Siku ya Ushairi wa Watoto Duniani yatumika kupeleka ujumbe maalum kwa wazazi,walezi

Wakati Siku ya Ushairi wa Watoto World Children’s Poetry Day (WoChiPoDa) ikiadhimishwa katika maeneo mbalimbali duniani kote, wazazi, walezi na walimu nchini wameaswa kuwapa fursa watoto wao ya kushiriki katika mafunzo na matamasha ya uandishi wa ushairi na usomaji vitabu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Lengo ni kuwajengea uwezo wa kuandika maandiko mbalimbali kulingana na mazingira wanayoishi, kwani kufanya hivyo kutasaidia kuibua na kuendeleza vipaji vyao katika kuliletea taifa maendeleo kwa siku za baadae.
Hayo yalisemwa na Mratibu wa siku ya ushairi WoChiPoDa mkoa wa Pwani, Bi. Rehema Kawambwa alipokua akizungumza katika maadhimisho ya siku ya ushairi wa watoto duniani yanayofanyika Jumamosi ya kwanza ya mwezi Oktoba ambayo mwaka huu yalifanyika katika shule ya msingi Kiluvya ‘B’ Kisarawe mkoani Pwani.

Rehema alisema ili kujenga uelewa kwa watoto kulingana na mazingira wanayoishi ni wazi kuwa ipo haja ya kila mzazi kutambua kuwa watoto wanayo haki ya kushiriki katika matamasha kama hayo ambayo yatawajengea uwezo wa kuwa waandishi wa ushairi na insha na vitabu mbalimbali vya hadithi na hatimae kuwa sehemu muhimu ya kuielimisha jamii ya watanzania.

Alienda mbali zaidi na kusema kuwa kazi ya uandishi ni kazi kama kazi zinginine hivyo endapo mtoto ataandaliwa vizuri na kuwa mwandishi mzuri si tu atakua sehemu ya kuwaelimisha wengine lakini pia ujuzi na kipaji alichonacho kitamsaidia kujiingizia kipato kama ilivyo kwa waandishi wengine wenye majina makubwa kote ulimwenguni.

‘’Ushiriki wa watoto wetu katika matamasha kama haya yanatoa fursa ya kuwajenga na kuwapata washairi wengi kwani ikizingatiwa hivi sasa hamasa ya kusoma vitabu imeshuka hivyo kwa hatua hiyo itasaidia kupata taifa lenye watu wanaopenda kusoma vitabu kwa siku za usoni,"alisema Rehema.

‘’Pia niende mbali zaidi uandishi wa ushairi pia utamuongezea mtoto kuendana na mazingira halisi hivyo kuandika mashairi kutamsaidia pia kuandika vitabu ambavyo faida zake kwa baadae ni kuviingiza sokoni ili kuwanufaisha kibiashara hivyo ni jukumu la wazazi kujitoa kwa kila hali ili kuwapa nafasi ya kujiinua kicunhumi kupitia uandishi,"alisema.

Naye mdau wa elimu ambae pia ni mzee maarufu katika Kata ya Kiluvya wilayani Kisarawe, Mohammed Kweku amesema ili kupata taifa zuri kwa siku za baadae ipo haja ya wazazi kutumia fursa mbalimbali za kielimu ambazo zimekua zikijitokeza ili kuwaimarisha zaidi badala ya kuwanyima nafasi hizo na hivyo kupelekea kujiingiza katika matukio yasiyofaa.

"Kutokana na watoto wengi kuharibika kimaadili ni wakati wao sasa wazazi tukatumia nafasi hizi zinazotolewa na wadau wa elimu katika kuwahamasisha na kuwashinikiza watoto kushiriki ili kuondokana na tabia ya kushinda shinda mitaani hususani katika siku za mapumziko ili kuwaepusha watoto wetu na makundi yakatayochangia kumomonyoka kwa maadili.’’alisema.

Wakizungumza kwa niaba ya watoto walioshiriki katika tamasha hilo wanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Kiluvya ‘B’ Abdallah Mbonde na Noela Urasa walisema kuwa kupitia tamasha hilo kutawafanya kupanuka kimawazo kwani ikizingatia hivi sasa taifa limejikita katika ukuaji wa Tanzania ya viwanda hivyo uandishi wa vitabu vya ushairi utawawezesha kuendeleza vipaji vyao.

Lakini pia kama chanzo cha biashara, kwani kupitia viwanda vya uchapishaji ili kuliendeleza taifa. Siku ya uandishi wa uandishi wa ushairi kwa watoto ilianzishwa mnamo mwaka 2014 na Bi. Gloria Gonsalves aishie nchini Ujerumani ambaye pia ni mwandishi wa vitabu na mashairi ikiwa na lengo la kuinua vipaji vya watoto kuwaweka pamoja na kwa kuwapa motisha ya kupenda na kujifunza uandishi wa mashairi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

2 Comments

  1. Shukrani zangu za dhati kwa sapoti yenu katika huu mpango (initiative) wa WoChiPoDa.

    ReplyDelete
  2. Hongereni sana Diramakini kwa habari hizi. Ni kati ya habari ambazo haziripotiwi sana, lakini zina tija kubwa kwa ustawi wa watoto wetu, niwape hongera walioasisi mpango huu wa usomaji vitabu

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news