Utekelezaji wa miradi ya Serikali kupitia Rais Shein wazidi kubadili taswira ya Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali imejenga jengo la biashara la “Michenzani Mall” ili wananchi waingie katika utaratibu wa kuuza biashara kwa njia za kisasa zaidi, anaripoti Mwandishi Diramakini (Zanzibar).

Dkt.Shein ameyasema hayo leo Oktoba 5,2020 katika ufunguzi wa jengo jipya la biashara la Michenzani Mall liliopo Michezani jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi,Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Bashiru Ali Kakurwa na viongozi wengine wa ndani na nje ya Zanzibar pamoja na wananchi.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Shein amesema kuwa, majengo ya biashara kama hayo hayajengwi kwa ajili ya shughuli za kuuza na kununua vitu peke yake bali yanajumuisha huduma mbalimbali za kijamii zinazohusiana na elimu, afya, urembo, manukato, burudani na kadhalika.

Rais Dkt.Shein ameongeza kuwa, ndani ya jengo hilo kuna maduka, sehemu za mazoezi ya viungo, sinema, sehemu za kucheza kwa watoto na shughuli kadhaa za kijamii ukiwemo ukumbi wa harusi na chumba maalum kwa kumpambia mabibi harusi, migahawa, sehemu za vyakula na vinywaji, saluni za nywele na sehemu nyinginezo.

Ameongeza kuwa, eneo hilo kabla palijaa makontena ya biashara ambayo hayakuwa na mpangilio maalum ndipo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba ilipofikiria kuwawekea wananchi wake mazingira bora ya ya kuvutia ya kufanya biashara.

Rais Dkt.Shein amesema kuwa, sekta ya biashara ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi na sekta hiyo ina uwiano mkubwa na sekta ya usafiri na usafirishaji ambayo huunganisha watu kutoka vijijini na mijini, kanda za Kitaifa na Kimataifa.

Kutokana na hilo, ndio maana Serikali yake anayoiongoza ya Awamu ya Saba iliivalia njuga kazi ya uimarishaji wa sekta hio ya ujenzi kwa kuongeza ujenzi wa barabara mpya na kuzifanyia matengenezo zile ambazo zilikuwepo.

Akieleza historia ya biashara hapa Zanzibar, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, katika kujitafutia maisha kabla ya Mapinduzi wananchi wa Zanzibar hawakuwa na fursa za kumiliki biashara kubwa kwa sababu biashara za aina hiyo zilihodhiwa na mabepari.

“Majengo kama haya ya biashara tunayakuta katika nchi za wenzetu na yameanza zamani tangu 1922 kule Marekani katika jiji la Kansas na likiitwa “Country Plaza,”amesema Dkt.Shein.

Aidha, Rais Dkt.Shein amesisitiza kwamba kwa wale wote waliokuwa wakifanya biashara katika eneo hilo kabla ya kujengwa jengo hilo jipya watapewa kipaumbe katika maombi ya kuomba kufanya biashara katika eneo hilo kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Rais Dkt.Shein pia, ametumia fursa hiyo kwa kutoa wito kwa vijana kuitumia fursa hiyo kwa kujipanga, kutafuta utaalamu wa kuandaa miradi yenye tija na kuitumia fursa ya uwepo wa “Mall” hiyo kwani tayari Serikali imeshawaandalia mazingira mazuri ya kuwepo kwa mfuko wa uwezeshaji utakaowakopesha fedha ili wafanye biashara waitakayo.

Hivyo, Rais Dkt.Shein amerejea usemi wake wa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuwataka baadhi ya vijana ambao kwao wao kazi ni za kuajiriwa serikalini tu kuachana na mawazo hayo na badala yake wajitume na Serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Rais Dkt.Shein amesema kuwa, katika kipindi hiki cha wiki mbili zilizopita amekuwa akifungua miradi mikubwa mbalimbali hapa Zanzibar ambapo matukio yote hayo yana maana kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na nchi kwa jumla ambapo pia, ni kielelezo halisi cha Mapinduzi Matukufu ya Januri 12, 1964.

Rais Dkt.Shein pia ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutekeleza mradi unaojulikana kwa jina la “BIG-Z” (Boosting Inclusive Growth for Zanzibar-Integrated Development Project), ambao Serikali kupitia Wizara ya Fedha itashirikiana na Benki ya Dunia kuufanikisha katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Ameongeza kuwa, mradi huo utakuwa wa miaka mitano hadi saba na lengo lake kuu ni kuimarisha mazingira ya maeneo hayo na kushajiisha ushirikishaji wa kijamii na kiuchumi ambapo miongoni mwa shughuli hizo ni uhuishaji wa eneo la mji wa Zanzibar (Michenzani Green Corridor).

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Shein ameipongeza Kampuni ya CRJE kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa kazi nzuri walioifanya ambayo imeonekana pamoja na kumshukuru na kumpongeza Mshauri Muelekezi wa ujenzi huo

Kampuni ya “Arques Africa ya Dar es Salaam kwa kuusimamia vizuri ujenzi huo huku akiupongeza uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na ZSSF kwa hatua hiyo nzuri ya maendeleo iliyofikiwa.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa ameeleza kuwa, mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 katika ukurasa wa 203 ilipoeleza hatua za kuimarisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), ili uendelee kuekeza katika miradi mbali mbali ya kiuchumi inayozalisha faida kubwa na kukuza mapato ya mfuko huo.

Ameeleza kuwa, kati ya miradi hiyo ni ujenzi wa “Michenzani Mall”, ambapo alisema kuwa katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Dkt.Shein (ZSSF) imewekeza miradi 12 mikubwa pamoja na miradi mingine midogo midogo ambayo yote hiyo imegharimu sh.Bilioni 140 huku akisema kuwa maendeleo yote hayo yamefanywa chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Khamis Mussa alisema kuwa, baada ya kukamilika kwa

michoro Aprili 30, 2018 ilitolewa zabuni kumtafuta mkandarasi ambapo jumla ya wazabuni 28 walijitokeza na baada ya tathmini Kampuni ya CRJE kutoka China ilishinda zabuni hiyo na kupelekea kutiwa saini mkataba wa ujenzi baina ya ZSSF na CRJE Oktoba 4, 2018 kwa gharama ya sh. Bilioni 27.9.

Amesema kuwa, ujenzi ulianza rasmi Novemba 23, 2018 na ulitarajiwa kuchukua muda wa miezi 21 hadi kufikia 30 Juni 2020 hata hivyo kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kuibuka kwa maradhi ya COVID-19 mradi uliongeza muda.

Amesema kuwa, kama zilivyo “Malls”, nyingine duniani “Michenzani Mall” inatoa fursa kwa kufanyika biashara ya kisasa ya rejareja na huduma nyingine zinazoendana na mahitaji ya mtu kutumia muda mwingi katika jengo hilo ambalo lina ghorofa kati ya tano na saba kwa kuzingatia ghorofa ya chini ya ardhi na sehemu mbili za pembeni mwa jengo.

Katibu Mkuu huyo amesema kuwa, ZSSF iliamua kuwa kazi ya ukodishaji wa sehemu za jengo hilo ifanywe na Kampuni yenye uzoefu hivyo ilitangaza zabuni na kufanikiwa kuipata Kampuni ya Knight Frank (T) LtD ambayo pia ina uzoefu wa shughuli hizo kwa soko la Zanzibar.

Pamoja na kutumia kampuni ya ukodishaji, wafanyabiashara wanaotarajia kupata nafasi katika jengo hilo ni mchanganyiko wa wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wageni na wazawa ambapo pia, Katibu Mkuu huyo alirejea ahadi ya Rais Dkt.Shein ya wafanyabiashara wa makontena waliokuwepo awali katika eneo hilo wapewe kipaumbele.

Sambamba na hayo, wafanyabiashara wapya ambao tayari wamejitokeza kukodi sehemu katika Mall hiyo ni pamoja na Kampuni ya GSM inayoendesha maduka maarufu ya Max, Baby Zone, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Benki ya Afrika, Horizon Pharmacy na Shamshu Phamacy, huku ZSSF ikiendelea na uchambuzi wa maombi mengine.

Amengeza kuwa, ZSSF inadhamiria kutekeleza nia yake ya kujenga jengo la kisasa la maegesho ya gari litakalokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wanaokuja kuuza au kununua katika jengo hilo ambapo jengo hilo linatarajiwa kuwa la ghorofa tatu ambazo zote zitatumika kwa ajili ya maegesho na litakuwa na uwezo wa kuchukua gari 150 kwa wakati mmoja.

Mapema Rais Dkt.Shein mara baada ya kulifungua na kukata utepe wa jengo hilo alipata fursa ya kulitembelea akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa Kitaifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news