ACT-Wazalendo yaridhia kushiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar

Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo imeridhia chama hicho kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) na imeagiza chama hicho kuwaruhusu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wabunge na madiwani waliochaguliwa kukiwakilisha chama katika vyombo vya uwakilishi kuanza kutimiza majukumu yao, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Aliyekuwa mgombea Urais Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Maalim Seif Sharrif Hamad.
 
Katibu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu ameyasema hayo leo Desemba 6, 2020 jijini Dar es Saklaam wakati akitangaza maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokaa jana kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa Taifa na chama chao nchini.

Shaibu amesema kuwa,baada ya Kamati Kuu kupokea maoni kutoka kwa wananchi, imejiridhisha kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa kwa moyo safi itakuwa ni kwa maslahi ya Zanzibar, Wazanzibari na Taifa kwa ujumla, katika kuhakikisha vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu na uvurugaji wa uchaguzi vinadhibitiwa kama ilivyokuwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010.

Amesema kamati hiyo imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia maoni ya wanachama na viongozi wa chama chao na kuangalia tathmini ya historia ya mapambano ya demokrasia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.


Amesema, chama kimechukua uamuzi wa kuwaruhusu wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wabunge, na madiwani waliochaguliwa kwenda kukiwakilisha chama hicho.

Shaibu amesema,kwa kuzingatia Ibara ya 9(3) ya Katiba ya Zanzibar, kamati hiyo imeridhia chama kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na imeielekeza Kamati ya Uongozi kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

"Mchakato wa kupendekeza jina la Makamu wa Rais wa Kwanza kwa mujibu wa katiba ya Chama chetu ibara ya 79A kifungu cha 2b kinasema kwamba upendekezaji wa jina la mwanachama wa kushika nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais ni madaraka ya uongozi wa chama.

"Kamati Kuu imeielekeza Kamati ya Uongozi kukaa na kujadili kisha itoke na jina moja la kupendekeza jina la mwanachama ambaye anapendekezwa kushika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais hadi sasa tayari Kamati ya Uongozi imeketi na mapendekezo hayo yamekwisha kuwasilishwa,"amesema.

Pia amesema, Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa maslahi ya wananchi inapaswa pamoja na mambo mengine kuhakikisha uchunguzi wa matukio yote yaliyotokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi ya uvunjaji wa haki za binaadamu, unafanyika na kuwafariji waathirika wote pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kupanga na kutekeleza matukio hayo na kufanyika kwa mabadiliko ya mfumo wa Uchaguzi Zanzibar.


Shaibu amesema kuwa, hatua hiyo inalenga kurejesha imani ya wananchi juu ya uwepo wa uchaguzi huru na wa haki pamoja na kufanyika marekebisho ya uendeshaji wa vyombo vya Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili vifanye kazi kwa weledi

"Kamati kuu imezingatia hali ilivyo Zanzibar hivi sasa ambapo siasa za chuki na uhasama zimerudi upya kutokana na makovu yanayotokana na uchaguzi wa Mwaka 2020. Zanzibar inahitaji busara kubwa katika kuponya majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo na inahitaji hekima na busara katika kuhakikisha kuwa matukio ya namna hiyo hayajirudii tena."Lazima kuwe na utaratibu wa kuhakikisha kuwa chaguzi zijazo zinakuwa huru, za haki, zinazokubalika na zenye hali ya utulivu,"amefafanua.

Pia amesema kuwa,katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28,mwaka huu Chama cha ACT Wazalendo kilipata wabunge wanne na wawakilishi wanne kabla ya mwakilishi mmoja kufariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news