Simba SC wapinduliwa, Yanga SC yapindua, Azam FC kileleni

Ipo hivi, Oktoba 22,2020 inakuwa siku ya mawazo kwa mabingwa watetezi, Simba SC baada ya kupoteza mechi ya kwanza ya msimu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ni baada ya kuchapwa bao 1-0 na wenyeji wao Tanzania Prisons, Uwanja wa Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu, wanabaki na alama zao 13 baada ya kipigo cha leo, sasa wakizidiwa pointi tatu na mahasimu wao, Yanga SC baada ya timu zote kucheza mechi sita, wakati Azam FC wanaendelea kuongoza kwa pointi zao 21 za mechi saba.

Yanga SC VS Polisi Tanzania FC katika dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam.

Simba SC Vs Tanzania Prisons Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga.
Bao lililoizamisha Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck limefungwa na mshambuliaji Samson Mbaraka Mbangula 49' akimalizia kazi nzuri ya beki Michael Ismail Mpesa.

Ushindi wa huo kwa Tanzania Prisons unawafanya wafikishe alama tisa baada ya kucheza mechi saba na wanapanda kutoka nafasi ya 14 hadi ya tisa kwenye Ligi Kuu ya timu 18.

Wakati Simba SC wakipinduliwa, mahasimu wao Yanga SC wameichapa 1-0 Polisi Tanzania bao pekee la kiungo Mukoko Tonombe 70' katika Uwanja wa Uhuru uliopo Jiji la biashara Dar es Salaam.

Huo ni ushindi wa kwanza kwa kocha mpya ambaye ni raia wa Burundi, Cedric Kaze baada ya kuiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza.

Tonombe au Teacher kutokana na staili yake ya ushangiliaji ambaye huu ni msimu wake wa kwanza tu tangu asajiliwe kutoka AS Vita ya nyumbani kwao, Kinshasa amefunga bao ameendelea kujadiliwa na mashabiki wa Yanga kwa kazi nzuri huku wakimpongeza kwa kuwafuta machozi, matokeo ambayo yalichangiw na pasi ya kiungo, Feisal Salum.

Kwa sasa Yanga SC inafikisha alama 16, sasa ikizidiwa tano na vinara Azam FC ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi

No comments

Powered by Blogger.