Rais mstaafu Pierre Buyoya ahukumiwa maisha jela

Mahakama Kuu nchini Burundi imemhukumu aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Pierre Buyoya kifungo cha maisha gerezani bila yeye kuwepo mahakamani, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, Rais Buyoya amehukumiwa pamoja na watu wengine 18 kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya aliyekuwa rais wa kwanza wa Burundi kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia, Melchoir Ndadaye.

Kwa mujibu wa Mahakama, watu hao19 wamepatikana na makosa ya kushambulia kiongozi wa nchi, na kujaribu kusababisha machafuko, mapigano na mauaji ya halaiki ya watu nchini Burundi.

Mashtaka dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Antoine Nduwayo yamefutwa baada ya ushahidi dhidi yake wa kushiriki katika njama hiyo kukosekana.

Rais Buyoya ambaye sasa anafanya kazi kama Mwakilishi Maalum na Kiongozi wa Ujumbe wa Amani wa kimataifa unaongozwa na Afrika (AFISMA) nchini Mali amekuwa akitafutwa na mamlaka nchini Burundi baada ya kibali cha Kimataifa kutaka akamatwe na kupelekwa nchini humo kutolewa mwaka 2018.

Kibali hicho cha kukamatwa kilitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Burundi , Sylvestre Nyandwi kwa kushukiwa kupanga njama za kumuua rais wa kwanza kutoka jamii ya Hutu, marehemu Ndadaye aliyeuawa siku kama ya leo Oktoba 21, 1993 zikiwa ni siku 102 baada ya kuapishwa kuwa Rais nchini humo.

Buyoya ambaye anatoka jamii ya Watutsi ametaja mashtaka dhidi yake kuwa mbinu ya kugawanya nchi na kubadili mawazo ya watu kutokana na matatizo yanayoikumba nchi hiyo. Burundi tangu ipate Uhuru mwaka 1962 kutoka kwa wakoloni wa Kibelgiji wamekuwa wakipitia katika kipindi cha vuta ni kuvute ambacho kinachochewa na makabila mawili yenye nguvu ya Wahutu na Watutsi.

No comments

Powered by Blogger.