Rais Magufuli awatangazia neema wafugaji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa mifugo barani Afrika na anakusudia kuifanya sekta hiyo kuwa na tija zaidi kwa Watanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo Novemba 13, 2020 wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kulihutubia Taifa ambapo amehaidi kuendelea kuimarisha Sekta ya Mifugo nchini ili iweze kuwa na tija zaidi.

"Kama mnavyofahamu, nchi yetu inashika nafasi ya pili kwa mifugo barani Afrika. Tuna ng'ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.3, kondoo milioni 5.65, punda 657,389. Lakini pia tuna idadi kubwa ya kuku, bata, kanga, n.k. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, sekta hii bado haijatunufaisha vya kutosha.

"Kwa kuzingatia hilo, kwenye miaka mitano ijayo, tunakusudia kuikuza sekta ya mifugo ili ichangie ukuaji uchumi na kupunguza matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira nchini. Tutaongeza maeneo ya ufugaji kutoka hekta 2,788,901 za sasa hadi hekta 6,000,000. Tunataka wafugaji wasiteswe na mifugo yao. Mifugo ni utajiri," amesema Rais Dkt. Magufuli.

Sambamba na hayo, Dkt. Magufuli amesema Serikali yake itahamasisha ufugaji wa kisasa, "tutaongeza vituo vya kuzalisha mbegu bora na pia kuongeza uzalishaji wa chakula cha mifugo viwandani kutoka tani 900,000 hadi milioni 8.

"Zaidi ya hapo, tutakamilisha ujenzi wa machinjio saba unaoendelea maeneo mbalimbali nchini, ambapo, kwa pamoja, zitakuwa na uwezo wa kuchinja ngombe 6700 na mbuzi 11,000 kwa siku.

Ujenzi wa machinjio hizo sio tu utasaidia kupatikana kwa nyama bora itakayouzwa hadi kwenye masoko ya kimataifa bali pia utawezesha upatikanaji wa ngozi bora kwa ajili ya kutengeneza bidhaa za ngozi,"amefafanua Rais Dkt. Magufuli.

Amesema, takwimu zinaonesha kuwa, takriban asilimia 90 ya ngozi inayozalishwa nchini kwa sasa haina ubora unaohitajika na sababu mojawapo ni uchinjaji wanyama kienyeji. 

"Kwa hiyo, machinjio yanayojengwa yatapunguza tatizo hilo. Nitumie fursa hii, kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza bidhaa za mifugo (nyama, ngozi, maziwa, kwato, n.k.).

"Na katika hilo, tunaahidi kutoa vivutio maalum kwa watakaowekeza kwenye viwanda hivyo ambavyo vitasaidia kuinua vipato vya wafugaji wetu na pia kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania. Na hapa, nataka niweke bayana kuwa, watendaji watakaokwamisha ujenzi wa viwanda hivyo tutawashughulikia,"amesema Rais Magufuli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news