Waziri Kalemani aagiza umeme usikatwe kipindi cha uchaguzi

Waziri wa Nishati,Dkt.Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na wakandarasi wote nchini kusimamia ipasavyo upatikanaji wa umeme wa uhakika katika kipindi chote cha uchaguzi, anaripoti Hafsa Omar (WN) Dar es Salaam.

Waziri wa Nishati,Dkt.Medard Kalemani (mwenye miwani), Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi. Innocent Luoga (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt.Tito Mwinuka (kushoto) pamoja na wataalamu mbalimbali wakati wakiwa kwenye eneo ambalo nguzo za zege zimehifadhiwa ambazo zitatumika kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha kupooza umeme kinachojengwa Dege katika Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam,Oktoba 17,2020. (WIZARA YA NISHATI).

Ametoa agizo hilo Oktoba 17,2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kufanya ukaguzi wa ujenzi wa kituo cha kupooza umeme kilichopo Dege Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Amesema, Serikali inataka wananchi wafanye uchaguzi wao bila ya kujitokeza kwa changamoto yoyote inayotokana na umeme na kuwataka mameneja wote wa Tanesco kulisimamia agizo hilo ili isitokee changamoto yoyote inayohusiana na umeme katika kipindi cha uchaguzi.

Nguzo za zege ambazo zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa mradi wa kituo cha kupooza umeme kilichopo Dege Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaamu,Oktoba 17,2020. (WIZARA YA NISHATI).

“Nitoe rai kwa mameneja wote wa Tanesco umeme usikatike wakati wa uchaguzi, usikatike kwa maeneo yoyote na muda wowote lakini hasa wakati wa uchanguzi na hasa tarehe 28 wakati wa kupiga kura tunataka wananchi wapige kura bila ya kero yoyote ya umeme,”amesema.

Pia, ameitaka Tanesco kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika unapatikana muda wote nchini ili wananchi watumie huduma hiyo katika kujiletea maendeleo mbalimbali katika maeneo yao.

Waziri wa Nishati,Dkt.Medard Kalemani akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika ujenzi wa kituo cha kupooza umeme kilichopo Dege Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam Oktoba 17,2020. (WIZARA YA NISHATI).

Hata hivyo, amesema matumizi ya nguzo za zege zitasaidia na kupunguza kero ya kukatika kwa umeme nchini kwakuwa nguzo hizo zinauwezo wa kukaa muda mrefu bila ya kuharibika.

“Ili wananchi waendelee kuwa na uhakika wa umeme lazima tutumie nguzo za zege, kwasababu maeneo mengine Dar es Salaam umeme unakatika kwasababu wataalamu wetu wanafanya marekebisho mara kwa mara yakiwemo ya kuondoa na kubadilisha nguzo zilizoharibika kwahiyo tukishaweka nguzo za zege tatizo hili litamalizika,”amesema Dkt.Kalemani.

Aidha, ameeleza kuwa tayari nguzo za zege zimeanza kusimikwa katika maeneo mbalimbali nchini, nguzo ambazo ni imara na zinadumu kwa miaka mingi zaidi bila ya kuharibika na ambazo zitaleta mageuzi makubwa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.

Waziri wa Nishati,Dkt.Medard Kalemani akizungumza na waandishi wa habari mara baada kumaliza kufanya ukaguzi wa kituo cha kupooza umeme kilichopo Dege Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam Oktoba 17,2020. (WIZARA YA NISHATI).

Amesema,maeneo ambayo yamepewa kipaumbele kwa kuanza kutumika kwa nguzo hizo ni pamoja na sehemu ambazo kuna majaruba au maeneo ambayo kuna majimaji ambapo nguzo zinaharibika kwa haraka.

Pia, amewapongeza wakandarasi wote aliopewa kazi ya kutengeneza nguzo hizo, kwa kukamilisha kazi zao kwa haraka na kuwataka kutengeneza nguzo zenye ubora wa hali ya juu.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati aliambatana na Kamishna Msaidizi wa Umeme Mhandisi. Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO), Dkt.Tito Mwinuka,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijiji (REA),Amos Maganga na waatalamu mbalimbali kutoka Tanesco.

No comments

Powered by Blogger.