TAKUKURU Temeke yang'ata, Afisa Tabibu aingia mikononi

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam katika kipindi cha mwezi Julai, 2020 hadi Septemba, 2020 imefanikiwa kupiga hatua kubwa katika kudhibiti vitendo vya rushwa ikiwemo kumfikisha mahakamani Afisa Tabibu aliyeomba na kupokea rushwa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 15, 2020 na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,Donasian Kessy

Amesema, hatua hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa majukumu yake ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kulingana na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 na imefanikiwa kutekeleza mpango kazi wake kupitia madawati yake yote ikiwa ni pamoja na Uchunguzi, Uzuiaji Rushwa na Elimu kwa Umma.
UCHUNGUZI NA MASHITAKA

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,Donasian Kessy amesema, katika kipindi hicho, TAKUKURU Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam imepokea taarifa 218 zinazohusu vitendo vya rushwa. 

Amesema, katika kipindi hicho Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni pamoja na taasisi binafsi zinaongoza kwa kulalamikiwa. Kwa mujibu wa taarifa hizo majalada mapya ya uchunguzi yaliyofunguliwa na kufika hatua ya uchunguzi wa kina ni majalada sita na majalada mengine yanaendelea na uchunguzi katika hatua mbalimbali. 

"Katika kipindi hicho Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Temeke imeokoa fedha kiasi cha shilingi 184,235,654.00 fedha hizo zimeokolewa kutoka katika chunguzi mbalimbali kama vile fedha za Saccos na fedha za mtu binafsi,"amesema Mkuu huyo.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,Donasian Kessy amesema, TAKUKURU Mkoa wa Temeke kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2020 imefanikiwa kufungua kesi mpya nne.

"Kesi ya kwanza ilifunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni tarehe 30/09/2020 kesi namba CC/56/2020 inamuhusu Silas Gerold Komba ambaye ni Afisa Tabibu wa Hospitali ya Vijibweni kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007. 

"Silas aliomba rushwa ya shilingi 300,000 ili aweze kumsaidia mwananchi mmoja ambaye ni mjamzito (jina limehifadhiwa) kujifungua vizuri kwa njia ya upasuaji wakati wake wa kujifungua utakapofikia,"amefafanua Mkuu huyo wa TAKUKURU. 

Pia amesema, kesi ya pili ilifunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke tarehe 11/09/2020 kesi namba CC/260/2020 inamhusu Jovinus Julius Lukonje Daktari wa Mifugo Bandari ya Dar es salaam ambaye alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15(1) (a) na (2) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007. 

Mkuu huyo amesema, Jovinus aliomba shilingi 400,000 kutoka kwa mwananchi mmoja ili amsaidie kupitisha mzigo bandarini kwa gharama pungufu ya inayostahili. 

Aidha, kesi ya tatu ilifunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke tarehe 15/09/2020 kesi namba CC/266/2020 na inamhusu Kennedy Jackson Kasera Katibu wa Maji Mtaa wa Uwazi ambaye alifikishwa mahakamani kwa kosa la kutoa hongo kinyume na kifungu cha 15(1) b na (2) cha sheria Na 11 ya mwaka 2007. 

"Kennedy alichukua fedha shilingi 1,000,000 kutoka katika akaunti yake na kumpatia mwananchi mmoja (jina limeifadhiwa) ili aweze kumnyamazisha asitoe taarifa kuwa fedha za Kamati ya Maji ziliingizwa katika akunti yake binafsi badala ya kuingizwa katika akaunti ya Mtaa wa Uwazi,"ameongeza Mkuu huyo.

Kesi ya nne, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,Donasian Kessy amesema ilifunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Temeke tarehe 15/09/2020 kesi namba CC/266/2020 na inamhusu, Bw. Elias Kassim Mtalawanje aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kijichi na mwenzake Constatine Mourice Onyando ambaye ni Mwenyekiti wa tawi la CCM Mgeninani. 

Amesema, kwa pamoja walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15(1) (a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007. 

Mkuu huyo amebainisha kuwa, Bw. Elias aliomba shilingi 1,000,000 ili asiweze kuzuia malipo ya mtu aliyetakiwa kulipwa fidia ya kiwanja na Bwana Constantine alishiriki katika kupokea fedha hizo.

UELIMISHAJI UMMA

"TAKUKURU iliendelea na jukumu la kuelimisha umma kupitia njia mbalimbali, lengo likiwa ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya rushwa. 

"Uelimishaji ulifanywa kwa kuendesha semina 18 kwa makundi mbalimbali na mikutano ya hadhara 27 kwa wananchi. Pia, tumetoa vipindi cha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa katika redio na television sita, ambapo mkazo mkubwa uliwekwa kwenye elimu dhidi ya rushwa kwenye uchaguzi na kudhibiti rushwa ya ngono. 

"Pamoja na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari mbili, kufungua klabu za wapinga rushwa nne, maonesho mawili, kuimarisha klabu za wapinga rushwa sabini na sita na uandishi wa makala mbili,"amefafanua Mkuu huyo.

UZUIAJI RUSHWA 

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,Donasian Kessy amesema, katika kipindi hicho Dawati la Kuzuia Rushwa limefanya chambuzi za mfumo minne kwa lengo la kubainisha mianya ya rushwa na kisha kudhibiti mianya hiyo kwa kutoa ushauri na mapendezo kwa mamlaka zinazohusika. 

"Chambuzi hizo zilihusisha uchambuzi wa mfumo kuhusu uendeshwaji wa huduma za miradi ya maji Manispaa ya Temeke, uchambuzi wa mfumo katika utekelezaji wa ruzuku ya TASAF kwa kaya maskini,uchambuzi wa mfumo kuhusu mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato kwenye masoko ya Manispaa ya Temeke pamoja na uchambuzi wa mfumo wa mianya ya rushwa katika kutatua migogoro ya ardhi katika mabaraza ya ardhi ya Kata na Wilaya ya Temeke,"amesema. 

MIKAKATI YA OKTOBO HADI DISEMBA 2020

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,Donasian Kessy amesema, Takukuru Mkoa wa Temeke imeweka mikakati ya kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2020 ya kudhibiti vitendo vya rushwa katika mkoa huo, ikiwa ni pamoja kuangalia njia bora ya kuweza kutokomeza vitendo vya rushwa katika miradi mbalimbali iliyopo katika Manispaa ya Temeke.

Amesema, miradi hiyo ni pamoja na miradi ya Elimu, Maji, Ujenzi wa miundombinu, ukusanyaji wa mapato na manunuzi ya umma, maliasili na utalii, madini,viwanda, biashara, (kuimarisha mazingira ya biashara), uwekezaji pamoja na miradi ya kilimo, mifugo na ushirika. 

"Aidha, tunayo mikakati ya kuelekea katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi huu wa Oktoba 2020 kwa kuelimisha wananchi kupitia njia mbalimbali ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara, kutoa semina kwa wagombea na mawakala wa vyama mbalimbali ili kudhibiti vitendo vya rushwa katika kipindi cha uchaguzi.

"TAKUKURU Mkoa wa Temeke inatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia mitandao yote ya simu kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi kwa namba ya bure 113 au kupiga 113 au kufuata maelekezo au fika katika ofisi ya TAKUKURU iliyopo karibu nawe kwani kupambana na rushwa ni jukumu langu mimi na wewe," amesema Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,Donasian Kessy.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news