Waziri Kalemani atoa siku 21 wananchi wote waliolipia umeme nchini waunganishiwe

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa agizo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na wakandarasi wote kuhakikisha kuwa wananchi wote waliolipia huduma ya umeme wanaunganishiwa umeme ndani ya siku 21,anaripoti Hafsa Omar,Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akizungumza wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kuzalisha mita za luku cha Multicable Ltd kilichopo katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam,Oktoba 5,2020.

Ametoa agizo hilo Oktoba 5,2020 wakati akiwa kwenye ufunguzi wa kiwanda cha kuzalisha mita za luku cha Multicable Ltd kilichopo katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Waziri Dkt.Kalemani amesema, wananchi 5,000 nchini wamelipia huduma hiyo na hadi sasa hawajaunganishwa na huduma hiyo ambayo ni muhimu katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kwa nchi kiujumla.

Ameeleza kuwa, uwepo wa viwanda vingi vya ndani ambavyo vinazalisha vifaa vya usambazaji wa umeme unarahisha usambazaji wa umeme nchini na hakuna tena sababu yoyote ambayo itapelekea ucheleweshaji wa uunganishaji umeme kwa wananchi.

“Nimeshaeleza hapo mwanzo kuwa hakuna tena sababu zinazosababisha wananchi wachelewe kupata umeme kwa kisingizio cha uhaba wa mita za luku, kwenye kiwanda hiki ambacho nimekifungua leo kuna takribani mita za luku 500,000 ambazo zipo tu hata hazijanunuliwa,"amesema Dkt. Kalemani.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (mwenye miwani) akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa taasisi za wizara hiyo wakipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Kiwanda cha Multicable Ltd Oktoba 5,2020.

Pia amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA kukamilisha kazi zao ifikapo Oktoba 15,mwaka huu, kwa kuwa vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya usambazaji umeme vinapatikana kwenye viwanda nchini,ambavyo ni vya bei rahisi na vyenye ubora wa viwango vya juu.

“Wakandarasi wote ambao miradi yao imekaribia kukamilika ambao wengi wao wamebakiza vijiji viwili au vitatu, wakamilishe kazi zao kwa haraka na hatutawaongezea muda na ifikapo Oktoba 15,mwaka huu wakabidhi miradi yao,”ameagiza Waziri Dkt.Kalemani.

Amewataka wananchi wote ambao hawajafikiwa na huduma ya umeme kwenye maeneo yao nchini watulie na kuiamini Serikali yao, kwani tayari Serikali imeshatekeleza miradi mingi na mpango wa Serikali ni kuhakikisha umeme unafika kwa wananchi wote ambao hawajafikishiwa umeme ndani ya miaka miwili ijayo.

Ameeleza kuwa, Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana nchini kote na kuwataka wawekezaji nchini kuendelea kufungua viwanda vingi zaidi vya vifaa vya usambazaji wa umeme,ambapo ameeleza kuwa, kufunguliwa kwa viwanda vingi kutawarahisishia wananchi kupata umeme kwa muda mfupi zaidi.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (mwenye miwani) akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa taasisi za wizara hiyo wakipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Kiwanda cha Multicable Ltd Oktoba 5,2020.

Amesema, Serikali itahakikisha inavilinda viwanda vyote vya kuzalisha mita za luku nchini ambavyo mpaka sasa vimefunguliwa viwanda takribani 10 vya uzalishaji huo, ambavyo vinasaidia kutoa ajira nyingi kwa watanzania na Serikali imejipanga kuhakikisha inavilinda viwanda hivyo kwa kuwatafutia soko la kuuzia bidhaa zao.

Pia amewashukuru wawekezaji wa viwanda vya kutengenezea vifaa vya kusambaza umeme nchini,amesema vimesaidia sana kutatua changamoto ya upatikanaji wa vitendea kazi vya usambazaji umeme nchini.

Vilevile, amewahamasisha wawekezaji mbalimbali nchini kuendelea kuwekeza katika viwanda vya kuzalisha mita za kusambazia gesi majumbani.

Ambapo ameeleza kuwa, tayari Serikali imeshaweka zuio kwamba ifikapo Januari,mwakani wakandarasi wote watakaopewa kazi ya usambazaji gesi majumbani hawataruhusiwa kuagiza mita kutoka nje ya nchi ili kulinda soko la ndani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha Multicable Ltd, Murtaza Alibhai amesema kuwa, wameamua kutekeleza sera Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli ya Tanzania ya viwanda kwa vitendo ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi nchini, ambapo amesema kiwanda hicho mpaka sasa kimeajiri zaidi ya wafanyakazi 700.
Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha mita za luku cha Multicable Ltd kilichopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Murtaza Alibhai akizungumza wakati wa ufunguzi wa kiwanda hicho, Oktoba 5,2020.

Amesema, kiwanda chao kitahakikisha kinazalisha bidhaa bora zenye viwango vya hali ya juu ili kuchangia uchumi kupitia sekta ya viwanda nchini.

Aidha, ameeleza kuwa wanatarajia kuanzisha kiwanda cha kutengeneza transfoma hivi karibuni ili kuhakikisha kuwa usambazaji umeme nchini unafanyika kwa haraka na watanzania wote wafurahie kupata huduma ya umeme mapema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news