Ajira mpya 13,000 za walimu zatolewa vijijini

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema Serikali imewapanga zaidi walimu wa shule ya msingi katika shule za vijijini ambako ndiko kwenye upungufu mkubwa zaidi ya walimu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 27,2020 kuhusu ajira mpya za walimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na mafundi sanifu wa maabara, Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa kwa upande wa shule za msingi upangaji wa walimu umefanyika kwa lengo la kuboresha uwiano wa walimu kwa wanafunzi.
Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa, asilimia 60 ya walimu wote walioajiriwa wamepelekwa katika shule za msingi hasa za vijijini ambako ndipo kwenye uhitaji mkubwa wa walimu nchini.

Ameendelea kufafanua kuwa Serikali imeweka kipaumbele kuajiri walimu kwa ajili ya shule za sekondari zenye mchepuo wa sayansi na hisabati, ufundi, kilimo na maarifa, maarifa ya nyumbani, lugha ya kiingereza, kichina na kifaransa.

Amesema kuwa, walimu wa masomo mengine wamepangwa kulingana na upungufu uliopo ambapo kipaumbele ni shule ambazo hazina walimu wa masomo husika.

Mhandisi Nyamhanga amesema pia wamezingatia shule zenye mahitaji maalum ambako walimu 481 wameajiriwa kwa ajili ya shule hizo na kuwa suala la umri wa ajira za Serikali limezingatiwa kwa walimu waliopata ajira ni wale waliomaliza chuo mwaka 2014 mpaka 2019.

Aidha, Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa waajiriwa wapya wa uwalimu wa shule za msingi na sekondari wanatakiwa kuhakikisha wanaripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya muda wa siku 14, kinyume na hapo watakuwa wamepoteza nafasi zao na zitajazwa kwa waombaji wengine.

“Waajiriwa wapya wanatakiwa kuripoti kazini kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 14 Desemba 2020 watakaoshindwa kuripoti nafasi zao zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa waliopo kwenye kanzidata ya Ofisi ya Rais –TAMISEMI,”amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.

Pia mewaagiza wakurugenzi wa halmashauri ambao walimu hao wamepangiwa kuwapokea na kuwawezesha kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma. 

Hata hivyo, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanatoa taarifa ya kuripoti waajiriwa hao na kuzijaza kwenye mfumo wa kielektroniki baada ya kila mtumishi kupokelewa katika kituo cha kazi.

“Kamilisheni mtaratibu za ajira haraka ili walimu hawa waingizwe katika mfumo wa malipo ya mshahara(payroll) mapema iwezekanavyo,"ameelekeza Mhandisi Nyamhanga.

Septemba 7, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitoa kibali cha ajira mpya za walimu 13,000 wa shule za msingi na sekondari pamoja na mafundi sanifu wa maabara za shule.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news