CRDB yaunga mkono Uchumi wa Buluu, Rais Dkt.Mwinyi aelezea mikakati

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imeamua kufanya Mapinduzi ya kiuchumi kwa kuendeleza Uchumi wa Buluu na kuweka mkazo katika kuziimarisha sekta za huduma, ikiwemo sekta ya utalii, ambayo ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Profgesa Neema Mori alipowasili katika viwanja vya Hoteli ya Verde Marina Mtini jijini Zanzibar kuhudhuria Semina Maalum iliyoandaliwa na Benki kwa Viongozi Waandamizi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyofanyika usiku wa Novemba 28, 2020 katika viwanja vya Marina na kulia kwa Rais Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela.(Picha na Ikulu).

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Jamal Kassim Ali akizungumza wakati wa hafla ya Semina ya Viongozi Waandamizi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyofanyika
katika viwanja vya Marina Hoteli ya Verde Mtoni jijini Zanzibar iliyofanyika usiku wa Novemba 28, 2020,kabla ya kumkaribisha Rais wa Zanzibar kuzungumza kjatika hafla hiyo.(Picha na Ikulu).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo katika hafla iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa viongozi waandamizi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, iliyofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Verde, Mtoni nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.Katika hotuba yake, Rais Dkt.Mwinyi amesema kwamba kutokana na udogo wa ardhi kila uchao zinaendelea kuibuka changamoto katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ambapo ardhi yote ya Unguja ni kilomita za mraba 1,666 na Pemba ni kilomita za mraba 988 ambapo ukubwa huo hauendani na ongezeko la watu.

Sheikh Abdulkadir Said Abdalla akisoma Quran kabla ya kuaza kuaza kwa semina maalum iliyoandaliwa na Benki ya CRDB Tanzania kwa viongozi waandamazi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliofanyika katika viwanja vya Marina Hoteli ya Verde Mtoni jijini Zanzibar usiku wa Novemba 28, 2020.(Picha na Ikulu).

Amesema kuwa, zamani ardhi ilitegemewa kwa kilimo na wananchi wengi waliweza kuendesha maisha yao kwa kutegemea shughuli za kilimo na ufugaji ambapo leo ardhi hiyo hiyo inategemewa sana kwa ujenzi wa makaazi, viwanda na shughuli nyingine za uchumi wa karne hii ya 21.

Kwa kulizingatia tatizo hilo la ardhi, Rais Dkt.Hussein Mwinyi amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane imeamua kutumia rasilimali mbadala ya bahari pamoja na kuimarisha sekta za huduma.

Amesema kuwa, Serikali imelenga kuendesha na kukuza uchumi wa buluu kwa kuzitumia kikamilifu rasimali zinazohusiana na bahari, ikiwemo shughuli zinazohusu sekta ya utalii, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi na bahari kuu, ufugaji na usindikaji wa samaki, ukulima wa mwani, pamoja na mazao mengine anuwai ya bahari.


Rais Dkt.Mwinyi amemuahidi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kumpa timu maalum ya kushirikiana na benki hiyo katika kufanya kazi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imeamua kutoa ushirikiano mzuri kwa sekta binafsi ambapo imekusudia kwa dhati kuwa wadau wezeshi wa sekta binafsi kwa kuwawekea mifumo rafiki na mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi bila kikwazo.

“Nimefurahishwa sana kusikia kwamba Benki ya CRDB imehamasika kutokana na mwelekeo wa maendeleo na dira yangu ya kuijenga Zanzibar mpya na kuamua kutuunga mkono katika jitihada zetu za kufanikisha malengo yetu tuliyoyakusudia, ahsanteni kwa moyo wenu huo wa kizalendo,”amesema Dkt.Hussein Mwinyi.


Aidha, amesema kuwa hamu ya Benki ya CRDB ya kushirikiana na Serikali hasa katika masuala ya uchumi wa Buluu imemtia moyo na ana imani kubwa kwamba ushirikiano huo utaongeza kasi ya uzalishaji na sekta zinazotegemea mazao ya baharini kama vile viwanda na usindikizaji vitaibuka na kuimarika.

Rais Dkt.Hussein ameendelea kusisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo la kimkakati la uwekezaji ambapo pia, Serikali imejipanga kuendeleza utalii, kukuza biashara na viwanda na kushajiisha uwekezaji katika maeneo mapya ya uchumi.

Katika hotuba yake hiyo aliitaka benki hiyo kuwa na ujasiri wa kuwapatia mikopo wananchi wanaojishughulisha katika sekta ya kilimo, uvuvi wa kawaida, ujasiriamali na ufugaji, wauzaji wa biashara ndogo ndogo na za kati wanahitaji kuwezeshwa zaidi ili biashara zao ziwaletee kipato chenye tija itakayoweza kuwakwamua na umasikini.


Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameihakikishia Benki hiyo ya CRDB kwamba Serikali iko tayari kushirikiana na benki hiyo na ushirikiano huo utaweza kuleta uchumi mpya hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba hiyo ni azma ya Serikali ya Awamu ya Nane.

Kwa lengo la kupanua wigo wa ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya CRDB, Rais Dkt. Hussein alipendekeza kwamba CRDB iangalie zaidi suala la uwekezaji katika miradi mikubwa ya maendeleo hapa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dkt.Hussein amewataka wafanyabiashara na wananchi wote wenye fedha nje ya nchi kuzileta fedha hizo nyumbani ili waweze kuijenga nchi yao na kuwaahidi kwamba hawatahojiwa wala kubughudhiwa kwa aina yoyote. “Tunataka kuijenga nchi yetu na nchi hujengwa na wananchi wenyewe".

Ameeleza haja kwa Benki ya CRDB kufikiria kufungua tawi jingine katika mji wa Wete kwani huduma inazotoa benki hiyo katika tawi lake ililolifungua Chake Chake mwezi Julai, 2017, zimewavutia wateja wengi kwa hivyo huu ni wakati muwafaka wa kufikiria suala hilo bila ya kuchelewa.


Ameongeza kuwa, wananchi wengi wanaamini kwamba benki kazi yake ni kuweka fedha za matajiri tu, kumbe kuna fursa nyingi muhimu zinazowafanya wale wasiokuwa na pesa waweze kuzipata na kuzitumia kila siku katika kuwaendeshea maisha yao, kwa mnasaba huo ipi haja kwa Benki ya CRDB kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma hiyo.

Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid kwa niaba ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi aliahidi kutoa ushirikiano mkubwa na benki hiyo na kueleza imani yake kubwa kwamba mafanikio makubwa yatapatikana.

Waziri wa Fedha na Mipango, Jamali Kassim Ali nae kwa upande wake amesema kuwa, wananchi walio wengi hasa wa ngazi ya chini wanahitajia huduma za benki hiyo, hivyo ni vyema wakachukua juhudi za makusudi kuwafikia.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela akiwasilisha mada juu ya shughuli za benki hiyo na jinsi ilivyojipanga katika kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane na kueleza kwamba benki hiyo iko tayari na kumuomba Rais aipe timu kwa ajili ya kufanya kazi ili kuleta maendeleo ya kasi na chanya.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Tanzania,Abdulmajid Mussa Nsekela akiwasilisha mada ya maendeleo ya Benki ya CRDB kwa washiriki wa hafla hiyo viongozi waandamizi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyofanyika katika viwanja vya Marina Hoteli ya Verde Mtoni jijini Zanzibar usiku wa Novemba 28,2020.(Picha na Ikulu).

Amesema kwamba, Benki ya CRDB imedhamiria kufanya kazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ikidhamiria kuunga mkono katika kujenga uchumi imara wenye kutegemea rasilimali za bahari yaani “Uchumi wa buluu”.

"Tunafahamu Serikali ya Awamu ya Nane imejipanga kuleta Mapinduzi katika sekta zote za maendeleo na sisi tumeweka mkakati wa ushiriki wetu kuanzia sekta ya utalii, kilimo, uvuvi, ujenzi, viwanda, miundombinu, elimu na afya,"amesema Nsekela huku akibainisha kuwa uwezeshaji huo unafanyika kuanzia kwa wajasiriamali wadogo, wakati na kwa makampuni makubwa.

Amesisitiza kwamba Benki ya CRDB imejidhatiti vya kutosha katika kutoa mikopo ya maendeleo usahili wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Tabianchi (GCF) ulioipata Benki hiyo mwishoni mwa mwaka jana umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwezo wa benki hiyo kutoa mikopo ambapo sasa hivi inaweza kutoa hadi dola za kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.


“Hizi ni fedha nyingi sana ambazo tumedhamiria kuzielekeza katika miradi ya maendeleo nchini kwa kushirikiana na Serikali na sekta binafsi,”ameongezea Nsekela.

Nsekela amesema, Benki ya CRDB inaendelea na zoezi la uunganishwaji wa mfumo wa kidijitali wa malipo katika taasisi za Serikali na binafsi ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. “.. tunafanya hivi tukiwa na uzoefu wa kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukusanya mapato katika sekta ya utalii ambapo zilikukusanywa fedha zinazofikia dola za kimarekani milioni 12 mwaka 2019 kutoka dola laki 4 mwaka 2014,”amesema Nsekela.

Mkurugenzi huyo ameeleza azma ya benki yake kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Awamu ya Nane ili kuifanya Zanzibar kuwa Dubai ya kesho sambamba na kuonesha utayari wake kwa kusaidiana na Serikali kutafuta wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar.

Benki ya CRDB ina matawi mawili Zanzibar ambapo moja lipo Unguja na jingine Pemba ambapo benki hiyo pia, imefanikiwa kupanua wigo wake wa huduma kupitia CRDB, wakala zaidi ya 160 ambao wanasadia kutoa huduma kwa Wazanzibari zaidi ya 300,000 na tayari mikopo ya benki hiyo hapa Zanzibar imefikia shilingi bilioni 101 ambazo zimekopeshwa katika maeneo mbalimbali huku wadau wake kwa asilimia 80 ni Watanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news