TAKUKURU yabaini mchezo mchafu mikopo ya halmashauri kwa vikundi

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imebaini mchezo mchafu katika mikopo inayotolewa na halmashauri kwa vikundi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani,Suzana Raymond ameyabainisha hayo leo Oktoba 16,2020 mkoani humo.

"Ndugu waandishi wa habari,nimewaalika kuja hapa ili kupitia kwenu, Watanzania wote wafahamu kazi zilizofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Pwani kwa kipindi cha mwezi Julai mpaka Septemba, 2020. 

"Ikumbukwe kuwa ni utaratibu wetu kufanya hivyo ili umma wa Watanzania wafahamu tunafanya nini na watuelewe kwa kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya rushwa nchini.

"Kwa msingi huo naomba kuainisha kazi zilizofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Pwani kwa kipindi hicho kama ifuatavyo:

UCHUNGUZI NA MASHITAKA

Kwa robo hii ya mwaka ofisi ilipokea malalamiko 318 kati ya hayo malalamiko 157 uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na malalamiko 74 yalionekana kuangukia katika sheria nyinginezo hivyo walalamikaji walishauriwa na kuelekezwa sehemu husika kwa lengo la kutatua kero zao. 
Aidha, jumla ya kesi 34 ziliendelea kuendeshwa katika mahakama mbalimbali za mkoa wa Pwani ambapo kesi 10 zilitolewa hukumu na upande wa Jamhuri ulishinda kesi sita kwa washitakiwa kuamuliwa kufungwa jela au kulipa faini, na kesi nne watuhumiwa hawakukutwa na hatia na hivyo waliachiwa huru.

Katika kushughulikia malalamiko yaliyowasilishwa, ofisi imefanikiwa kuokoa mali mbalimbali zikiwemo fedha, nyumba na viwanja kama ifuatavyo;-

Ofisi ya TAKUKURU Chalinze

Katika robo hii ya mwaka, Ofisi hii imefanikiwa kurejesha kiasi cha Shilingi 6,470,000  kwenye akaunti ya Halmashauri ya Chalinze.

Fedha hizi zinatokana na ukiukwaji wa taratibu za mikopo inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu uliofanywa na kikundi cha MIONO SACCOS cha Kata ya Miono huko Chalinze kilichokuwa kimekopa kiasi cha shilingi 9,100,000 toka Halmashauri ya Chalinze. 

TAKUKURU ilibaini kwamba viongozi wa Kikundi hicho cha Miono Saccos yaani Mwenyekiti na katibu alipokea mkopo huo usio na riba toka Halmashauri ya Chalinze na wao kwenda kukopesha kwa wafanyabiashara pasipo hata kuwajulisha wanakikundi wengine kinyume na masharti ya mkopo huo unaotolewa kwa mujibu wa sheria ya fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kifungu cha 37 (a) (4). 

Pia ofisi ilifanikiwa kurejesha kiasi cha shilingi milioni 1,368,000 kwenye akaunti ya Kijiji cha Msoga Kata ya Msoga.

Fedha hizi zilirejeshwa zinatokana na ubadhirifu wa fedha za mapato yatokanayo na madini ya ujenzi uliofanywa na aliyekuwa Mtendaji wa kijiji hicho cha Msoga. 

Kwani ilibainika kuwa mtendaji huyo wa kijiji alipokea kiasi cha Shilingi 1,368,000 kwa nyakati tofauti kutoka kwa mkusanya ushuru wa kijiji hicho na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi. Baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikubali kukabidhiwa fedha hizo na kuomba kuzirejesha na ndipo alipozirejesha kwenye akaunti ya kijiji cha Msoga. 

Ofisi ya TAKUKURU Kibaha

TAKUKURU mkoa wa Pwani imefanikiwa kurejesha nyumba ya Bi.Mayasa Ally Mmeleke iliyokuwa ikishikiliwa na kutaka kuuzwa na Bw.Godlisten Ndimbo baada ya Bi. Mayasa kushindwa kumalizia deni alilokuwa anadaiwa na Bw. Ndimbo.

Awali ilidaiwa kwamba tarehe 15/09/2019 Bi. Mayasa alikopa Shilingi 3,000,000 kutoka kwa mkopeshaji na kuweka rehani hati ya nyumba yake namba MZR/MKZ/641 iliyopo Kitongoji cha Mkuza Wilaya ya Kibaha kwa makubaliano ya kulipa riba ya shilingi 1,200,000 ambapo mkopaji angerejesha jumla ya shilingi 4,200,000. 

Hata hivyo mpaka kufikia mwezi Novemba, 2019 mkopaji alikuwa amesharejesha kiasi cha shilingi 2,400,000.Aidha, kiasi kilichokuwa kimebaki ndio kilipelekea mkopeshaji kutaka kuuza nyumba ya Bi. Mayasa kitu ambacho ni dhuluma. 

TAKUKURU ilifanya uchunguzi wa kina na kubaini ukiukwaji mkubwa wa sheria uliofanywa na mkopeshaji kwa kufanya biashara ya ukopeshaji wa fedha bila kusajiliwa, kinyume kifungu cha 6(1) cha sheria ya mabenki yaani “Banking and Financial Act” ya mwaka 2006 ambacho kinakataza mtu kufanya shughuli za kibenki au kutoza riba pasipo kuwa na leseni kutoka benki kuu.

Pia mkopeshaji alibainika kukwepa kulipa kodi kutokana na biashara hiyo anayoifanya kinyume cha Sheria.Mtuhumiwa ameelekezwa kuacha biashara hiyo mpaka atakapofuata taratibu za kisheria zinazotakiwa. 

Ofisi ya Kibaha pia imefanikiwa kuwasaidia viwanja watumishi wapatao 12 waliokuwa wanadai mishahara kwa kazi ya ulinzi katika kampuni iitwayo PRC ASSOCIATES SECURITY (T) LTD ya mjini Kibaha. 
 
Kwani watumishi hao walifanya kazi katika kampuni hiyo ya ulinzi kwa takribani miaka mitatu pasipo kulipwa mishahara yao na kufanya jumla ya deni la mishahara wanayodai kufikia Shilingi 23,000,000. 

Mmiliki wa kampuni tajwa alipofuatwa na TAKUKURU alionyesha ushirikiano na kuamua kuwalipa viwanja watumishi wake badala ya fedha chini ya usimamizi wa serikali ya mtaa na watumishi hao kuridhika na hatua hiyo kwani walihangaika sana kutafuta haki yao katika sehemu mbalimbali bila mafanikio yoyote na hatimaye sasa watumishi hao wamelipwa na kupata haki yao. 

Ofisi pia imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni ishirini na tano (25,000,000) kutoka kampuni ya MAFUBILO ikiwa ni sehemu ya deni la wakulima wa korosho wanaounda umoja wa UVUKI wilaya ya Kibaha. 

Ofisi ya TAKUKURU Mafia

TAKUKURU wilaya ya Mafia ilifanikiwa kuokoa shilingi 4,261,675/= ambazo zilikusudiwa kuchepushwa na baadhi ya watumishi na mawakala katika Halmashauri ya wilaya ya Mafia wenye dhamana ya kukusanya ushuru kwa kutumia mashine za kieletroniki “Point Of Sale”. 

Aidha kiasi cha shilingi 4,925,000/= zimerejeshwa katika akaunti ya Chama Cha Ushirika wa Korosho na Nazi wilayani Mafia. Fedha hizo zilikuwa zimechepushwa na viongozi wa chama hicho ambao kwa sasa wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Hata hivyo uchunguzi wa tuhuma dhidi ya viongozi hao bado unaendelea.

Ofisi ya TAKUKURU Kibiti 

OFISI imefanikiwa kuokoa bati zipatazo 168 zenye thamani ya shilingi 4,704,000/= zilizotakiwa kuezekwa kwenye madarasa ya shule shikizi ya msingi ya NYAMBANGALA iliyopo kata ya DIMANI wilaya ya Kibiti.

 Awali ilibainika kwamba mkataba wa ujenzi wa madarasa hayo ulihitaji kuezeka mabati ya “gauge 28” lakini madarasa hayo yaliyojengwa kwa mtindo wa “Force Account” yaliezekwa kwa bati za “gauge 32”, hivyo TAKUKURU iliingilia kati na hivyo kufanyika marekebisho kwa mujibu wa mkataba.

 Hujuma hii ilifanywa kwa njama baina ya Mwalimu Mkuu wa shule aliyekuwa msimamizi mkuu wa ujenzi huo pamoja na mzabuni aliyepewa kazi ya kuwasilisha mabati hayo.

Ofisi imefanikiwa kuokoa na kurejesha fedha taslimu shilingi 64,966,094/ ambazo zimechepushwa na wanunuzi wa korosho (50,000,000/) na nyingine (14,966.094/ ) zilikuwa zimechepushwa na viongozi wa AMCOS.

 Fedha walilipwa wakulima waliokuwa wanadai katika AMCOS za Juhudi, Mwambao na Ruarushe

Ofisi ya TAKUKURU Rufiji

Wakati huo huo, TAKUKURU kupitia ofisi yetu ya wilaya ya Rufiji tuliweza kuokoa kiasi cha shilingi 2,500,000 kutokana na tozo za kodi kutoka kwa mfanyabiashara JAFARI MCHEKWA aliyekiuka taratibu za uvunaji wa mazao ya misitu kwa kuvuna magogo ya mti wa mkuruti katika maeneo yasioruhusiwa.

 Fedha za faini hiyo tayari zimekwishaingizwa katika akaunti ya Mtendaji wa wakala wa misitu Tanzania.

TAKUKURU wilaya ya Rufiji tuliweza kuokoa kiasi cha shilingi 1,264,500/ kilichotokana na ukiukwaji wa taratibu uliofanywa na maafisa wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji kufanya ukadiriaji mdogo wa ujazo wa magogo yaliyokua yanapigwa mnada katika kijiji cha NYAMWAGE, 
 
Kwani ilibainika kuwa ujazo uliowasilishwa na maafisa wa Halmashauri ulikua na meta za ujazo 21 badala ya 25.5 zilizopatikana baada ya TAKUKURU kuingilia kati na kufanya upimaji upya kwa kushirikiana na ofisi ya wakala wa misitu nchini, na hivyo kufanikiwa kupata ongezeko la meta za ujazo 4.5 zilipelekea kijiji kujipatia fedha za ziada shilingi 1,264,500 baada ya mauzo.

Pia, kiasi cha Shilingi 900,000/= kiliokolewa kutokana na malipo hewa ya mauzo ya korosho yaliyolipwa kwa mfanyabiashara ABDALLAH GOCHI kinyume na taratibu kwani hakustahili kupata malipo hayo, hivyo TAKUKURU iliingilia kati na kuamuru mfanyabiashara huyo kurejesha fedha hizo ili mhusika aliyestahili malipo hayo aweze kupata haki yake.

Katika kipindi hicho hicho TAKUKURU Wilaya ya Rufiji ilifanikiwa kurejesha shilingi 1,200,000 ambazo maafisa ardhi wilaya ya Rufiji ambao ni MASHAKA ABDALAH na OMARY MAZORA walijipatia kwa njia zisizo halali kwa kuuza viwanja vya halmashauri bila mwajiri wao yaani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kujua.

Pia tuliweza kukamilisha urejeshwaji wa fedha kiasi cha shilingi 12,000,000/- kwa mwalimu mstaafu YUSUPH RASHID KIMWERI ambazo alikuwa amemlipa Bw. IBRAHIM MAREMA MASWE kupitia akaunti yake. Fedha hizi zinatokana na mkopo umiza uliokopeshwa kwake wa Tshs. 700,000/- na hivyo kutakiwa kurejesha Tshs. 13,000,000/- zikiwa ni fedha alizokopeshwa Tshs. 700,000/- pamoja na riba ya mkopo huo.

Ofisi ya TAKUKURU Kisarawe

Kupitia Ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Kisarawe tuliweza kumsaidia mwananchi mnyonge Bi. KHADIJA BANI mkazi wa mtaa wa Bomani wilayani Kisarawe kulipwa kiasi cha shilingi 12,500,000.

Fedha hizi ni sehemu ya Shilingi 26,000,000/= alizotakiwa kulipwa kama fidia ya mazao katika shamba lake lililochukuliwa na kampuni ya RAK KAOLIN Co. LTD mwaka 2016. 
 
Shamba hilo lilichukuliwa kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya Kaolin lakini haikumlipa fidia mama huyo aliyetwaliwa shamba lake mpaka TAKUKURU ilipoingilia kati ndipo wakamlipa kiasi hicho na kuahidi kumalizia kiasi kilichobaki ndani ya mwezi huu Oktoba, 2020.

 Kwani sheria za uchimbaji madini zinamtaka mwekezaji kulipa fidia za wote walioathirika na mradi huo kabla shughuli ya uchimbaji haijaanza, kitu ambacho kampuni tajwa ilikiuka.

Ofisi ya TAKUKURU Mkuranga

Kupitia Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mkuranga tuliweza kuwarejeshea wakulima wa chama cha Msingi cha KIMANZICHANA KUSINI kiasi cha Shilingi 34,081,840/= ambazo walikuwa wamedhulumiwa na Viongozi wa Bodi ya AMCOS na kampuni ya COFEE TRADERS.

Aidha shilingi 7,753,000/=ziliokolewa kutoka kwa viongozi wa Bodi wa vyama vya msingi vya KISEGESE, KILIMAHEWA KASKAZINI na MUUNGANO ambazo zilikuwa mali ya wakulima. Fedha hizo zilitokana na mauzo ya korosho msimu wa 2018/2019. Utaratibu wa kuwarejeshea wakulima husika unaendelea.

TAKUKURU wilaya ya Mkuranga pia ilifanikiwa kurejesha kwenye akaunti ya Halmashauri kiasi cha Shilingi 930,000/= kutoka kwa Bw. SHABAN MPONDA, Afisa Mtendaji wa Kata ya Vikindu.

 Fedha hizo alizikusanya kutoka kwa watendaji wa vijiji kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Kata lakini mtendaji huyo alizifanyia ubadhirifu.

Aidha tuliweza kufanikisha kufufuliwa kwa mradi wa maji wa Shule ya Sekondari PANZUO mradi ambao ulikufa tangu mwaka 2017 baada ya Mkandarasi SEBA CONSTRUCTION & DRILLING CO.LTD kutumia “solar panel” na “pump” ambazo hazikuwa na ubora.

 Hivyo TAKUKURU ilianzisha uchunguzi kujua kwanini mkandarasi hakufuata matakwa ya mkataba uliomhitaji kuweka vifaa vyenye ubora kitu kilichopelekea mradi kushindwa kutoa maji kama ilivokusudiwa, 
 
Lakini baada ya TAKUKURU kuingilia kati tulimtaka mkandarasi kufanya marekebisho yaliyotakiwa kwa kuzingatia mkataba wa kazi aliopewa na serikali, hivyo basi, mkandarasi alifanya marekebisho na sasa mradi unafanya kazi na maji yanatoka katika shule hiyo ambapo Shilingi 32,296,600/= zilitumiwa na mkandarasi ili kufanya marekebisho hayo.

Kwa hiyo mkoa wa pwani kwa robo hii tumefanikiwa kuokoa mali na fedha taslimu zenye dhamani ya shilingi 243,120,709/= ( milioni miambili arobaini na tatu mia moja na ishirini elfu, mia saba na tisa).

ELIMU KWA UMMA.

Ndugu waandishi wa habari,katika kipindi hicho tumeweza kuelimisha jumla ya wananchi 6,224 kupitia semina 74, mikutano 62, maonesho 2 na vipindi 6 vya redio. Pia kwa kufungua klabu za wapinga rushwa 18 na kuimarisha klabu zipatazo 71

Elimu tuliyotoa ilihusu Madhara ya Rushwa katika chaguzi za kisiasa kwani mnatambua kuwa nchi yetu ipo katika mchakato kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwezi huu kwahiyo wananchi ni lazima wapate elimu ya madhara ya Rushwa katika uchaguzi na kuwajengea uwezo wa kuchagua viongozi waadilifu watakaosaidia nchi katika kuleta maendeleo ya kweli. 

Pia elimu ya Rushwa ya Ngono ilitolewa kupitia kampeni yetu ya VUNJA UKIMYA KATAA RUSHWA YA NGONO yenye lengo la kuondoa kero ya rushwa hii kwa jamii hasa katika vyuo vya elimu ya juu na mashuleni ambako waadhirika wakubwa wa rushwa hii ni ndugu zetu akina dada. Aidha tulitoa elimu juu ya “Wajibu na ulinzi wa mwananchi katika mapambano dhidi ya Rushwa”,

UZUIAJI RUSHWA 

Katika eneo la Uzuiaji Rushwa tulifanya uchambuzi wa mifumo 12 katika maeneo Mbalimbali ambayo ni; Ukusanyaji wa mapato yatokanayo na huduma (Service Levy), pia tulichambua mfumo wa upatikanaji wa leseni za biashara zitolewazo na Halmashauri za wilaya ili kubaini mianya ya rushwa na kutafuta mbinu za kuziba mianya hiyo.

Baadhi ya mianya iliyobainika katika uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato ni pamoja na wafanyabiashara wengi kutokuwa na elimu ya huduma ya “service levy” kama ilivyo kwa ada, ushuru na kodi nyinginezo. 
 
Na katika uchambuzi wa mfumo wa upatikanaji wa leseni za biashara tulibaini kuwa wafanyabiashara wengi wanafanya biashara zao pasipo kuhuisha leseni zao za biashara na kuipotezea mapato serikali na pia kuna wafanyabiashara wanaopewa notisi za kulipia leseni zao lakini hawafanyi hivyo na kuendelea na biashara.

Na katika kufuatilia wafanyabiashara wasiolipa service levy, kuna mfanyabiashara mmoja alikaidi kulipa kwa muda mrefu lakini baada ya TAKUKURU kufuatilia alikimbia na kwenda kulipa mara moja kiasi cha shilingi 18,218,420.37 na hivyo kuiingizia fedha Halmashauri ya mji wa Kibaha. Hayo ni baadhi ya matunda ya chambuzi za mifumo tunazofanya katika utendaji wetu

UFUATILIAJI WA MIRADI

Ndugu waandishi wa habari,

Mtakumbuka kuwa ni jukumu la TAKUKURU kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo katika nchi yetu inakuwa na tija na kuleta matunda yaliyokusudiwa. Katika robo hii ya mwaka tumekagua jumla ya miradi ya maendeleo 16 katika sekta za elimu, afya, na ujenzi.
 
Miradi hiyo ina thamani ya shilingi Bilioni tatu, milioni mia tisa therathini na tano, laki nane tisini na moja elfu mia tatu na arobaini na senti hamsini na tano (Shilingi 3,935,891,340.55). 
 
Aidha, katika ufuatiliaji wa miradi hiyo baadhi ya miradi ilibainika kuwa na udhaifu katika usimamizi wa sheria, kukosekana kwa elimu kwa walipa ushuru, udanganyifu katika utoaji wa taarifa za mapato katika biashara, wafanyabiashara wengi kutolipa ushuru wa huduma (Service Levy),
 
Na katika baadhi ya miradi ilibainika kuwa na mapungufu yaliyotokana na manunuzi ya vifaa vingi kuliko uhalisia na kukiuka taratibu za manunuzi hivyo uchunguzi umeanzishwa kwa lengo la kupata hasara iliyotokana na manunuzi hayo, na watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria. 

MIKAKATI YETU KWA KIPINDI CHA OKTOBA HADI DISEMBA 2020

Kama ilivyo dira ya Taifa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwaka huu, mikakati ya mkoa wa Pwani ni kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika pasipokuhusisha vitendo vya Rushwa kwa kufanya yafuatayo;

Kufikisha elimu ya madhara ya Rushwa kwa wananchi wote mpaka ngazi ya kijiji ili waone umuhimu wa kuchagua viongozi waadilifu watakaokuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wakati wa uchaguzi. 
 
Na kuwajengea uwezo wananchi kutambua viongozi sahihi wenye nia ya dhati ya kumkomboa mtanzania, viongozi watakaokuwa mstari mbele kuunga mkono mapambano dhidi ya Rushwa na ufisadi.

Kufanya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazotufikia, zikiwemo tuhuma za rushwa katika Uchaguzi kwa lengo la kupata ushahidi.

WITO WA TAKUKURU KWA WANANCHI

Ndugu waandishi na wananchi,

"Naomba kutumia fursa hii kuwasihi wananchi wa mkoa wa Pwani na watanzania kwa ujumla kutumia haki yenu ya kupiga kura hapo tarehe 28/10/2020 kwa kuchagua viongozi wasiojihusisha na vitendo vya Rushwa. 
 
Aidha mwananchi unaweza kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa TAKUKURU kupitia namba za BURE 113 AU kwa ujumbe mfupi wa simu kwa kupiga *113# kisha fuata maelekezo,"Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani,Suzana Raymond amefafanua kwa kina leo Oktoba 16,2020 mkoani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news