miundo mbinu ya elimu, nguvu kazi pamoja na upatikanaji wa maslahi bora.

Alisema, kutokana na msukumo mkubwa wa Dkt.Shein, chuo hicho kimeweza kuanzisha ‘SUZA TV’ iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa taaluma kwa wanafunzi wa sekondari, hususan wanaosoma masomo ya Sayansi na Hisabati.

Katika hatua nyingine, mwanataaluma Ameir Mohamed Makame, akisoma risala ya wanataaluma, alitoa pongezi kwa Dkt.Shein kwa mchango mkubwa wa kukiendeleza chuo hicho ndani ya kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake kwa kuangalia maslahi yao pamoja na kuwepo uwazi katika suala la upandishaji vyeo.

Alisema, katika kipindi hicho wanataaluma walipata fursa za masomo ndani na nje ya nchi pamoja na kupata nyadhifa za kufanyakazi katika maeneo mbalimbali.

Alisema, jumuiya ya wanataaluma inampongeza kwa dhati Dkt. Shein kwa hatua ya kuwaamini na kuwateua wanataaluma wanawake kushika nyadhifa za kuiongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja chuo hicho.

Hata hivyo, mwantaaluma huyo alisema bado kada hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya kuwepo idadi ndogo ya wanataaluma katika kiwango cha shahada ya uzamivu.

Aidha, aleleza kuwa wanataaluma wa SUZA wanakabiliwa na kuwepo kwa tofauti kubwa ya maslahi (mishahara) kati yao na wenzao wanaovitumikia vyuo vikuu mbalimbali Tanzania Bara.

Ameir alieleza matumaini makubwa waliyonayo wanataaluma wa SUZA ya kuwa Mkuu wa chuo hicho ajae atayapatia ufumbuzi masuala hayo ili kuwatia moyo wanataaluma.

Katika hafla hiyo, viongozi mbalimbali wa Serikali walihudhuria akiwemo Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mgombea wa Urais kupitia CCM Dkt. Hussein Ali Mwinyi, mawaziri pamoja na wake wa viongozi wakuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news