Miaka mitano ya kuwekeza kwa faida zaidi yaanza

Baada ya miaka mitano ya mafanikio makubwa katika sekta ya viwanda nchini, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya miaka mitano ijayo kuanzia sasa inatarajia kufanya makubwa zaidi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameyasema hayo leo Novemba 13, 2020 wakati akifungua Bunge la 12 na kulihutubia Taifa bungeni jijini Dodoma.

Dkt. Magufuli amesema, ni ndoto kufikiria kwamba utaweza kukuza uchumi au kupambana na umasikini pamoja na tatizo la ukosefu wa ajira bila kuelekeza nguvu katika kukuza sekta ya viwanda.

Amesema, Duniani kote, sekta ya viwanda ndiyo mhimili mkuu wa kukuza uchumi, kupambana na umasikini pamoja na matatizo ya ajira.

"Kwenye miaka mitano iliyopita, tulifanikiwa kujenga viwanda vipya takriban 8,477 ambavyo vilitengeneza ajira zipatazo 480,000, ambapo Mkoa wa Pwani uliongoza kwa kujenga viwanda vingi.

Hivyo basi, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendeleza jitihada za kukuza sekta hiyo. Mkazo mkubwa tutauweka kwenye viwanda vyenye kutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini (mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi); vyenye kuajiri watu wengi; na ambavyo bidhaa zake zinatumika kwa wingi hapa nchini (nguo, bidhaa za ngozi, mafuta ya kula, sukari, saruji, n.k.).

Ili kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, tutaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kuangalia masuala ya kodi na kuondoa vikwazo na urasimu. Pamekuwepo na urasimu mwingi na kusumbuliwa kwa wawekezaji kwa kuzungushwa zungushwa na hivyo kuwafanya wakate tamaa.

Mimi nataka mwekezaji mwenye fedha akija apate kibali ndani ya siku 14. Kwa sababu hiyo, nimeamua suala la uwekezaji ikiwa ni pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kulihamisha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais ili hao wanaokwamisha nikapambane nao mwenyewe.

Lakini, zaidi ya hapo, tumepanga kujenga Ukanda na Kongani (clusters) za viwanda kila mkoa kulingana na mazao na maliasili zinazopatikana,"amefafanua Rais Dkt. Magufuli.

Post a Comment

0 Comments