Zitto amtenga Bernard Membe urais

"Nitampigia Kura Tundu Lissu ili Awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania [Tamko langu kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2020]," anaandika Zitto Kabwe kama alivyonukuliwa na Mwandishi Diramakini.

Ndugu Bernard Membe ambaye alikabidhiwa ilani ya Chama cha ACT Wazalendo kupeperusha bendera ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni, leo Oktoba 16, 2020 azimio la Kiongozi Mkuu wa chama, ndugu Zitto Kabwe limeonyesha wazi kuwa, Membe si chaguo lao tena.

"Wananchi wa Bangwe,

Wananchi wa Kigoma Mjini,

Watanzania Wenzangu,

Nawashukuru sana kwa Dua, Sala na maombi yenu kwangu na wenzangu tulipopata ajali ya Gari huko Kalya, jimbo la Kigoma Kusini, Oktoba 6, 2020. Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi ya kuendelea kuishi. Ilikuwa ajali mbaya sana, Lakini Mungu hakutaka nife. Mola alitaka niishi ili nione Watanzania wakifanya Mabadiliko makubwa ya Uongozi wa Taifa letu.

Mabadiliko ni lazima yatokee kwa sababu Nchi yetu imeumia sana Katika miaka hii mitano iliyopita. Kamwe hatuwezi kuendelea na ukandamizaji wa Haki, Uhuru pamoja na maisha magumu Kiasi hiki. Tunapaswa sote kwa pamoja kusema SASA BASI. Twende tukachague Mabadiliko. Oktoba 28, 2020 iwe ni Siku mpya ya Haki, Uchumi Mpya, na Uhuru kwa Watanzania.

Chama chetu, ACT Wazalendo kiliamua kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi huu wa mwaka 2020 kwa kuweka wagombea kila ngazi, pamoja na kuzalisha Ilani ya Uchaguzi iliyofanyiwa kazi vizuri na kwa umakini mkubwa. Hata hivyo vikao vya Chama kupitia Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu viliazimia kwamba Viongozi wa kitaifa waendelee na juhudi za kuunganisha nguvu ya Vyama vya Upinzani ili kuwa na Ushirikiano dhidi ya Chama tawala.

Kutokana na uwepo wa sheria kandamizi ya Vyama vya Siasa, ushirikiano wa kisheria tumeona hauna maana kwetu kama Chama kwani Msajili wa Vyama hawezi kuidhinisha jambo linalokwenda kuiondoa CCM madarakani.

Kamati ya Uongozi ya Chama chetu imeshauriana na kuona kuwa huu ni mwaka wa kihistoria kwa Watanzania, mwaka wa kuamua hatma ya Maisha yao. Ni mwaka wa Watanzania kuchagua Kiongozi atakayerejesha Furaha katika Maisha yao, atakayeheshimu Katiba ya nchi yao, atakayejali Maendeleo ya Watu badala ya Vitu, atakayeheshimu Wanawake wa Tanzania na atakayerejesha uhuru wa Watu. Sisi ACT Wazalendo hatupo tayari kuwa kizuizi cha safari hii ya Mabadiliko, nami kama Kiongozi wa Chama ninao wajibu wa kulieleza hilo kwa Uwazi kwa niaba ya Viongozi wenzangu wa Kamati ya Uongozi.

Hivyo basi, baada ya maelezo hayo, natangaza rasmi kwa Wanachama, Wafuasi, wapenzi wa ACT Wazalendo na Watanzania kwa Ujumla, kuwa:

1. Pale kwenye Kata ama Jimbo ambalo ACT Wazalendo tuna Mgombea, tunaomba Muwapigie Kura wagombea wa ACT Wazalendo.

2. Pale ambapo kwenye Kata au Jimbo la Uchaguzi hakuna Mgombea wa ACT Wazalendo, lakini kuna wagombea wengine wa Vyama vya Upinzani, ACT Wazalendo tunawaomba MPIGIE KURA MGOMBEA WA CHAMA CHA UPINZANI mwenye nguvu zaidi ili kutokutawanya Kura.

3. Kwa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mimi Zitto Zuberi Ruyagwa Kabwe NITAPIGA KURA YANGU kwa ndugu Tundu Antipas Mughwai LISSU. Huyu ndiye Mgombea wa Upinzani ambaye ana nguvu ya kumshinda Mgombea wa Chama tawala, amefanya kampeni nchi nzima, mwitikio wa Wananchi kwake ni mkubwa sana, ameeleza kwa ufasaha dhamira yake ya kuleta mabadiliko na sina mashaka na dhamira hiyo, pamoja na anayotaka kuyafanya kama Rais, ni mambo hayo ndiyo yaliyonipa msukumo wa kumpigia Kura Lissu. Zaidi NINAMUAMINI LISSU kutokana na historia yake ya kupigania Haki za Watu. Ninaomba kila mpenda Haki na Mabadiliko nchini ampigie kura ya URAIS ndugu Tundu Lissu ili awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Natanguliza Shukran kwenu


Kabwe Z. Ruyagwa Zitto

Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo

Bangwe, Kigoma Mjini

Oktoba 16, 2020

No comments

Powered by Blogger.