Waziri Mkuu amaliza mgogoro wa ardhi Kilosa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ardhi katika shamba la Chanzuru lenye ukubwa wa ekari 1,598 lililopo wilayani Kilosa, Morogoro kati ya Laizer Maumbi na Ameir Nahad kwa kuagiza likabidhiwe kwa Laizer ili aweze kuliendeleza kwa kulima mkonge,anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao kati yake na Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na Ardhi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Katibu Tawala na watendaji wa Mkoa huo, Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Ardhi wa wilaya hiyo na Laizer Maumbi kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma leo Novemba 30, 2020. Kikao hicho kimemaliza mgogoro wa ardhi wa shamba la Chanzulu wilayani Kilosa kati ya Laizer na Ameir Nahad ambapo imeamriwa kwamba shamba hilo lenye ukumbwa wa ekari 1,598 apewe Laizer ambaye atawekeza katika kilimo cha mkonge.(Picha na OWM).

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameagiza eneo wanaloishi wananchi ndani ya shamba hilo kikiwemo kitongoji cha viwanja 60 na Chekeleni lihakikiwe na kupimwa ukubwa wake na kisha mkulima huyo akafidiwe eneo jingine na wananchi hao wasibugudhiwe.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Novemba 30, 2020 katika kikao chake na Makatibu Wakuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Viongozi wa mkoa wa Morogoro, wilaya ya Kilosa pamoja na Laizer. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma.

“Viongozi wa Serikali simamieni na mratibu vizuri ili wananchi wanaoishi katika vitongoji vilivyomo ndani ya shamba hilo wasibugudhiwe waachwe waendelee kuishi na eneo lililobaki lisilokuwa na mgogoro apewe Laizer. Sehemu hiyo iliyopungua Laizer atafutiwe shamba jingine ili kufidia,"amesema Waziri Mkuu.

Amesema, awali shamba hilo lilikuwa linamilikiwa na Sadruddin Rajabali ambaye alimuuzia Laizer ambaye aliamua kuachana na shughuli za ufugaji na kuanza kulima mkonge, na alipokuwa katika harakati za kubadilisha umiliki shamba hilo liliuzwa kwa mtu mwingine.

Waziri Mkuu amewataka watumishi wa sekta ya ardhi wilayani Kilosa wahakikishe suala hilo wanalisimamia vizuri ili haki itendeke kwa mkulima huyo kukabidhiwa shamba lake na watumishi waliohusika katika mgogoro huo wachukuliwe hatua.

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa mkoa wa Morogoro uhakikishe inabainisha maeneo makubwa yote ambayo hayajaendelezwa na kutoa mapendekezo Serikalini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Loatha Sanare ametumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Mkuu kwa kumaliza mgogoro huo na kuahidi kwamba atasimamia utekelezaji wa maagizo na maelekezo yaliyotolewa.

Naye, Laizer ameishukuru Serikali kwa hatua iliyofikiwa ya yeye kukabidhiwa shamba hilo ambalo ndilo tegemeo lake kwa sasa, kwani aliuza mifugo yake yote na kununua shamba hilo ambalo amepanda mkonge.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news