Rais Dkt. Mwinyi atangaza neema Sekta ya Michezo Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itawekeza kwenye michezo katika kuibua, kulea na kuendeleza vipaji vya vijana, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ameyasema hayo leo Novemba 11, 2020 katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la Kumi la Wawakilishi hafla iliyofanyika huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Rais Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa, katika hatua hiyo ya kuwekeza kwenye michezo itakwenda sambamba na kukaa na wadau wa soka kutafuta jawabu la kuamsha msisimko wa ligi ya Zanzibar.

“Wakati nakua timu za Zanzibar za Small Simba, Malindi, Mlandege na KMKM zilikuwa ni timu zenye sifa na kuchachafya timu za Bara na zile za Afrika Mashariki,” amesema Dkt. Hussein Mwinyi.

Rais Dkt. Hussein ameongeza kuwa, azma ya Serikali ni kuona Timu ya Taifa ya Zanzibar inakwenda mbali katika kushiriki michuano ya Afrika ili kutumia vizuri fursa ya uanachama katika Shirikisho la Michezo la Afrika (CAF) ambayo imeipigania kwa miaka mingi.

Aidha, Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameeleza kwamba, eneo jingine ambalo litafanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Nane ni kushughulikia Sanaa, burudani pamoja na michezo kwani mambo hayo matatu yana nafasi ya kipekee katika kuwaunganisha Wazanzibari, kuwatambulisha Wazanzibari duniani na kukuza uchumi na ajira.

Ameongeza kuwa, Muziki wa Taarab, muziki wa kizazi kipya na Sanaa ya filamu kupitia matamasha ya ZIFF na ‘Sauti ya Busara’ yameitangaza sana Zanzibar na kuwa na mchango wa kipekee hivyo, ameahidi kuyalea na kuyakuza matamasha hayo na mengine ili kutangaza hazina ya utamaduni na ustaarabu wa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii, kipato pamoja na ajira.

Kutokana na ligi ya Zanzibar kuwa na changamoto ya ufadhili, Rais Dkt. Hussein Mwinyi amewahakikishia wanamichezo kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha ligi ya Zanzibar inapata ufadhili wa uhakika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news