Biteko ang’aka Mgodi wa North Mara kutokufuata Sheria ya 'Local Content'

Imeelezwa kwamba Mgodi wa North Mara umekiuka Sheria ya Ushirikishwaji wa Watanzania (Local content) baada ya kutangaza zabuni nje ya nchi na kupata mzabuni kinyume cha sheria za Madini, anaripoti Issa Mtuwa (WM), Mara. 
Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akimsikiliza mmoja wa Mameneja wa Mgodi wa North Mara, Hilaire Diarra akitoa maelezo kuhusu uhifadhi wa tope sumu (TFS), mwenye shati la kijani ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, kushoto kwa Waziri ni Mkurugenzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini , Dkt.Mwanga na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu Rais Muungano na Mazingira , Mwita Waitara. (Picha na Issa Mtuwa-WM).

Hayo yamesemwa Desemba 18, 2020 na Waziri wa Madini, Doto Biteko baada ya kufanya ziara maalum mgodini hapo. 

Kanuni za Madini (Ushirikishaji wa Watanzania), 2018 Tangazo la Serikali Na. 2/2018 zinataka wamiliki wa migodi kutangaza zabuni hapa hapa nchini na endapo hakuna Mtanzania mwenyewe sifa au vinginevyo, zabuni hiyo inatangazwa nje ya nchi na atakayepatikana atalazimika kushirikiana na Mtanzania. 

Waziri Biteko amesema, kwa mujibu wa sheria hiyo, mgodi utakaokiuka utatozwa adhabu ya dola za kimarekani milioni tano. Ameongeza kuwa, sheria hiyo inalenga kutoa fursa ya watanzania katika kushiriki katika masuala ya uchumi wa madini. 

Meneja Mkazi wa Mgodi wa North Mara, Hilaire Diarra amekiri kosa kutofuata sheria kwa kuwa walikuwa katika presha ya kutekeleza mradi huo. Diarra ameomba radhi na kwamba wapo tayari kufuata maelekezo yatakayotolewa na Serikali. 

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeo ya jamii (CSR), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amehoji kuhusu utekelezaji wake ambapo Meneja Mgodi anayeshughulikia Mahusino, Gilbert amesema wametekeleza kwa kujenga madarasa, kujenga visima vya maji na masuala ya afya japo Prof. Msanjila alimwambia hawajafuata utaratibu unaotakiwa katika kutekeleza miradi ya CSR. 

Kutokana na majibu hayo, Biteko ameuagiza mgodi kuandaa mpango wa utekelezaji wa miradi ya CSR na kuwasilisha kwenye mamlaka ya serikali za mitaa ili waipitie na kuidhinishwa tayari kwa ajili ya kutekeleza. 

Akizungumzia kuhusu masuala ya fidia, Biteko amesema wanaolipwa ni wale wenye haki akisisitiza kuwa utaratibu wa mtindo wa watu kutegesha hawawezi kulipwa fidia. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema, suala la fidia Nyamongo linacheleweshwa na wananchi kutokana na mchezo wa tegesha. Amesema, watu watakaobainika sheria itachukuwa mkondo wake. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news