Wanafunzi 23,621 kufanya Mitihani ya Kidato cha Nne Zanzibar leo

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said amesema Mitihani ya Kidato cha Nnne inatarajiwa kuanza leo Novemba 23, 2020 ambapo jumla ya wanafunzi 23,621 wanatarajiwa kufanya mitihani hiyo kwa Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Akitoa taarifa ya mitihani kwa waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mazizini mjini Unguja, Waziri Simai amesema miongoni mwa watahaniwa hao 14,061 sawa na asilimia 59.3 ni wanawake na watahaniwa 9,605, sawa na asilimia 40.7 ni wanaume.

Waziri amesema kuwa,katika mitihani hiyo kuna jumla ya vituo 232 vya kufanyia mtihani wa Elimu Lazima kidato cha nne kati ya hivyo vituo 172 sawa na asilimia 74.1 ni vya Skuli za Serikali na vituo 60 sawa na asilimia 25.9 ni vya Skuli binafsi.

Aidha, Waziri amewataka wanafunzi kuachana na vitendo vinavyoashiria udanganyifu wakati wote wa mitihani yao kwani vinaweza kusababisha kuwaharibia matokeo yao.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhandisi Idrissa Muslim Hija amesema ili watahaniwa wote wapate matokeo ya daraja la awali ipo haja ya kuwa watulivu na kufuata maelekezo kwa makini ili kufikia malengo yao.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mwalimu Mohammed Salim Nassor amesema, maandalizi ya mitihani kwa upande wa Pemba yamekamilika na kuiomba jamii kuwapa ushirikiano wa hali ya juu watahaniwa ili waweze kufikia malengo yao na kuiletea sifa Taifa ya ufaulishaji wa daraja la juu.

Nae Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bi. Asya Iddi Issa amesema wizara kwa kushirikiana na Maafisa Elimu wa Mikoa yote Zanzibar imejipanga vyema ili kuhakikisha mazingira, miundombinu na vifaa vyote vya Skuli mbalimbali vinakuwa katika mazingira mazuri na salama ili kuwawezesha wanafunzi wanafanya mitihani yao kwa utulivu.

Wakati huo huo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohamed Said amefanya ziara ya kutembelea mazingira ya jengo la wizara hiyo na kuwataka wakurugenzi wote wa Wizara ya Elimu kuhakikisha wizara inakua katika mazingira safi na salama pamoja na kutekeleza kwa vitendo maagizo yote yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Simai ameahidi kuwa karibu na watendaji wote wa wizara yake kuanzia viongozi, maafisa, walimu na wanafunzi ili kuhakikisha Sekta ya Elimu inaendelea kupiga hatua nchini.

Post a Comment

0 Comments