'Rais' wa Tanga jela miaka 30 kwa madawa ya kulevya

Mahakama ya Uhujumu Uchumi, imemuhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 mfanyabiashara maarufu jijini Tanga, Yanga Omari (Rais wa Tanga) baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kusafirisha na kuuza madawa ya kulevya aina ya Heroin kiasi cha gramu 1,052.63, anaripoti Mwandishi Diramakini.  
 
Pia Mahakama hiyo imewaachia huru mkewe Rahma Ali na mfanyakazi wa ndani Halima Anuwar baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha kuhusika na biashara hiyo.
Akitoa hukumu hiyo Jaji Imaculata Banzi wa Mahakama hiyo, amesema ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na kumhukumu kifungo hicho.

Jaji Banzi amesema, gari aina ya Land-Cruser V8 na silaha yake vilivyokuwa vikishikiliwa na serikali virejeshwe kwa familia yake ikiwemo madawa aliyokamatwa nayo yateketezwe mara moja.

Yanga Omari anadaiwa kwamba, Agosti 2018 na wenzake hao wawili walikamatwa mtaa wa Bombo jijini Tanga wakitaka kusafirisha dawa hizo za kulevya.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, Wakili wa upande wa mshitakiwa Mohamed Kajembe, aliiomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake, kwa sababu ni kosa lake la kwanza, ana umri mkubwa zaidi ya miaka 50, anategemewa na familia kubwa ikiwemo kuwa na tatizo la shinikizo la damu.

Baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, Wakili Kajembe alieleza nia ya kukata rufaa baada ya kupata nakala ya hukumu pamoja na maelezo ya mwenendo wa kesi hiyo.Shauri hilo limeendeshwa na Mawakili wa Serikali Faraja Nchimbi, Pius Hilla, Salim Msemo, Constantine Kakula na Donata Kazungu.

Awali katika kuthibitisha shitaka hilo upande wa Jamhuri uliwaita mashahidi saba na kutoa vielelezo nane ambapo upande wa utetezi Mshtakiwa alijitetea mwenyewe na hakuwa na kielelezo chochote.

Mshtakiwa Yanga Omary Yanga alikamatwa Oktoba 1,2018 na Maafisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya baada ya kupekua nyumba yake iliyopo Mkoa wa Tanga eneo la Bombo na baada ya kukutwa na dawa hizo mshtakiwa alishtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya chini ya kifungu cha 15 (1)cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news