Waziri Jafo atoa tuzo 485 kwa walimu, wanafunzi, shule, halmashauri na mikoa

Serikali imetoa wito kwa wamiliki wa shule binafsi kuwa wazalendo katika kutoa elimu kwa kuhakikisha wanatoa elimu bora ili kuzalisha watoto wenye elimu bora itakayo wasaidia katika kulitumikia Taifa,anaripoti Majid Abdulkarim, Dar es Salaam.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Selemani Jafo jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji tuzo za kitaifa za Taaluma ya Elimu kwa walimu, wanafunzi, shule, halmashauri na mikoa iliyofanya vizuri kitaaluma kwa mwaka 2019 ambapo jumla ya tuzo 485 zimetolewa kwa washindi. 

Waziri Jafo amesema kuwa, utoaji wa tuzo unaleta ushindani mkubwa katika shule binafsi na umma hivyo wamiliki wa shule wanatakiwa kutoa elimu bora kwa watoto wa kitanzania na kuacha kutanguliza maslahi yao mbele bali uzalendo ili kupata watoto wenye elimu bora itakayowasaidia katika kulitumikia Taifa na kuleta maendeleo kwa ujumla.

“Utamaduni wa utoaji tuzo utasaidia sana kuwaondoa watu wajanja ambao wanatupeleka pabaya ambapo sio muelekeo wa Taifa letu, mwelekeo wetu ni sisi wenyewe kujenga Taifa letu wenyewe kwa uzalendo mkubwa na wala hakuna mtu atakayekuja kutoka nje kutujengea Taifa letu hata siku moja,"amesema Jafo.
Aidha, Jafo amesema kuwa mwaka 2020 shule 10 bora za kidato cha sita ni shule za nane za umma ambapo shule tatu ni za kata huku shule iliyoongoza kitaifa ni Kisimiri, Mwandeti na Dareda.

“Hii ndiyo kazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyotutuma sisi wasaidizi wake kufanya ya kuzalisha watoto bora kutoka katika shule za binafsi na umma watakaokuwa na moyo wa uzalendo wa kutumikia Taifa,”amesema.

Vile vile, Mhe. Jafo ametoa pongezi kwa watendaji wote wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kazi nzuri iliyofanyika na wanayoendelea kufanya katika kuwatumikia watanzania ili kuwaletea maendeleo.

Naye mmoja wa wanafunzi waliopata tuzo kutoka shule ya Kibaha, Alex Joseph amesema kuwa, kitendo cha TAMISEMI kutoa tuzo hizo kinatoa hamasa kubwa kwa walimu, wazazi, wanafunzi na Viongozi kwenye sekta muhimu ya elimu ambayo ndio chachu ya maendeleo ya nchi.

“Hivyo natoa wito kwa kwa TAMISEMI kuendelea kutoa tuzo hizo kwani zinahamasisha wanafunzi wengi kufanya vizuri na kuendelea kujituma katika masomo,"amesisitiza mwanafunzi Alex Joseph.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news