Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yawapongeza Majaliwa, Ndugai na Tulia

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imempongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Mbunge wa Ruangwa kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kulia) akiteta jambo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai (kushoto). Katikati ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson. (Picha na Maktaba/Diramakini).

Pongezi hizo zimetolewa leo Novemba 17, 2020 na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Mathew Pauwa Mhina Mwaimu.

Amesema, tume inamtambua Mheshimiwa Majaliwa kama mdau na mshiriki mkubwa wa tume katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na jamii inayoheshimu uhifadhi na ulinzi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

"Tume inamtakia Mheshimiwa Majaliwa kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo,"amesema Jaji mstaafu Mwaimu kupitia taarifa hiyo.

Wakati huo huo tume hiyo imempongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa kuteuliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Tulia Ackson ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini kwa kuteuliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Tume ikiwa ni taasisi ambayo hufanya kazi kwa kushirikiana na Bunge ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na jamii inayoheshimu uhifadhi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, inawakaribisha na inawatakia kila la heri katika majukumu yao hayo mapya,"amesema Jaji mstaafu Mwaimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news