KATIBU MKUU MADINI ATOA MIEZI MIWILI MGODI WA STAMIGOLD KUANZISHA MIGODI MIPYA

Wizara ya Madini imetoa kipindi cha miezi miwili kwa Mgodi wa Stamigold kuwasilisha mpango wa kuanzisha migodi mipya, anaripoti Issa Mtuwa (WM) Kagera.

Kauli hiyo kwa Stamigold ambayo ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inafuatia kuonyesha uwezo wa kuanzisha na kuendesha migodi mipya.

Hayo yamesemwa Novemba 22, 2020 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila alipotembelea mgodi huo wa Stamigold unaomilikiwa na Serikali kupitia STAMICO kwa lengo la kuona maendeleo ya uendeshaji wa shuguli za mgodi huo.

“Leo ninatoa agizo ndani ya miezi miwili kuanzia Desemba na Januari 2021 mwisho ninataka nipatiwe taarifa hiyo inayoonesha mpango wa kuanzisha migodi mipya,”amesisitiza Prof.Msanjila.

Baada ya kufika mgodini hapo, Meneja Mkuu wa STAMIGOLD Mhandisi Kilasha Shamika alitoa taarifa ya uendeshaji wa mgodi pamoja na changamoto zake zinazojitokeza wakati wa uendeshaji wa mgodi.

Mhandisi Shamika amemueleza Katibu Mkuu kuwa uendeshaji wa shuguli za mgodi zinaendelea vizuri na hadi hivi sasa mgodi unajiendesha kwa fedha zake.

Ameongeza kuwa, kutokana na uzalishaji wanaoufanya, hawapati faida kubwa lakini kiasi hicho kinawapa nafasi ya kupunguza madeni ya zamani ambapo mgodi tayari umeshalipa shilingi bilioni 10 kati ya jumla ya shilingi bilioni 39 wanazodaiwa.

“Kutokana na uendeshaji wa mgodi, mgodi kwa sasa hauzalishi madeni mapya. Mgodi unatekeleza maagizo mbalimbali yaliyotolewa na viongozi katika utoaji wa motisha kwa wafanyakazi,”amesema Mhandisi Shamika.

Ameongeza kuwa, katika kutekeleza kwa maagizo hayo, mgodi umeanza kutoa mikataba ya miaka miwili miwili ambayo inawapa utulivu kazini. Pamoja na hilo, wafanyakazi wametafutiwa fursa ya kupata mkopo kutoka kwenye benki mbalimbali na uanzishwaji wa chama cha wafanyakazi.

Akizungumzia kuhusu changamoto Mhandisi Shamika amesema, suala la ukosefu wa umeme ni tatizo na kueleza kwamba gharama za mafuta zimekuwa kubwa ambapo kila mwezi hutumika sh.bilioni 1.2, wakati endapo wengetumia umeme gharama yake ingekuwa Shilingi milioni 300 kwa mwezi na hivyo kuokoa kati ya shilingi milioni 700 au 800 kwa mwezi.

Amesema, changamoto nyingine ni mtaji kwa ajili ya kuanzia miradi mingene kama mradi wa Visusi.
Katika hatua nyingine, Prof. Msanjila alitoa pongezi kwa STAMIGOLD kwa kazi nzuri wanayoifanya mgodini hapo.

Aliongeza kwa kuanza kuendesha mgodi kwa gharama zao, kutengeneza faida japo ni kidogo, kulipa madeni ya zamani, kutoendelea kuzalisha madeni mapya na kutengeneza mazingira ya utulivu kwa wafanyakazi.

“Nimefurahi sana kwa haya yote mliyoyasema kwenye taarifa yenu. Nimefurahi ingawa mna changamoto kadhaa,” amesema Prof.Msanjila.

Akizungumzia changamoto zilizosemwa Prof. Msanjila amekiri suala gharama za mafuta ni tatizo na kuahidi kulifuatilia suala hilo kwenye mamlaka zinazotakiwa kuleta umeme mgodini. Kuhusu mtaji amesema, mgodi una 'asset' ambayo ni pamoja na lesseni za uchimbaji ambayo ni sehemu ya mtaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news