Spika Ndugai:Wote ni wabunge halali

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai amewaapisha wabunge wawili walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini

Wabunge walioapishwa leo Novemba 30, 2020 ni Mheshimiwa Humphrey Polepole na Riziki Said Lulida, zoezi ambalo limefanyika katika viwanja vya Bunge.

Baada ya kuwaapisha wabunge hao wawili, Ndugai amesema wabunge 19 Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao pia wamevuliwa uanachama na chama hicho ni wabunge halali na kwamba yanayoendelea ndani ya chama hicho, hayo ni ya kwao wao CHADEMA.
Wabunge wa Kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, Mhe. Riziki Lulida na Mhe. Humphrey Polepole wakiwa katika picha ya pamoja na Spika wa Bunge Mhe.Job Ndugai na Katibu wa Bunge Ndg. Stephen Kagaigai mara ya kuapishwa kwenye viwanja vya Bunge hii leo Jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Bunge).

Wabunge hao ni Halima Mdee,Asia Mohamed, Felista Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Simon, Anatropia Theonest,Salome Makamba, Conchester Lwamraza, Grace Tendega, Ester Matiko,Secilia Pareso,Ester Bulaya, Agnes Kaiza, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga na Tunza Malapo 

"Wabunge wote walioaapishwa ni wabunge halali wakiwemo wa CHADEMA, nashangaa wamewafukuza hao wabunge 19, hayo yanayoendelea ni ya kwao. Tutawapanga wabunge wote kwenye kamati kulingana na sekta zao zinapoangukia,"amesema Spika Ndugai, huku akiwataka waandishi wa habari kuwa na weledi kuhusu shughuli za Bunge na kuepuka kuwa sehemu ya upotoshaji. 

Polepole na Lulinda wameapishwaa baada ya kuteuliwa na Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kupitia nafasi 10 ambazo Katiba imempa nguvu ya kufanya hivyo. 
Mbunge wqa Kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, Mhe. Riziki Lulida akila kiapo mbele ya Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai katika viwanja vya Bunge hii leo Jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Bunge)

"Kwa hiyo wale waliokuwa na wasiwasi sijui kuna nini na nini, wala nawaambia wasiwe na wasiwasi wale ni wabunge kamili.Ninawaomba Watanzania wote tupige vita ukandamizaji dhidi ya wanawake kwa kisingizio chochote,"amesema Spika Ndugai huku akionyesha kushangazwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Freeman Mbowe akisema amepigwa chini na ni mzoefu wa kuanguka.

"Kwa mtu mzima na mwanaume wa Kitanzania ni aibu kubwa kutukana wanawake. Nimuonye (Mbowe) wanawake ni mama zetu na ni dada zetu, hata pale wanapokuwa wamekosea sio kuwafukuza kama vibaka," alisema Spika Ndugai na kuongeza. Lakini yupo mwanamke alikuwa anagombea kule Morogoro amesimama na kuwaita wenzake ni COVID 19, unaona kuwa safari ya wanawake ni ndefu. Hamjui hao wanawake 19 wamepita mapito gani, vipo vyama ni kampuni za watu, yaani wanawaburuza kama wanavyotaka,"amefafanua Spika Ndugai.

Spika Ndugai amesema kuwa, "hao ni wabunge, hawawezi wao na genge lao la wanaume wakafanya hivyo dada zetu, lazima ubaguzi wa kijinsia upigwe vita na kila Mtanzania. Mbowe umesahau, Halima Mdee alivyovunjika mkono kwa ajili ya kumfuata gerezani. Esther Bulaya alipigwa hadi akazimia akalazwa hospitali kwa ajili yake, Ester  Matiko amelala gerezani kwa ajili ya kumpigani, lakini mshahara wao ni kuwafukuza bila kuwasikiliza.
Mbunge wa Kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, Mhe. Humphrey Polepole akila kiapo mbele ya Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai katika viwanja vya Bunge hii leo jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Bunge).

"Haiwezekani, analalamika mwanachama wao Nusrat ambaye alikuwa mahabusu. Analalamika kwa nini ametoka mahabusu,awe ametoka usiku au muda gani ili mradi ametoke wewe unachotakiwa ni kushukuru Mungu, ndiyo maana tunasema baadhi ya hivi vyama ni shida."

Katika hatua nyingi Spika Ndugai amekemea vikali watu wanaobeza sehemu zinapofanyikia shughuli za Bunge, huku akifafanua kuwa zinaweza kufanyika sehemu yoyote eneo la Bunge ambalo Spika wa Bunge ataona linafaa.

"Wapo rafiki zetu ambao hivi karibuni wamejipambanua kukejeli shughuli za Bunge. Ni watahadharishe kuwa sio sawa kwa mtu yeyote kukejeli shughuli za Bunge hata wabunge waliokwishakuapishwa.

No comments

Powered by Blogger.