Benki ya NMB yavutiwa na Uchumi wa Buluu Zanzibar

Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamevutiwa na jinsi Benki ya NMB ilivyojipanga kushiriki katika shughuli za maendeleo visiwani humo na mchango inaoutoa kujenga uchumi imara wa kisasa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Wakizungumza wakati wa hafla ya Usiku wa Taarab Zanzibar siku ya jumamosi, viongozi hao walipongeza nia Benki ya NMB kufanya kazi karibu na serikali huku wakiahidi ushirikiano wa kutosha na benki hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alipowasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar kuhudhuria Taarab ya kumpongeza iliyofanyika Jumamosi usiku. Benki ya NMB ilikuwa ndiyo mdhamini mkuu wa taarab hiyo. Katikati ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zuberi Ali Maulid.

NMB inashiriki kuijenga Zanzibar kupitia huduma zake mbalimbali na tayari imejipanga kushirikiana na Serikali ya Dkt Hussein Ali Mwinyi kutekeleza miradi mbalimbali.

Akizungumza kabla ya burudani kuanza, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema benki hiyo si tu kuwa ina nia ya kusaidia maendeleo ya Zanzibar lakini pia ina msuli wa kuchangia kifedha.

“Benki ya NMB ina uwezo mkubwa kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati.Benki ina mezania ya zaidi ya trilioni 7 sasa, mtaji na ukwasi wa kutosha,” Bi. Zaipuna amefafanua na kuongeza kuwa NMB ni benki ambayo ina uwezo na iko tayari kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati. Mheshimiwa Rais, tumejipanga vyema kuwahudumia wananchi wa visiwani na kusaidia kutimiza maono ya serikali mpya,”ameongeza.

Usiku wa Taarab uliandaliwa rasmi kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ushindi wake wa kishindo. Hafla hiyo iliandaliwa na CCM Mkoa wa Mjini Magharibi huku NMB ikishiriki kama mdhamini mkuu.

Mbali na Dkt Mwinyi, viongozi wengine wakuu waliokuwepo ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah, na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zubeir Ali Maulid.

“Ushiriki wa karibu wa Benki ya NMB katika hafla hii ni kielelezo kingine tosha cha utayari wa kufanya kazi na Serikali hii na kushiriki katika maendeleo ya Zanzibar,” Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt Abdulla Juma Mabodi, aliwaambia waliodhuria.

“Tayari wana mchango mkubwa kwenye uchumi wetu. Sisi kama chama pamoja na serikali tunawapongeza kwa hilo na tunawashukuru sana NMB kuwa tayari kuchangia kwenye uchumi wa buluu,”ameongeza.

Baadhi ya wananchi wa Zanzibar wakishiriki katika hafla ya Taarab Maalum ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Mwinyi (hayupo pichani) wakijumuika katika taarab huiyo wakati Kikundi cha Culture kikitoa burudani kwa wimbo wake  “Mpewa hapokonyeki” ikiimbwa na Msanii Bi.Mgeni Khamis, iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar usiku wa Desemba 5,2020.

Naye Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Bw. Idrisa Kitwana Mustafa, amewaambia wanahabari baada ya hafla hiyo kuwa mchango wa NMB katika kuleta mageuzi ya uchumi wa bluu utakuwa wa msingi sana.

Maendeleo ya uchumi wa bluu ni moja ya ajenda kubwa za Serikali ya Awamu ya Nane. Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la 10 la Wawakilishi mwezi uliopita, Dkt Mwinyi aliahidi kuijenga Zanzibar mpya kwa kupitia uchumi wa kisasa wa bluu.

Kuhusu uchumi huo, Bi. Zaipuna alisema: “Benki ya NMB imejipanga kushirikiana na serikali kutimiza maono yake kwenye uchumi wa bluu na tayari tumeanza kwa vitendo. Wiki hii tumetoa elimu ya kuwajengea uwezo wavuvi, wakulima wa mwani na wavunaji wa chumvi.” Programu hii inalenga kuwafikia wananchi 2,000 itakapofika mwezi Machi mwaka 2021.

“Tukishawajengea uwezo, lengo ni kuanza kuwapa mikopo ya riba nafuu ya Fanikiwa ambayo huanza kwa kiwango cha chini cha shilingi 500,000 mpaka shilingi milioni 5,” Bi Zaipuna alifafanua. NMB pia ina shiriki katika maendeleo ya utalii wa Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments