Majaliwa, Ndugai, Mo Dewji kunogesha hafla ya wabunge wapya Tawi la Simba Bungeni

Mwenyekiti wa tawi la Simba Bungeni maarufu Simba Mjengoni,Rashid Shangazi amesema kuwa tawi hilo limeandaa hafla ya chakula cha usiku kesho kwa ajili ya kuwakaribisha wabunge wapya mashabiki wa Simba,anaripoti Alex Sonna,(Fullshangwe) Dodoma.
 
Shangazi amesema kuwa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni miongoni mwa wageni wa heshima watakaohudhuria hafla ya kuwakaribisha wabunge wapya ambayo imeandaliwa na wabunge wanachama wa Klabu ya Simba tawi la Bunge jijini Dodoma.

Hafla hiyo pia itahudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na Naibu Spika, Dkt.Tulia Ackson ambao ni wanachama wa Simba pamoja na mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo, Mohammed Dewji (Mo Dewji).

Mwenyekiti wa tawi la Simba Bungeni maarufu Simba Mjengoni, Rashid Shangazi, akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa kuelekea katika hafla ya kuwakaribisha wabunge wapya mashabiki wa Simba itakayofanyika kesho jijini Dodoma.

Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 17, 2020 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo Shangazi amesema kuwa, lengo la hafla hiyo itakayofanyika kesho jijini Dodoma ni kula chakula cha usiku pamoja, kufahamiana pamoja na wabunge wapya kupata fursa ya kujisajili kwenye tawi hilo na kujisajili na kadi ya uanachama ya timu hiyo.

Shangazi amesema, lengo la kuanzishwa kwa tawi hilo ni kuuza bidhaa za klabu hiyo na kuwa wakala wa bidhaa na vifaa vya Simba pamoja na kupata sehemu mahususi ya wabunge kutazama mpira.

Mwenyekiti wa tawi la Simba Bungeni maarufu Simba Mjengoni, Rashid Shangazi,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuelekea katika hafla ya kuwakaribisha wabunge wapya mashabiki wa Simba hafla hiyo itakayofanyika kesho jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Bi.Barbara Gonzalez,akielezea jinsi walivyojipanga kesho katika hafla ya kuwakaribisha wanachama wapya ambao ni wabunge mashabiki wa timu hiyo.
Meneja wa Benki ya Equity, Upendo Makula,akitoa wito kwa wabunge wapya mashabiki wa Simba pamoja na wanachama kujitokeza kwa wingi kujisajili kabla ya hafla ya chakula cha pamoja.

”Alichokisema Mwenyekiti Mo Dewji kuwa watanzania wengi ni Simba wala hakukosea, mfano hapa Bungeni wabunge wa zamani na wa sasa ambao wamejisajili Simba ni 280 unaweza ukaona namna gani tulivyo wengi,"amesema.

"Simba ni muongoza mwendo tutaeleza mipango kabambe tuliyonayo, lengo letu ni kulifanya tawi letu kuwa kubwa zaidi duniani, ni Bunge la Tanzania tu ambapo klabu ya mpira ina tawi ndani yake na klabu hiyo ni Simba pekee, wengine wakianzisha basi wamechukua kwetu,”amesema Shangazi.


Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakifuatilia mkutano huo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Simba, Bi.Barbara Gonzalez amesema kuwa timu hiyo imejikita kuongeza ushindani wa kimchezo barani Afrika na Duniani.

Naye Meneja wa Benki ya Equity, Upendo Makula amesisitizia wabunge na wanachama ambao sio wanachama ni mashabiki tu waje Equity Bank wajisajili na waweze kupata kadi zao za uanachama. Aidha, amesema kuwa Dodoma wanaendelea vizuri na tayari wameshatoa kadi 1,000 hadi sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news