Rais Shein awaaga Wazanzibar asema amewaachia amani, utulivu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amewaaga wananchi wa Zanzibar na kuwaambia kuwa Awamu ya Saba imefanya mambo mengi huku akisema kuwa anawaachia zawadi ya amani na utulivu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Ali Mohamed Shein akionesha Kitabu cha Dira ya Maendeleo ya Zanzibar kwa mwaka 2050, baada ya uzinduzi huo uliofanyika katika
Uwanja wa Mao Zedong jijini Zanzibar leo Oktoba 19,2020 na kushoto kwa  Rais ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman.(Picha na Ikulu).

Dkt. Shein ameyasema leo Oktoba 19,2020 katika viwanja vya Mao Dze Dong jijini Zanzibar katika hotuba yake ya kuwaaga wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar pamoja na kuzindua Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050.

Hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mama Mwanawema Shein, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni mgombea kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, mawaziri, na viongozi wengine wa vyama vya siasa, dini na serikali.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Shein amesema kuwa, mbali ya jitihada alizozichukua za kuwaachia wananchi mifumo na vitu ambavyo vitarahisisha mwenendo wao wa kujipatia huduma za maisha vile vile anawaachia zawadi ya amani na utulivu.

Rais Dkt. Shein amewasishi wananchi kuzidisha upendo, umoja na mshikamano miongoni mwao ili zawadi hiyo anayowaachia iweze kudumu na kung’ara zaidi.

“Zawadi hii ya amani na utulivu mtaweza kuitumia nyinyi na vizazi vitakavyokuja baadae kwa hivyo itunzeni sana na muilinde kwa nguvu zenu nyote,”amesema Rais Dkt. Shein.

Aidha, Rais Dkt. Shein amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba bila ya kutetereka kinyume na matarajia ya wale waliokuwa hawaitakii mema imefanya mambo mengi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Amesema kuwa, Serikali imefanikiwa kuyatekeleza mambo ya maendeleo kwa kuzingatia shida na kero kadhaa zilizokuwa zikiwakabili wananchi kwenye huduma za msingi za jamii.

Ameongeza kuwa, wananchi wamekuwa wasikivu katika kufuata taratibu na sheria za nchi mambo ambayo taasisi zilizopewa majukumu ya ukusanyaji wa mapato zimeweza kufanya vizuri sana.

Dkt. Shein amewapongeza wananchi kwa usikivu wao hasa pale lilipotokea janga la COVID 19 ambapo waliweza kufuata maelekezo yote ya Serikali na yeye pamoja na Serikali anayoiongoza kwa ushirikiano na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli walikuwa makini katika kuwapa maelekezo wananchi.

Amesema kuwa, wananchi wa Zanzibar kila pembe wanathamini jitihada zilizochukuliwa na Serikali yao katika kuleta maendeleo yenye manufaa kwao na kuziunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo yenye ufanisi ambayo wanajivunia.

Rais Dkt. Shein ametoa shukurani kwa zawadi alizotunukiwa na wananchi na kueleza kuwa hicho ni kielelezo cha jinsi wanavyomjali na yeye kwa upande wake anawajali, anawathamini na anawapenda wote wananchi wake.

Katika hotuba yake hiyo aliwapongeza viongozi wote wakuu wa SMZ na SMT pamoja na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wataalamu wote wa Tume ya Mipango kwa kuiwasilisha Dira ya Zanzibar 2015 kwa wananchi pamoja na kuwapongeza wakuu wa vikosi vya SMZ na SMT.

Amewapongeza viongozi wote wa Chama na Serikali pamoja na Wakuu wa Mikoa Mitano ya Zanzibar na Wilaya, watendaji wengine wote, masheha na Madiwani pamoja na Wazee wa CCM kwa busara, hekima na maendeleo yao ambayo kwa wakati wote yalikuwa na manufaa kwa ustawi wa nchi.

Kwa upande wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 imetengenezwa kwa utaalamu wa hali ya juu kutokana na uzoefu ambao wataalamu wazalendo wamekwishaupata kwenye shughuli ya namna hiyo.

Amesema kuwa, maandalizi ya Dira ya 2050 yamezingatia mabadiliko ya haraka ya sayansi na teknolojia duniani fursa zinazojitokeza katika sekta zinazoibua zikiwemo uchumi wa kutumia rasilimali za bahari (uchumi wa Buluu), mtehama, mafuta na gesi asilia.

Ameongeza kuwa, katika Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imepata mafanikio mengi kupitia utekelezaji wa Dira ya 2020 na mafanikio makubwa yamepatikana hiyo ni kutokana na kuwa yako wazi.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Shein amewahimiza wananchi kwa kila aliyetimiza masharti yaliyowekwa na Tume kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 28 Oktoba, 2020 kwenda kupiga kura ili wasipoteze haki yao ya demokrasia.

Amewataka wananchi kuchagua viongozi wakweli na wenye nia njema ya kuwaletea wananchi maendeleo yanye manufaa na wala wasichague viongozi wanaotaka kuielekeza nchi katika shari na mfarakano.

Amewataka kuangalia maslahi ya nchi yao ambayo ndiyo yatakayowawezesha kuishi vizuri wakiwa nchini mwao “Wahenga wanasema mtu kwao ndio ngao na anayebomoa kwao ni mtumwa”, alisisitiza Dkt.Shein.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Muhammed Ramia Abdiwawa alieleza kuwa Dira hiyo ni ya watu wote na Dira ya 2020 Rais Dk. Shein aliisimamia na hiyo mpya inatokana na miongozo yake huku akisema kuwa Dira ya 2050 ni ya vijana zaidi.

Amesema kuwa, dira hiyo itajikita zaidi katika mageuzi ya Kiuchumi na kusisitiza kuwa Dira hiyo itakuwa ndio muongozo wa miaka 30 ijayo ambayo imefanywa na wataalamu wa ndani kwa mara ya kwanza na kuwashikirisha wananchi hadi vijijini na ambayo itapekekea kufikia uchumi wa juu ifiapo 2025 ambapo kila mwananchi anatarajiwa kuwa na kipato cha Dola za Marekani 4400 kwa mwaka.

Mapema Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Mwita Mgeni alitoa historia ya kuundwa Dira hapa nchini na kusema kuwa utayarishaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 ilipitia kwa wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na Kamati ya Makatibu Wakuu, wajumbe wa Tume ya Mipango na hatimae ridhaa ya Baraza la Mapinduzi.

Amesema kuwa, dira hiyo ina muundo na lengo ni kuifikisha Zanzibar katika uchumi wa kati wa kiwango cha juu ifikapo mwaka 2050, pamoja na vipaumbele kadhaa.

Amesema kuwa, dira hiyo itakuwa ni msingi imara wa kutoa mashirikiano ya pamoja katika maendeleo yatakayosukuma utendaji thabiti wa sekta binafsi katika kuendeleza uchumi

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hemed Suleiman akisoma hotuba kwa niaba ya wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar alimpongeza Rais Dkt. Shein kwa kuiwacha Zanzibar ikiwa na amani na utulivu sambamba na uongozi wake imara wenye hekima na busara.

Amesema kuwa, Zanzibar inaendelea kuwa na amani na ndio maana imekuwa kivutio kikubwa cha watalii ambapo pia, katika uongozi wa Rais Dkt. Shein kumepatikana mafanikio makubwa ikiwemo kuimarika kwa sekta za maendeleo ikiwemo kilimo, elimu, biashara,afya, maji safi na salama, kuimarika kwa sekta ya utalii, ujenzi wa barabara, majengo ya ofisi za Serikali, biashara na huduma nyengine.

Aidha, ameeleza hatua alizozichukua za ujenzi wa misingi mikubwa ya maji ya mvua, pamoja na ujenzi wa madaraja, eneo la Mwanakwerekwe ambalo lilikuwa likituama maji huku akieleza historia aliyoandika kwa kuongeza mishahara kwa sekta ya umma na sekta binafsi.

Amesema kuwa, wananchi wameridhika na uongozi wa Rais Dkt.Shein pamoja na maendeleo aliyowaletea wananchi wa Zanzibar na kuahidi kuyadumisha na kuyaimarisha yale yote aliyowaachia.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alizitaja zawadi alizotunukiwa Rais Dk. Shein pamoja na Mama Mwanamwema Shein kutoka kwa Mikoa yote Mitano ya Zanzibar.

Katika hafla hiyo burudani mbalimbali zilitumbuiza zikiwemo zile za asili pamoja na zile za kizazi kipya ambapo ngoma ya Tukulanga, Kibati zilitumbuiza pamoja na wasanii wa kizazi kipya akiwemo IT na ZUCHU.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news