Rais Dkt. Mwinyi atangaza Baraza Jipya la Mawaziri

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi leo Novemba 19, 2020 ametangaza Baraza la Mawaziri ambalo limefanyiwa maboresho huku nafasi za manaibu waziri na uteuzi wa mawaziri wizara mbili akiziweka kiporo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Pia amesema msimamo wake bado uko pale pale wa kuendeleza maridhiano na kuendeleza umoja miongoni mwa Wazanzibari kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akitangaza majina ya mawaziri katika wizara mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya Nane katika ukumbi wa mikutano Ikulu jijini Zanzibar leo wakati alipozungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Serikali na binafsi. 

Baraza hilo ambalo limekuja na sura mpya za mawaziri, Rais Dkt.Mwinyi amesema baada ya uteuzi huo, wateule wote wataapishwa kesho kutwa jijini Zanzibar.

Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar wakati akitangaza baraza hilo mbele ya vyombo mbalimbali vya habari kutoka ndani na nje ya Zanzibar wakiwemo viongozi mbalimbali wa Serikali.

“Ofisi ya Rais, badala ya kuwa na mawaziri watatu kama mwanzo, sasa ofisi ya Rais itakuwa na mawaziri wanne. Kama nilivyosema katika hotuba yangu ya kufungua Baraza la Wawakilishi, nilieleza umuhimu wa sekta binafsi, kwa hiyo Waziri wa kwanza atakuwa akishughulikia Uchumi na Uwekezaji, atashughulikia sekta binafsi, uwekezaji na diaspora,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria katika hafla ya kutangazwa majina ya mawaziri katika wizara mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Rais wa Zanzibar ya Awamu ya Nane na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi katika ukumbi wa mikutano Ikulu jijini Zanzibar leo Novemba 19, 2020 wakati alipozungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Serikali na binafsi. 

Rais Dkt.Mwinyi amewatangaza mawaziri hao wateule kuwa ni kutoka Wizara ya Ofisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji ambapo alimteua Mudrik Ramadhan Soranga, Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Rais amemteua, Masoud Ali Mohamed kuwa Waziri. 

Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Rais Dkt. Mwinyi amemteua Haroun Ali Suleiman kuwa waziri ambayo ilitokana na kuziunganisha zilizokuwa Wizara ya Katiba na Sheria na Utumishi na Utawala Bora huku Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Waziri ni Jamal Kassim Ali.

Pia Rais Mwinyi ametangaza kuwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi amemteua Khalid Salum Mohammed kuwa waziri huku Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo ni Dkt.Soud Nahoda Hassan kuwa waziri.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Rais Dkt.Mwinyi amemteua Simai Mohamed Said kuwa waziri huku Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akimteua Tabia Mwita Maulid kuwa waziri. Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Serikali na binafsi wakiwa katika ukumbi wa mikutano Ikulu jijini Zanzibar wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akitangaza majina ya mawaziri katika wizara mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya Nane leo Novemba 19, 2020.

Pia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rais Dkt. Mwinyi amemteua Riziki Pembe Juma kuwa waziri huku Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale akimteua Lela Mohamed Mussa kuwa waziri.

Rais Dkt. Mwinyi amesema, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi alimteua Rahma Kassim Ali kuwa waziri na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi amemteua Abdalla Hussein Kombo kuwa waziri ambapo Wizara ya Maji na Nishati alimteua Suleiman Masoud Makame kuwa waziri.

Katika baraza hilo ambalo linaundwa na wizara 15, wizara mbili ameziacha wazi akisubiri iwapo Chama cha ACT Wazalendo ambacho kimekidhi takwa la kisheria kitaridhia kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Niliahidi maridhiano, kwenye kampeni nilisema tunataka Wazanzibar tuwe pamoja na kutekeleza Katiba, ACT Wazalendo walipata zaidi ya asilimia 10, tukafuata matakwa ya Kikatiba kwamba watupe jina la Makamu wa Kwanza wa Rais, kwakuwa jina halijafika nafasi tumeiacha wazi.

“Kuhusu kutokuwa na mpinzani katika Baraza la Mawaziri, upande wa Baraza la Mawaziri nimeacha baadhi ya nafasi wazi, Wawakilishi wa ACT hawajaenda kuapishwa, kwa hiyo lazima tuwape muda wao Kikatiba, tumewaandikia pia kuwaomba wakaapishwe. 

“Nimetangaza Mawaziri pekee leo, Manaibu Waziri nitawaweka wakihitajika, nakusudia kupunguza idadi ya watu serikalini, penye mahitaji tutaweka, wizara kubwa sana na yenye kazi nyingi sana tutawaweka ila sehemu nyingi hatutaweka ili kupunguza idadi. Viongozi wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama Zanzibar ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria katika hafla ya kutangazwa majina ya mawaziri katika wizara mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi katika ukumbi wa mikutano Ikulu jijini Zanzibar leo Novemba 19, 2020 wakati alipozungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya Serikali na binafsi. 

“Kuhusu idadi ndogo ya wanawake kwenye baraza, mimi ni muumini wa kutoa nafasi kwa wanawake ila unapofanya uteuzi unaangala sifa sio jinsia, bado tupo kwenye uuandaji wa Serikali kukiwa na nafasi na wapo wanaostahili tutawapa, ila lini tutafika 50 kwa 50 sio rahisi kusema.

“Moja ya kazi nitakazowatuma Mawaziri ni kuhakikisha wanakusanya kodi kwa wingi, mengi nitawaambia siku ya kuwaapisha, kuhusu michezo nipo tayari kukaa na wadau wa michezo tuangalie kila ambalo ni la kujenga kwenye michezo tulifanye kazi ili kuiinua,"amefafanua kwa kina Rais Dkt. Mwinyi wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.

Hata hivyo, Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa,maboresho ya baadhi ya wizara yanalenga kuzipa uzito sekta husika ikiwemo ya uvuvi na utalii ili ziweze kuleta tija kubwa zaidi katika kuwezesha kuharakisha maendeleo nchini.

Wizara ambazo zimeachwa kiporo ni ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na ile ya Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii,Jinsia na Watoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news